Ajira mpya sekta ya Elimu - Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti hatujalipwa mishahara ya Agosti na Septemba

Ajira mpya sekta ya Elimu - Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti hatujalipwa mishahara ya Agosti na Septemba

A

Anonymous

Guest
Ajira Mpya katika sekta ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, tuliingia kazini na kuripoti Agosti lakini mpaka sasa tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kutolipwa mshahara wetu wa mwezi wa nane pamoja na mwezi wa tisa.

Tulipojaribu kwenda kuulizia makao makuu ya halmashauri, maafisa wa Idara ya Rasilimali Watu (HR) walitupa majibu mepesi sana wakisema taarifa zetu zilichelewa kuchakatwa (process) au mfumo umekumbwa na changamoto (collapse/hang).

Kinachotushangaza zaidi ni kwamba, katika mwezi wa tisa, kuna wenzetu kama wanne hivi waliopata mshahara, huku wengi wetu tukiwa tumebaki bila kulipwa chochote na bila kupewa namba za hundi (check numbers).

Tukijiuliza hawa wenzetu waliwezaje kupata mshahara wakati taarifa zetu zote zilitumwa kwa pamoja, hatupewi majibu ya kueleweka.

Suala hili la kucheleweshewa mishahara kwa ajira mpya limekuwa ni tabia na utamaduni unaojirudia mara kwa mara katika Halmashauri hii ya Serengeti. Kila awamu mpya ya watumishi wanaoripoti hapa lazima wapitie mateso haya haya ya kukosa mishahara kwa miezi miwili au zaidi.

Mkurugenzi anatambua kabisa kuwa hatujapata mishahara na baadhi ya watumishi walishawahi kumfuata. Hata hivyo, ushauri tuliopewa ni kwamba tukope fedha kwa watumishi wenzetu ili tuishi, jambo ambalo ni gumu sana kwa mazingira ya sasa kwa sababu kila mwalimu ana bajeti yake na hawezi kukukopesha kwa urahisi.

Sisi tunafanya kazi kwa bidii, tuna familia, tumeoa na tuna watoto wanaotutegemea, lakini hatujui hatima wala haki yetu. Tunaomba mamlaka za juu zitusaidie kuingilia kati ili kurekebisha idara hii ya HR ya Halmashauri ya Serengeti na kuhakikisha watumishi wapya wanapata stahiki zao bila kuwekewa vikwazo au majibu ya mizunguko.
 
Back
Top Bottom