SoC04 Akili bora, Tanzania bora!

SoC04 Akili bora, Tanzania bora!

Tanzania Tuitakayo competition threads

GianaAlbert

New Member
Joined
Jun 25, 2024
Posts
1
Reaction score
0
Khatib ni kijana mwenye umri wa miaka 27 aliyeweza kusoma na kuhitimu katika chuo kimoja jijini dar es salaan na kutunukiwa shahada ya uhandisi. Katika safari ya kuanza ajira yake na hapo aliweza kutumika katika kampuni isiyo ya kiserikali. Baada ya muda kadhaa Khatib alianza kuonyesha dalili za mgonjwa wa akili, alianza kwenda kazini bila kuwa nadhifu isivyokua kawaida yake. Wiki moja baadaye alianza kuokota takataka barabarani na kuongea mwenyewe. Ndugu waliamua kumpeleka kwa waganga na kwenye maombi wakiamini watu wabaya wamemroga kujana wao. Alipata ahueni kidogo lakini hali yake ilirudi na kuwa zaidi ya ya hapo awali iliyopelekea kijana huyu afungwe kamba nyumbani. Baada ya kuhangaika bila mafanikio walipata ushauri wa kumpeleka kijana wao hospitali ya afya ya akili Mirembe iliyopo Dodoma. Alipata matibabu na kufanya afya yake itengemae japo hakuweza kurudi kama alivyokua hapo awali. Daktari alisikika akisema “ laiti angalipata matibabu mapema angeweza kurudi katika hali ya kawaida na kurudi kazini bila changamoto yoyote.” Ndugu zake wakajibu kwa masikitikk “ Laiti tungalijua”

Utangulizi
Afya ya akili ni moja ya mambo muhimu kwa binadamu ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uwezo wa mtu kufanya kazi, kujifunza, na kuishi maisha ya kuridhisha. Hata hivyo, matatizo ya afya ya akili mara nyingi yanaeleweka vibaya na yamezungukwa na unyanyapaa. Kesi ya Khatib inaonyesha jinsi familia na jamii kwa ujumla wanavyoweza kushindwa kutambua na kushughulikia matatizo ya akili kwa wakati unaofaa.Huu ni mfano mmoja tuu kati ya mingi inayoendelea katika jamii yetu inayopelekea kupoteza nguvu kazi ya vijana katika taifa letu.

Afya ya akili imekua fumbo kubwa na hata pale linapofimbuliwa mapokeo yake bado hayajawa mazuri. Hii inanirudisha nyuma wakati VVU na UKIMWI ilikua ni janga kubwa sana lakini bidii ikafanyika juu ya elimu na sasa mabadiliko yanatupa faraja ya hali ya juu mno! Vivyo hivyo mabadiliko haya yanawezekana kwa swala hili tena la afya ya akili.

TANZANIA YENYE ELIMU SAHIHI JUU YA AFYA YA AKILI…INAWEZEKANA!!!

Je, tunawezaje kufikia kwenye matamanio yetu? Haya ni malengo kufikia maono yetu.

MALENGO YA MUDA MFUPI (miaka mitano)

Kuongeza kipengele cha afya ya akili kwenye kampeni za VVU na UKIMWI. Programu za ukimwi katika afya ni moja ya programu zinazofanya vizuri sana kutokana na ukongwe wake, ufanisi na mafanikio katika kazi. Ni vyema basi wanapokua wakifanya shuguli zao basi watoe pia elimu juu ya afya ya akili mfano; Baada ya ushauri nasaa kwa makundi ya wagonjwa wanaokuja kupima au kuendeleza matibabu, wakati wa bonanza za ukimwi ambapo wahisika wengi huwa vijana, wanapotembelea wahanga wa madawa ya kulevya na kwenye madangulo kwani takwimu zinaonyesha upo uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya vilevi na madawa na changamoto za afya ya akili.

Ndani ya miaka mitano ni dhahiri jamiii itakua imepata mwanga juu ya afya ya akili, hii inatupa matumaini kwenye kuifikia Tanzania tuitakayo.

MALENGO YA MUDA MREFU(miaka 25)

1. Ushirika kati ya sekta ya afya na sekta nyingine. Sekta ya afya haiwezi pekeake kuelimisha kila mtanzania lakini ushirikiano na sekta zingine kama sekta ya elimu, sekta ya sanaa, utamaduni na michezo, sekta na kilimo na sekta nyingine nyingi katika kutoa elimu juu ya afya ya akili mfano; mashuleni wanafunzi wanaweza kuwa na klabu zinazowapa elimu juu ya afya ya akili na namna ya kutunza afya ya akili binafsi.

2. Jitihada pia kutoka kwa mashirika mbalibali yasiyo ya kiserikali. Hii ni kuunga mkono jitihada za kutoa elimu kwa jamii juu ya afya ya akili. Pia kupambana na unyanyapaa na kuelimisha familia zilizoathiriwa na wapendwa wao kua na changamoto za afya ya akili.

3. Kuongezwa kwa wataalamu wa afya ya akili ambayo itasaidia upatikanaji wa huduma hizi hata katika vituo gya afya. Hiibiyawezekana kwa kupitisha uwekezaji kwenye kusomesha wataalamu wa afya ya akili ndani na nje ya nchi ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa wataalamu.

Hitimisho.
Ni vigumu sana kuondokana na tamaduni za kiimani kwani mafanikio hayaji kwa kuachana ghafla na tamaduni bali kwa kushirikisha tamaduni zetu na ujuzi wa kisayansi kufikia malengo. Kwa kusema hivyo,waganga wa jadi na viongozi wa dini wapewe hii elimu kwani nia yetu ni afya njema juu ya muumini huyu. Mgonjwa anaweza akapona kama mganga atamueleza mgonjwa kuja hosoitali hata kama ataendelea kupata huduma za kiganga au maombi kwa viongozi wa dini basi asiache kwenda hospitali. Sambamba na hilo; Kwa kutoa elimu bora na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya akili na kupambana na unyanyapaa, Tanzania yangu itaijenga jamii yenye uelewa mzuri wa afya ya akili na wenye kuwaji watu wote ikiwemo wenye magonjwa ya afya ya akili na kuleta matumaini kwa watu hao. Ninayo imani kubwa sana kwa njia hizi tutakua tumepiga hatua kubwaa kama taifa juu ya afya ya akili na tutaweza kutunza na kutumia nguvu kazi ya vijana wetu bila kuzidiwa nguvu na magonjwa ya akili. Vita hii ni yetu sote!TANZANIA YENYE ELIMU SAHIHI JUU YA AFYA YA AKILI…INAWEZEKANA!!
 
Upvote 4
Back
Top Bottom