Akili gani anayoipenda Mwenyezi Mungu?

Akili gani anayoipenda Mwenyezi Mungu?

Zacht

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2020
Posts
1,026
Reaction score
2,266
▪ Ni Nani Ulul Albab?

▪ Aliyejaaliwa Hikima, amepewa kheri nyingi

Mwenyezi Mungu anawapenda watumiao akili, au wenye kutia mambo akilini (Ulul Albab) . Hii ni kauli Yake katika Kitabu Kitukufu, Qur’an:

"Na wale wanaojiepusha kufanya ibada ya masanamu, na wakanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, habari njema (bishara njema) ni zao. Basi wape habari njema waja wangu hawa: Ambao husikiliza kauli (nyingi zinazosemwa), wakafuata zile zilizo njema. Hao ndio aliowaongoa Mwenyezi Mungu, na HAO NDIO WENYE AKILI. (Qur'an 39:17-18)

"(Mwenyezi Mungu) humpa hikima (akili yenye nafuu) Amtakaye, na aliyepewa hikima bila shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila WENYE AKILI.” (Qur'an 2:269)"

“Sema: “Hawawi sawa wabaya na wema, hata huo wingi wa wabaya ukikufurahisha (usimili katika wingi huo). Basi mcheni Mwenyezi Mungu ENYI WENYE AKILI ili mpate kufuzu.” (Qur'an 5:100)"

Katika Hadithi moja ya Mtume(S.A.W), watu walimsifu sana mtu kwa matendo yake ya ibada, Mtume, (S.A.W) akawauliza, “kwani huyo mtu ana akili kiasi gani?” Watu wakauliza, ‘ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi tunamsifu mtu kwa matendo yake, nawe unauliza akili yake?’

Mtume akasema “mpumbavu hupatwa na makubwa kwa upumbavu wake kuliko mchafu anavyopatwa na ya kupatwa kwa machafu yake. Na Siku ya Mwisho watu watapanda daraja kwa akili zao.”

Hadith hiyo inaoana moja kwa moja na aya isemayo kuwa watakaonyanyuliwa daraja ni wenye elimu. Yafahamika kuwa elimu ndiyo kichocheo kikuu cha matumizi, makuzi na mawanda ya akili.

Elimu ndiyo inayopevusha akili na kuongeza thamani yake katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu anayeelimika huwa tofauti sana na Yule asiye na elimu.

Akili ni neema na ni sehemu muhimu mno ya utu wa mwanadamu. Katika matumizi ya kawaida, akili ndiyo inayomtofautisha mwanadamu na mnyama. Kama si akili, mwanadamu angelikuwa ni mnyama kamili.

Mwanazuoni mmoja amesema “Mwenyezi Mungu kawaumba Malaika na akili lakini bila matashi na matamanio; Kawaumba wanyama na matamanio lakini bila akili; na Kawaumba wanadamu na vyote viwili; akili na matamanio.

Hivyo basi, binadamu ambaye akili yake inatawala matamanio yake, huyo ni bora kuliko Malaika. Na binadamu ambaye matamanio yake yanatawala akili yake, huyo ni m-baya kuliko mnyama.”

Bila akili, utu wa mtu haukamiliki, na labda hata umuhimu wa kuwepo kwake duniani hupungua kwani ulimwengu hukosa faida naye. Kuna mifano mitano ya kuonesha upungufu wa mwanadamu kwa ukosefu wa akili.

Utoto: hili ni eneo la kwanza la upungufu wa akili wa mwanadamu. Mtoto huweza kufanya chiochote wakati wowote kwa sababu ya uwezo wake mdogo wa kiakili.

Ndiyo maana mambo ya mtoto hubezwa. Mtu mzima anapofanya jambo lisiloendana na umri wake hubezwa kuwa ‘hakui’ au ana ‘akili za kitoto’. Akili ya utoto ni akili isiyoambatana na tafakuri, ni akili isiyoweza kupima matokeo ya maamuzi.

Mtoto huweza kushika moto kwa sababu akili yake imeshindwa kujua matoleo ya uamuzi wa kushika moto. Watu wazima wengi walikuja kujutia baadae yale waliyoyafanya utotoni!

Kwa sababu hiyo, hata uamuzi wa kufuata dini ya haki wa mtoto husubiri mpaka apevuke kiakili. Mtoto ana msamaha, na ana pepo ya moja kwa moja kwa sababu ya upungufu wa akili yake. Hajajenga akili au akili yake haijajengeka.

Wazimu: hili ni eneo la pili la upungufu wa akili ya mwanadamu. Mwendawazimu ni mtu aliyepungukiwa na kiasi kikubwa cha utu wake kwani mambo anayoyasema au kuyafanya huwa hayastahili kufanywa na binadamu wa kawaida.

Maisha ya Mwendawazimu ni maisha yanayotengwa na jamii yake. Si mtu anayefaa tena katika jamii. Ni uhai unaokuwa umebakia kwake lakini kuendelea kwake kuishi ni sawa na kuendelea kupoteza thamani yake.

Katika hukumu za Uislamu, mwendawazimu haandikiwi tena amali. Kalamu imesimama. Na ndio kusema hafungwi tena na wajibu wa ibada. Baadhi ya magonjwa ya akili, wakati mwingine hupona, na wakati mwingine ndio basi tena.

Katika mambo fulani, mwendawazimu anaweza kufanana na mtoto mdogo. Kama ambavyo mtoto mdogo anaweza kutembea bila kuvaa nguo, mwendawazimu naye huweza kufanya hivyo.

Uzee-ni eneo jingine la upungufu wa akili. Mtu aliyechoka kiakili kwa sababu ya umri uliopindukia, huweza kufanya mambo yasiyowakilisha akili timamu. Mzee huyu huweza kufanya mambo mithili ya mtoto. Huu ni umri dhalili ambao baadhi ya watu huufikia.

Uhayawani-hili ni eneo jingine ambalo huwajumuisha watu ambao wanazo akili timamu lakini wanafanya mambo yanayoakisi upungufu wa akili. Uhayawani ni matokeo ya mwanadamu kuipa nguvu zaidi silika yake ya kinyama hasa baada ya kuukataa mwongozo wa Mwenyezi Mungu.

Kama ilivyosemwa na mwanazuoni tuliyemnukuu hapo juu, uhayawani ni matokeo ya akili ya mwanadamu kutawaliwa na matamanio ya nafsi yake. Katika kundi hili wapo watu wanaofanya mambo ambayo saikolojia ya binadamu huyakataa.

Mathalani, mwanamke mwenye akili timamu anapojivua uke wake na kuubakisha nusu au utupu kabisa kwa hiyari yake, huyu ni hayawani. Maamuzi yake ya kuvaa ovyo au kutovaa hutokana na nguvu ya silika yake ya unyama.

Thamani yake hushuka huku jamii yake ikiaminishwa kuwa kujisitiri au kutojisitiri kwake ni uhuru wake, na si uhayawani wa kukemewa! Mwanamke huyu huwania na kugombea taji la kutembea uchi hata mbele ya macho ya wazazi wake achilia mbali watu baki!

Kwa jina la Umiss fulani, ameweza kuionesha dunia nzima maungo yake ambayo mwanamke mwenye akili zake hawezi kuyaonesha. Lakini si mwanamke tu, bali hata mwanaume ambaye zipu yake huvuka hata kwa kitoto cha miaka miwili, huyu naye ni hayawani.

Lakini anamzidi hayawani kwani ng’ombe hamwendei ndama wa miezi miwili! Hili ni eneo baya sana la ukosefu wa akili kwani lenyewe ni la ufujaji wa makusudi wa akili.

Hiyo ni katika matumizi ya kawaida. Lakini kuna ufujaji katika matumizi makubwa zaidi ya Akili. Katika kiwango hiki, wapo wasomi wa shahada za msingi, uzamili na uzamivu ambao, kwa kiasi kikubwa, hutumia akili katika fani na taaluma zao lakini wao hao hao hukosa kabisa akili ya kufikia hitimisho la ukweli kuhusu maisha yao.

Ni ufujaji huu wa akili unaozaa hata ‘wakanusha Mungu’. Ni ufujaji huu wa akili unaomporomosha mtu mwenye elimu hadi kuwa chini ya wenye wasio na elimu katika eneo la itikadi.

Ni watu wa kawaida wangapi wanaomwamini na kumwabudu Mungu huku makumi, mamia kwa maelfu ya wasomi wakishindwa kufanya hivyo?! Athari za kumsujudia Muumba (sijida) huonekana kwenye mapaji ya uso ya watu wa kawaida huku mapaji ya madaktari wa falsafa yakikosa athari hizo kwa sababu eti hawaamini Mungu au wana mashaka na dini!

Sababu ya msomi kuahidiwa kunyanyuliwa daraja ni kwamba yeye angetangulia zaidi kifikra katika kumkubali na kumwabudu Mungu. Yeye angelikuwa na ushahidi mwingi zaidi wa elimu ya mazingira katika kujenga imani ya uhakika au yakini ya kumjua Mola Muumba.

Lakini yeye anapokuwa nyuma katika imani hiyo, au anaposhindwa kabisa kumuona na kumwamini Muumba, ni wazi atakuwa ameporomoka mno kutoka kwenye nafasi aliyopangiwa, na kuwa chini ya waliopaswa kuwa chini.

Akili ya msomi hufujwa kwa namna nyingi. Hufujwa pale inaposhindwa kuufikiria ukweli dhidi ya uongo. Uongo huo waweza kuja kwa sura ya siasa, dini, na kadhalika.

Akili ya msomi ingetarajiwa kutoa upinzani mkali dhidi ya mifumo ya kisiasa inayochipuka kwa msingi wa dhana ya kumkana Mungu. Siasa za dunia zimebuniwa na akili ya watu walioukataa ukweli kuwa ulimwengu ni kazi ya Mungu, na hivyo yeye ndiye Mwenye haki ya kuitawala dunia, na mwanadamu awe wakala tu wa mamlaka hayo.

Kwa kuwa siasa ya mwanadamu imejengwa juu ya msingi batili wa kukanusha ukweli kuhusu nafasi ya Muumba, kila kitu chake huchukua mkondo huo huo wa uongo. Siasa hizi za wanadamu hujaa uzushi, uongo na ghiliba ambazo huzidi kufuja akili za watu wakiwemo wasomi.

Ni katika mazonge haya ya kiakili, hata wasomi wa uzamivu hufungwa minyororo ya kisiasa na kuwa watumwa wa kiakili pale wanaposhindwa kufanya uchunguzi huru au utafiti makini wa kile wanachoaminishwa.

Wanakuwa sehemu ya wanyonge wanaoburuzwa na kuburutwa kwa minyororo ya uzushi na uongo hadi kuamini ndivyo sivyo huku jitihada za kuwakomboa zikikwazwa na hoja zao wenyewe za kuhalalisha utumwa wao wa kiakili. Hii ni aina mbaya sana ya utumwa.

Ni katika mazingira haya, uzushi na uongo huchukua sura bandia ya ‘ukweli’. Dhana za uadilifu na haki husinyaa huku dhuluma ikistawi.

Ni mahali pagumu sana pale ambapo watu wanasulubiwa kwa uzushi huku msomi aliyetarajiwa kuukataa uzushi akiamini bila tafakuri huru. Hayo ni matokeo mabaya ya ufujaji wa akili katika kiwango cha usomi.
Huenda hapa sasa ndipo panapotupa changamoto ya kuwasaka ma-ulul-Albab. Hawa ni watu wanaozitumia vizuri akili zao. Kama si mwongozo wa Qur’an, basi mwanadamu angeyatazama matumizi ya akili katika matunda ya fani zake za elimu tu.

Mwanadamu angetazama majengo marefu aliyojenga kwa akili yake, ndege alizounda kwa akili yake, kompyuta aliyounda kwa akili yake na kadhalika. Kwa kiasi kikubwa, angeitazama Amerika, Ulaya na hata China ambayo ni Mataifa yanayoweza kufanya chochote kwa uwezo wao wa kiakili.

Lakini Ulul-Albab hawapatikani huko. Si kwamba Muumba hapendi yaliyofanywa na wanadamu ulimwenguni bali anachukizwa na kushindwa kwa akili zao kuutambua ukweli kuhusu Yeye Muumba.

Imani juu ya Mwenyezi Mungu na utii kamili Kwake ndiyo chimbuko la afya ya akili ya mwanadamu. Bila imani hii, mwanadamu hawi timamu japo anazo akili kichwani. Bila imani sahihi, mwanadamu haoanishi vipawa vyake vya akili na shukurani kwa Muumba.

Hujiona mkamilifu asiyehitaji mwongozo wa Muumba. Jeuri hii ndiyo chanzo cha ufisadi ndani ya ulimwengu alioujenga na kuupamba kwa akili yake. Ulul-Albab ni jamii ya wanadamu wanaotia akilini ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu.

Wenye yakini iliyojengeka juu ya msingi wa elimu sahihi iliyochanganya ujumbe wa Manabii na maarifa ya mwanadamu. Wenye akili ni wale wanaosumbuka kujibu swali la Nani yuko nyuma ya Maumbile ambayo mwanadamu ameyakuta na kuyatumia.

Wenye akili ni wale wanajihoji kuhusiana na wapi walikotoka na wapi wanakokwenda? Wenye akili ni wale wanaofanya jitihada zote katika kuliendea na kulifikia lengo la kuumbwa kwao.

Hawa ni watu adimu, na historia imeshuhudia uchache wao katika zama za kila nabii. Hawa ni wale waliokwenda kulia ilihali ulimwengu mzima ulikwenda kushoto!

Hawa ni wale waliokataa kusema ndiyo mahala pa siyo. Wameachana mbali kiakili sio tu na maadui wa fikra zao bali hata na marafiki wa fikra zao walioikubali imani sahihi kama wao.

Upeo wao wa akili umewatofautisha na jamii kubwa ya walioamini na waliokadhibisha. Si rahisi wao wenyewe kujitambua wala watu wengine kuwatambua.

Nidhamu yao ya kuyahoji-hoji maumbile muda wote ili kupata jawabu la uhakika la wao ni Nani na wako hapa duniani kwa ajili gani ndiyo inayotawala akili yao.

Tafakuri yao ya kila Neno la Muumba ndiyo inayojenga akili yao, na kunoa vipawa vyao. Hawaitengi akili ya ubunifu wa sanaa ya dunia inayopamba na kurahisisha maisha yao bali wanaijumuisha akili hiyo na akili ya kumtambua Mola wao ili sanaa hiyo iambatane na shukurani kwa Muumba wao.

HAO NDIO ULUL ALBAB.

"Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasio tumia akili zao."
Quran 10:100

Ctrl+c & Ctrl+v
 
Back
Top Bottom