Watani habari gani, nawasalimu jamani,
Kumi na moja i ndani, nakuja na hizi ghani,
Limenijia kichwani, wazo hili si utani,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijelengesha tungua!
Nimemuona mtini, ndege kweli chakarani,
Ana mbwembwe kama nini, na rangirangi mbawani,
Sijui ni wa Kingoni, Anaimba kama nini,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijilengesha, chukua
Kafumba macho tawini, na kawimbo mdomoni,
Ndege wenzake mtini, wamenyamaza kwa soni,
Anabadilisha tyuni, kama kasomea fani,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijilengesha pasua
Mwindaji akaja chini, na manati mkononi,
Kaangalia mtini, achague ndege gani,
Mwenye kelele mtini, akamlenga jamani,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijilengesha, kamua
Mara Puh! Ndege chini, wenzake wako angani!
Kisu kikambusu shingoni, kisiwe kibudu jamani,
Kanyonyolewa majini, akatundikwa motoni,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijilengesha nyanyua!
Ndipo nikaja amini, chunguza kwanza mtini,
Yule anojiamini, huimba sana tawini,
Ni kitoweo mtani, cha maakuli jioni,
Ndege akilia sana, karibu kutunguliwa!
Akijilengesha tumbua!
Na. M. M. Mwanakijiji (BGM) Sauti ya Kijiji
Siko kifani zaidi,ni hoja kuhusu ndege,
Ninayo yangu miadi,kama alivyo moringe,
Wengi wao makuwadi,kutaka wote waige,
Kama hoja ni ya ndege, mie nachagua bata,
Bata ndo namchagua, ndiyo wangu modeli,
Bila ya kuchakachua,kwa utulivu ni kweli,
Pakata ukidadua, pachika kwa baisikeli,
Kama hoja ni ndege, mie nachagua bata,
Mandege yako mengi, bundi njiwa kunguru,
Sijui wewe kitegi, ulimpata maguru,
Tumia hata ulegi,usije pata udhuru,
Kama hoja ni ndege,mie nachagua bata,
Utatungua wangapi,katika miti mingapi,
Usije pata makapi,kwa kuzani ni kopi,
Hoja yako ndio ipi,nipe nikupe tipi,
Kama hoja ni ndege, mie nachagua bata,
Pakata kwa raha zako, baada ya kumuoka,
Manati kitu ni chako,ya nini kukukuruka,
Huitaji mulengo wako,usije pata sumbuka,
Kama hoja ni ndege,mie nachagua bata,
Ni wewe mwanakijiji,ulezoea porini,
Kwetu yapo majiji, hewala i kibindoni,
Nenda mpaka ujiji,bata mpaka sebureni,
Kama hoja ni ndege,mie nachagua bata,
Ngoja niweke koma,bata wangu nimpakate,
Asije pata ukoma,kisha nimpe mate,
Nisije mwaga tama,kuku waule wote,
Kama hoja ni ndege,mie nachagua bata,