Kamanda wa Polisi wa Pwani, Ali Nuno, ametoa onyo kali kwa wanasiasa wanaodaiwa kufadhili makundi ya wahuni (goons), akisema kuwa serikali haitaendelea kutoa ulinzi kwa viongozi watakaobainika kutumia au kufadhili makundi hayo kutekeleza vitendo vya vurugu.
Akizungumza na wanahabari, Nuno alisema ulinzi wa serikali umetolewa ili kulinda viongozi wanapotekeleza majukumu yao ya umma, si kuwapa nafasi ya kufadhili au kutumia wahuni kuvuruga amani na kuhatarisha usalama wa wananchi.
Aidha, aliwasihi wanasiasa kuendesha siasa za ustaarabu kwa kuzingatia misingi, sera na hoja zenye manufaa kwa wananchi badala ya kutumia vijana kama nyenzo za kusababisha machafuko au kuendeleza siasa za vitisho.
Nuno alisisitiza kuwa Kenya ni kubwa kuliko mtu yeyote, hivyo viongozi wote wana wajibu wa kuweka mbele maslahi ya taifa, kuheshimu utawala wa sheria na kulinda amani na mshikamano wa nchi.
Kauli yake inajiri wakati mjadala kuhusu matumizi ya makundi ya wahuni katika siasa ukiendelea kushika kasi, huku Wakenya wengi wakitaka viongozi kuwajibika na kuhakikisha siasa zinaendeshwa kwa amani na heshima kwa sheria.