PreGE2025 Aliyekuwa katibu mkuu wa NCCR- Mageuzi ajiondoa kwenye chama hicho

PreGE2025 Aliyekuwa katibu mkuu wa NCCR- Mageuzi ajiondoa kwenye chama hicho

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla)

Sijapewa username bado

JF-Expert Member
Joined
Aug 15, 2024
Posts
1,775
Reaction score
2,891
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kawe katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kupitia chama hicho, Bi. Martha Raphael Chiomba, ametangaza rasmi kujiondoa ndani ya NCCR-Mageuzi.

Katika barua rasmi aliyoiwasilisha hivi karibuni kwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, na ambayo Jambo TV imebahatika kuiona, Martha amesema sababu binafsi ndizo zilizopelekea kuondoka kwake.

“Hivyo kwa barua hii, nakujulisha kuwa kuanzia tarehe ya leo yaani 26/04/2025 nimejiondoa rasmi kuwa Mwanachama wa NCCR-Mageuzi kwa sababu binafsi”, ameeleza Martha katika barua hiyo huku akiwashukuru WanaNCCR kwa ushirikiano wao katika kipindi chote alichokuwa pamoja nao.

Hatua hiyo ya Martha imeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wadau wa siasa, ambapo wengi wamehusisha uamuzi wake na migogoro inayoendelea kufukuta ndani ya chama hicho cha upinzani kwani inakuja siku chache baada ya Mwenyekiti wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shabani Itutu, kuwapokea viongozi wengine waliokuwa waandamizi ndani ya NCCR-Mageuzi kutoka mikoa mbalimbali.

Hivi karibuni, Itutu alipokea wanachama hao wapya akieleza kuwa, "kujikita kwetu katika kuimarisha demokrasia na usawa kwa kila mwananchi ndiyo sababu ya kuwa kimbilio la wengi."

Miongoni mwa waliopokelewa katika mkutano huo wa wanahabari walikuwa ni Dk. Saganda Khalid Saganda, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Shinyanga na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa; Michael Makene, aliyekuwa Katibu wa Wilaya ya Ilemela na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa; pamoja na Michael Leiser, aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa wa chama hicho. Ramadhani Amrani Mrisho, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mwanza, Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama, naye alikuwa miongoni mwa waliohamia ADC.

Kwa sasa, NCCR-Mageuzi inaongozwa na Mwenyekiti wake Haji Ambari Khamis, huku Makamu Mwenyekiti akiwa Joseph Selasini. Katika mwelekeo wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, chama hicho kimepitisha jina la Haji Khamis kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Joseph Selasini kuwa Mgombea Mwenza.
1745928155540.png
 
Back
Top Bottom