Amuoe binti yupi?

Amuoe binti yupi?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
Asalamaleko malenga, magwiji mlobobea,
Wa kijiji nimetinga, na swali nawaletea,
Ninyi mlioko Tanga, Dodoma na hata Mbeya,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Kijana kanijongea, moyoni ametatizwa,
Anataka kuongea, ameshachoka kubezwa,
Nikamwambea sogea, mbona mwana unalizwa,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Babu mimi nimechoka, maisha ya ukapera,
Nimechoka natamka, zimenishinda papara,
Yaamin Mwabudika, naomba zako busara,
Kati ya hawa watano amuoe binti yupi?

Katika zangu safari, nimewakuta watano,
Hata ng'ambo ya bahari, nimewanasa kwa neno,
Muda sasa ni tayari, nimeyapata maono,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Wote kwa sura wazuri, maumbo wamejaliwa,
kwa nje sioni shari, macho yao kama njiwa,
Sijakiona kiburi, sababu nikavutiwa,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Wa kwanza ndiye Rehema, mzuri kwa kila kitu,
Tatizo ni kulalama, utadhani debe patu,
Hachoki kusemasema, utadhani yeye fyatu,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Yupo na dada Regina, msomi amebobea,
Tatizo lake ni pana, nimeshindwa kuzoea,
Mitaani sana sana, kutwa yuko kutembea,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Maria yeye wa tatu, kajaliwa biashara,
Mchoyo wa kila kitu, ni mwepesi wa hasira,
Roho yake ina kutu, na hachelewi kufura,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Wa nne ni Honorita, chakaramu na mcheshi,
Hucheka unapomwita, tatizo lake ubishi,
Hubisha hata kwa ndita, mpaka patafuka moshi,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Wa tano nakutajia, Kokuguna wa Bukoba,
Mapenzi kanipatia, tena siyo ya kibaba,
Tatizo nawaambia, Uvivu kwake si haba,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Kijana kamalizia, na kichwa akatikisa,
Mabinti kanitajia, kila mmoja ana kosa,
Shauri kaulizia, yupi awe mke hasa,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Kaditamati na tama, kiti changu nakikunja,
Kijana namtazama, nadhani huyu mjanja,
Mabinti amewasema, na wote keshawaonja,
Kati ya hawa watano, amuoe binti yupi?

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Mapenzi tumeshasema ni yao watu wawili
Hili walijua vyema hata wenzetu tumbili
Kijana kashasema wake undumilakuwili
Babu mate tema muache afie urijali

Mzee uepuke lawama simshauri dhalili
Asiefunzwa na mama dunia itamsaili
Kijanae wa zahama sio mwana wa adili
Babu mate tema muache afie urijali

Ngono zembe yachachama kijana wala hajali
Iweje babuwe salama umshauri mkejeli
Au hujui pima mwoaji wa kiziraili
Babu mate tema muache afie urijali

Muoaji alie mwema hataonja kuwili
Hatatafuna vijimama ili kumjua mwali
Katu hataila nyama maana si ibilisi
Babu mate tema muache afie urijali
 
Back
Top Bottom