Muhoni John (25), anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Serengeti kwa tuhuma za kumwagia maji ya moto mkewe, Naomi Lucas kwa madai ya kuchelewa kumpikia chakula.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema leo Jumanne Oktoba 20, 2020 kuwa mkazi huyo wa kitongoji cha Nyansirori kijiji cha Rwamchanga wilayani Serengeti alitenda jambo hilo jana Oktoba 19, 2020 na kisha kumfungia ndani mkewe ambaye aliokolewa na majirani leo. Amesema Naomi amelazwa hospitali ya wilaya kwa matibabu.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Thomas Twani amesema baada ya kupata taarifa walikwenda nyumbani kwa mtuhumiwa na kumkuta akiwa na sime kiunoni.
“Tulipewa taarifa na majirani baada ya kufika tulimnyang’anya sime na tulimuona Naomi. Mtuhumiwa ana wake wawili mmoja alienda kuchunga mifugo huyu majeruhi akabaki kwa shughuli za nyumbani.”
“Saa tano asubuhi akaulizia chakula na Naomi akamwambia ndiyo anashughulikia kwa kuwa maji yalikuwa yameishachemka, wakati anafuata unga yeye akachukua maji na kumwagia mgongoni hadi kwenye makalio,” amesema.
Amesema kuwa baada ya tukio hilo akamfungia ndani bila huduma na hakupewa chakula, “majirani walisikia kelele na asubuhi mmoja akawa anasikia mtu anaugulia maumivu alipouliza mke mwenzake akaficha, hata hivyo akalazimika kutaka ukweli ndipo akatoa taarifa.”
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya, Daniel Safi amekiri kumpokea majeruhi, “anaendelea na matibabu,” bila kueleza ukubwa wa jeraha alilonalo.
[emoji2398]Mwananchi