*ANGA LA WASHENZI II -- 24*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Hapa kwenye vurumai ya watu, sasa akageuka kuwa chui aliye mawindoni, jicho lake lilimwagukia Chong Pyong lisimwache. Na baada ya muda mfupi akawa amemtia mkononi. Akamzimisha na kutoka naye kwa kupitia emergency door.
ENDELEA
Baada ya muda mfupi Lee akawa amefanikiwa kufika na Chong Pyong mahali alipoweka makazi, akamlaza hapo na kwenda kuoga kuondoa uchovu. Alipomaliza akakumbuka kuwa hakuchukua chakula, akashuka chini kuendea.
Aliporejea akakuta kitanda kitupu! Chong Pyong hakuwapo. Hamaki kugeuka nyuma, mara kiti kikarushwa kwanguvu kumfuata. Haraka akakwepa, kiti kikakita ukutani na kuvunjika.
Chong Pyong akajaribu kurusha mateke na ngumi, lakini hakuwa na mafunzo ndani yake, hakuweza kufua dafu kwa Lee, akatulizwa punde na kujikuta sakafuni akiugulia maumivu.
Akamuuliza Lee yeye ni nani na nini anahitaji kwake? Lee akamwambia ingekuwa busara kama angemuuliza kabla hajaamua kumshambulia. Lakini kwa wakati huo, Chong Pyong akadhani aidha Lee ni afisa wa polisi, na basi kama sio, atakuwa jambazi aliyetumwa amuangamize.
Basi akaanza kujitetea akijieleza yeye hana makuu na mtu. Anacharaza zake gitaa tu kwa ajili ya kuingizia kipato familia yake na si kingine. Kama haitoshi, akaendelea kubwabwaja kwa hofu, akasema mpaka mengine ambayo Lee hakuwa na haja nayo.
Kwa maelezo hayo Lew akatambua Chong Pyong alikuwa mtu wa aina gani. Mpenda starehe na anasa. Alafu pia ni mwongomwongo.
Basi akamtaka anyamaze. Yeye hayupo hapo kwa ajili ya kumdhuru ila ana shida na mtu mmoja tu ambaye anafahamu atakuwa na taarifa zake, naye si mwingine bali Chen Zi!
Chong Pyong akatoa macho kusikia jina hilo. Kwa sekunde kidogo akatulia akimtazama Lee kwa uso wa maulizo. Akamuuliza Lee yeye ni nani? Lee akamjibu shabiki mpenzi wa Chen Zi. Chong Pyong akamtazama tena kwa sekunde kama tano pasipo kunena kitu.
Mosi, kuna kitu alikuwa anafahamu. Pili, kuna kitu alikuwa anaogopa. Mara akatikisa kichwa akasema, Chen Zi ni mfu. Hana taarifa zozote juu yake.
Lee akamdaka shingo na kumbamizia ukutani, alafu akamning'iniza kwa mkono wake mmoja akitazama uso wa Bwana huyo ambao ulijawa na vipuli.
Akamwambia kwa sauti ya chini, hana masikhara naye. Na hapo walipo ni ghorofa ya kumi, haoni soni kumtupia nje akajifia endapo asiposema anachokihitaji. Tena haraka asimpotezee muda. Ni nini kilimuua Chen Zi?
Basi bwana yule akiwa amekabwa kwanguvu asiweze hata kuhema, akapambana kunena huku jasho likimchuruza. Lee akamwachia avute hewa akiwa amempatia dakika moja tu kueleza, la sivyo waendelee na zoezi!
Chong akavuta hewa kwa pupa huku akikagua shingo yake. Baada ya sekunde kadhaa, akamtazama Lee kwa macho yake mekundu. Akameza mate. Akasema hajui kitu. Kitu pekee ajua ni kuwa Chen Zi alizidisha dozi ya madawa ya kulevya.
Lee akamdaka tena shingo na kumbamiza ukutani! Mara hii hakumkaba, akabadili zoezi, akadaka moja ya kipini puani mwa Chong Pyong, akakinyofoa kwanguvu. Damu zikaruka! Chong Pyong akapiga kelele kali za maumivu.
Ila Lee hakukoma, wala hakumwongelesha, akadaka kipini kingine kwenye nyusi ya Chong Pyong, nacho akakivuta kwanguvu, damu zikachuruza!
Chong Pyong akalalama kwa maumivu. Lee, sasa mkono wake ukiwa umejawa damu, akadaka tena kipini kingine cha Chong Pyong, sasa cha mdomoni, Chong Pyong akapaza sauti, nasema! Nasema! Uso wake ukiwa umejawa na damu.
Lee akamwacha na pasipo kuongeza neno, akamtazama kwa macho yenye kiu na neno. Basi Chong Pyong akavuta kwanza pumzi kisha akasema kuwa Chen Zi hakufa kwa madawa, bali aliuawa na watu wasiojulikana. Akasema anaamini watu hao walikuwa ni wapinzani wake kimuziki.
Lee akamuuliza, sasa ilikuwaje vyombo vyote vya habari nchini na vya kimataifa vikatangaza kuwa amekufa kwa kuzidisha dozi ya madawa ya kulevya? Chong Pyong akahema kwanza. Kisha akamwambia Lee kuwa huo ni mchezo tu ulipangwa kwani Chen Zi alipewa sumu, na alipopoteza fahamu, wakamvutisha madawa na kuacha baadhi mezani mwake, mpaka mauti kumkuta.
Lee akashangazwa na hiyo taarifa. Akamuuliza bwana huyu, aliyajuaje hayo, na kwanini hakuchukua hatua kuripoti huo ukweli?
Chong akabanwa na kigugumizi. Akajitetea alikuwa anaogopa pengine angefanya hivyo, watu hao wangemuwinda na kummaliza. Aliamua kunyamazama kunusuru roho yake.
Na kitendo cha kwamba alijuaje, alipata kushuhudia hayo yakitukia. Hapa Lee akamuuliza swali jingine, hao wauaji akiwaona ataweza kuwatambua kwa kuwatazama?
Kabla Chong hajajibu, simu yake ikaita mfukoni. Hapa wakatazamana kwa sekunde kama tatu. Lee akazamisha mkono wake mfukoni mwa Chong na kutoa simu. Ilikuwa ni iphone 8 rangi ya fedha. Akapokea na kuweka 'loud speaker', kisha akamuwekea Chong Pyong mdomoni.
Sauti iliyotoka simuni ilikuwa ni nzito. Na mara moja ilimuuliza Chong yupo wapi muda huo? Chong akalaghai yu mgahawani. Sauti ikauliza tena wapi amefikia kwenye lile swala la yule jamaa anayemtafuta Chen Zi?
Hapo Chong Pyong akabanwa na kigugumizi. Alimtazama Lee wakakutana jicho kwa jicho. Lee akamkazia ndita na kumpa ishara aendelee kuongea na simu.
Chong Pyong akasema bado hajafanikiwa, kisha akakohoa mara tatu. Mara simu ikakata. Lee akaelewa kile kikohozi kilikuwa ni ishara.
Na sasa akatambua kuwa Chong Pyong alikuwa ana mengi ya kumjuza. Kwa namna moja ama nyingine ni adui anayemtafuta. Akamuamuru ampatie nywila za simu yake. Hili swala likawa gumu kidogo kwa Chong Pyong.
Lakini baada ya Lee kunyofoa vipini vyake vitatu, akashindwa kustahimili maumivu, akatoa nywila, Lee akafungua simu na kuzama ndani. Akaingia Facebook na kukuta Chong Pyong akitumia jina la Chen Zi!
Akaelekea kwenye kona ya ujumbe, huko akakuta 'conversation' kati yake na Chong Pyong akiigiza kuwa Chen Zi! Kumbe Chong alikuwa miongoni mwa wale watu ambao Lee aliwaomba anwani na wakampatia kisha Lee alipoitafuta akaishia kujikuta katika nyumba ya yule kikongwe mjane!
Kama haitoshi, kumbe Chong Pyong alikuwa anawasiliana na wale Chen Zi wengine wote ambao Lee aliwasiliana nao na kisha wakampatia anwani ya uongo!
Kwanini Chong Pyong anatumia jina la Chen Zi huko Facebook? Kwanini na wenzake wanayatumia majina hayo? Na kwanini walimlaghai?
Kabla hajapata majibu ya maswali hayo, Lee akaamini kuwa Chong Pyong atakuwa anahusika na mauaji ya Chen Zi halisi, kwa namna moja ama nyingine! Kwanini walimuua? Na hao ma - Chen Zi wengine ni wakina nani?
Akamkaba Chong Pyong na kumwamuru amueleze kila analolijua, la sivyo atanyofoa roho yake ndani ya sekunde moja tu! Aliminya mishipa ya koo la Chong mpaka mwanaume huyo akatoa ulimi nje, macho yakitumbuka!
Alipomwachia, akadondoka chini akipapatika kuhema! Lee akamwambia ana sekunde tatu tu za kusema, la sivyo ataendeleza zoezi na mara hii hatalisitisha kamwe mpaka atakapogeuka kuwa mfua
Mara wakiwa hapo, Lee akasikia vishindo vizito mlangoni mwake. Vilikuwa vya watu waliotoka kukimbia kisha wakasimama ghafula!
Vishindo hivyo vilipokoma, sauti nzito zikaulizana. Lee akatambua hapo si salama. Ndani ya sekunde tatu mbele, mara mlango ukavunjwa na wanaume watatu majabali wakaingia ndani wakiwa wamebebelea bunduki mikononi. Miongoni mwao alikuwapo yule jabali mweusi aliyepewa agizo la kumtafuta Lee.
Wakatazama huku na kule, hawakumwona mtu zaidi ya Chong Pyong aliyekuwa amelala chini akihema kama bata. Kutazama dirishani, wakaona li wazi, Lee alikuwa ametoroka kwa kutumia shuka!
**