JOANA ANAONA KITU USIKU --- 05
Simulizi za series inc.
ILIPOISHIA…
Uso wa mama ulikuwa na kielelezo kilichompa walakini, kuna jambo halikuwa sawa.
“Moa, umechukua bangili kule kwenye kisanduku chumbani?” Mama aliuliza.
Moa akajikuta anaishiwa nguvu kabla hata hajanena.
ENDELEA…
“Nakuuliza umechukua bangili yangu kule chumbani?” mama akarudia kuuliza.
“Hapana,” Moa akajibu akitikisa kichwa.
Mama akakwapua mkono wa Moa na kuuminya kwanguvu.
“Niambie ukweli, Moa. Kuna bangili yangu imepotea, na baba yako amesema hajachukua. Ni nani kama si wewe?”
“Sijachukua, mama,” Moa akasimamia msimamo wake. Alijua fika kama angelikubali basi yangelimkuta makubwa.
Mama akabadilika rangi akawa mwekundu kwa hasira. Macho yake meupe yakaanza nayo kuwa mekundu kana kwamba anataka kulia.
Moa akaogopa sana. Akajua siku hiyo anauawa.
Ajabu mama yake asifanye jambo, akanyanyuka na kwenda zake. Basi usiku mzima Moa akawa macho akihofia kwamba mama yake anaweza kurejea na kumuadhibu, pengine ameenda kuteka kitu cha kumuadhibia.
Alikuwa anatetemeka, ila mpaka asubuhi hakuna kilichotokea.
Zikapita pia siku na miezi miwili. Moa akasahau kabisa yale ya bangili. Filipe alihama shule hivyo hakuwepo hata wa kumkumbusha.
Siku moja aliingia ndani ya chumba cha mama yake baada ya kuagizwa akachukue kiasi fulani cha fedha juu ya meza kwa ajili ya kununulia vitafunwa.
Alichukua fedha hiyo, lakini akaona kitu kilichokamata macho na muda wake. Mara ya kwanza alihisi amefananisha ila alipotazama vema akagundua alikuwa sahihi, hakufananisha.
Ilikuwa ni ile bangili! Bangili aliyoiiba na kwenda kumpatia Filipe.
Kabla hajafanya jambo akili yake ikamrudisha nyuma na kuanza kumkumbusha yale yote yaliyotukia. Alivyompa bangili hiyo Filipe, msiba wa dada yake na maswali ya mama yake usiku pembezoni mwa kitanda.
Alikuwa kama vile amepigwa na bumbuwazi. Alishtuliwa na sauti ya mama yake ikimuita. Haraka akatoka ndani na kwenda.
Lakini tangu hapo akawa anawaza. Alifikiria sana kuhusu bangili ile chumbani mwa mama yake. Lakini binadamu tumeumbiwa kusahau, kadiri ‘masiku’ yalivyokatiza akasahau.
Ila sasa, habari hii inamjia akiwa mtu mzima anayejitambua. Tendo la mama yake kumfuata chumbani kuhusu bangili linajirudia kwa mara ya pili.
Uso wa mama yake uliobebelea ghadhabu na hasira juu ya bangili unarudi tena kwa mara ya pili. Mambo hayakuwa yamebadilika.
Sasa shaka lake juu ya bangili za mamaye linazidi kuthibitishwa na kuonekana lenye mantiki. Mama ana mahusiano na bangili hizi, tena mahusiano yenye afya bora. Lakini mahusiano haya ni mema kwa wengine?
Wale waliokuwa wanasema mama yake ni mlozi, je, walikuwa sahihi?
Alijihisi mtupu ndani ya nafsi yake. Alikaa nje kwa muda mrefu sana kabla hajaingia ndani ambapo aliendelea kuwaza.
Ni dhahiri usiku wake alikuwa anaenda kuumaliza pasipo kuonja kitanda.
Aliitazama bangili ile ya Joana, akajiuliza maswali mengi. Mwishowe akaamua kuchukua maamuzi. Aliamua liwalo na liwe lakini hawezi kumrudishia Joana bangili ile.
Alimpenda sana na hakuwa radhi kuona anateseka.
Alipanga kuitupilia mbali bangili hiyo ama kuiteketeza kabisa, alafu atamdanganya mama yake kwamba ameirejesha.
Lakini mama hatagutukia uongo huo? Alijiuliza. Potelea mbali, nitakuwa nishaiteketeza! Akapiga moyo konde. Hapo sasa akalala japo ni vidakika vichache kabla jua halijachomoza.
Alikuja kuamshwa kwenye majira ya saa sita mchana na kaka yake akapate chakula.
Akaamka kichovu, akanawa uso na kwenda kula. Huwa wanakula kifamilia, kwahiyo mezani hukutana wote.
“Mbona kulala mpaka saa hii?” mama aliuliza. Uso wake ulikuwa unatazama sahani lakini macho yake yakiwa kwa Moa.
Moa akasita kujibu. Alitafuta jibu sahihi kwanza baada ya kufikiria kwa sekunde kadhaa:
“Nimechoka.”
“Ulikuwa unafanya nini usiku?” mama akauliza.
“Nilikuwa nasoma,” Moa akajibu. Mama akanyamaza na kuendelea kula mpaka mwisho pasipo kusema kitu.
Baadae kwenye majira ya saa tatu usiku, Moa akiwa amebebelea ile bangili ya mama ya mama yake, akatoka na kwenda karibu kabisa na maeneo ya baharini, mahali fulani penye jengo ambalo halikuwa limekamilika.
Humo ndani akawasha moto na kuitupia bangili ndaniye. Akasimama na kutazama bangili hiyo inavyoteketea, ikiupamba moto na kuupa rangi ya bluu.
Akahakikisha bangili hiyo imekuwa majivu kabisa na moto umekwisha, ndipo akatoka kurejea nyumbani.
Huko akamkuta kaka yake anayemfuatia akiwa peke yake. Alikuwa ameketi sebuleni akitazama mpira kwenye televisheni.
Hakumwongelesha, akashika njia aende zake chumbani. Ila punde akaitwa.
“Mama amezidiwa, amewahishwa hospitali,” kaka yake alimpasha habari. Akashtuka.
“Muda gani?”
“Muda si mrefu. Wameniacha hapa nitazame nyumba.”
“Tatizo nini?”
“Hatujajua nini tatizo. Baba alistaajabu amedondoka chini na kuanza kuweweseka. Haraka wakampakia kwenye gari na kumwahisha hospitali.”
“Hawajakupa taarifa yoyote mpaka sasa?”
Kaka akatikisa kichwa na kubinua mdomo. Moa akaenda chumbani na kuketi kitandani. Kichwa chake kikifura mawazo.
Alihusanisha ugonjwa wa ghafla wa mamaye na kuchomwa kwa bangili, akaona vinaendana kabisa. Sasa afanyeje? Ina maana atakuwa amemuua mama yake kwa kuchoma bangili?
Aliona kuna haja ya kumjulia hali mama yake kabla ya chochote, basi akachomoa simu yake mfukoni na kumpigia baba yake. Baada ya muda mfupi simu ikapokelewa. Baba akamwambia mama anaendelea vema.
“Muda si mrefu tutarudi nyumbani,” alihitimisha kwa kusema hivyo kisha simu ikakata.
Moa akashusha pumzi. Sasa alijua mama yupo salama, lakini yeye je? – atakuwa salama? Mama akirudi atafanya nini? Atagundua kuwa amechoma bangili ile?
Japokuwa alikuwa anapiga moyo wake konde, ila aliamini kabisa mama yake atakuwa amejua kilichofanyika.
Alijikuta akitetemeka mwili kana kwamba yupo uchi kwenye kanda baridi. Meno yaligongana na vidole vilisinyaa. Ndani ya tumbo alihisi kuna donge fulani la moto linakatiza na kumsugua.
Hakupata amani.
Alikaa hivyo mpaka pale mama, baba na kaka yake wa kwanza waliporejea toka hospitalini. Mama alikuwa hajiwezi hata kuongea, walimpitisha na kwenda kumlaza ndani chumbani moja kwa moja.
“Wamemchoma sindano, alikuwa kama vile amewehuka kwa namna alivyokuwa mkorofi,” kaka mkubwa alimwambia Moa. “Alikuwa anakutaja mara kadhaa, akiapa kukuua!”
Moa akajua sasa vita imeanza rasmi. Akapata mashaka sana kuhusu uhai wake. Aliona ni vema sasa akashirikisha familia juu ya tatizo lake hilo. Mficha maradhi kifo humuumbua.
Akamuita baba na kaka zake, kisha akawaeleza yale yote yaliyojiri. Akaeleza kwa hisia sana, macho yake yakiwa mekundu, akisaga meno.
Ajabu, hakuna aliyemuamini wala kumpa uzito uliostahiki. Waliona ni kama anaunganisha ngonjera kuleta hadithi fulani ya kusisimua, hadithi ambayo imeshachosha masikio ya wasikilizaji.
“Wote tunajua matatizo aliyo nayo mama yako tokea zamani. Namna gani alivyonusurika kuuawa kwa kudhaniwa ni mlozi, kisa tu asili ya macho yake. Tulipigana sana kumpa moyo japokuwa lilimuathiri kisaikolojia, leo hii unakuja na kutaka kumuondolea hata ile nguzo moja aliyobaki nayo?” Baba alinguruma.
Wote wakamuunga mkono na kumwacha Jona mpweke.
“Kama angelikuwa mlozi usingelikuwa hai hata leo, angekwishakumaliza zamani za kale!” kaka mkubwa akajazia.
Pasipo kujua maongezi hayo yote yalikuwa yanamfikia mama aliyekuwa chumbani amejilaza kitandani.
Mama akaapa kummaliza Moa kabla hakujakucha.
MOA ATAPONA?
NINI HATMA YAKE INGALI FAMILIA HAIPO NAYE?
NINI MADHARA YA KUCHOMWA BANGILI? JOANA ATAKUWA HURU?
Usikose sehemu ijayo.
Simulizi za series
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app