*ANGA LA WASHENZI II -- 31*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Gari hili lilikuwa ni Nissan Patrol rangi nyeupe. Vioo vyake vilikuwa vyeusi usiweze kuona ndani. Punde gari hilo likazimwa na mwanaume mmoja akatoka ndani.
Akalisogelea lile gari lililowaleta Miranda na Marwa.
ENDELEA
Akalikagua na kisha akarudi kwenye ile Nissan Patrol waliyokuja nayo. Ndani ya muda mfupi wakashuka wanaume wanne, wote walikuwa wamevalia nguo nyeusi kuanzia juu mpaka chini. Nyuso zao hazikuwa za kuvutia, bali kutisha.
Walikuwa na miili mipana wakionyesha waja wa shari. Na wasiwe na papara, wakaegemea gari lao na kungoja kwanza muda. Mmoja wao, ambaye alikuwa dereva, akatoa simu mfukoni na kupiga.
Ikaita mara mbili kabla haijapokelewa.
"Yes, boss. Tumewakuta ... ndio, sawa ... tutahakikisha hatufanyi makosa."
Kisha akakata simu na kuidumbukiza mfukoni. Alikuwa ni nani huyo aliyeongea naye? Najua bila shaka unadhani ni Sheng. Hujakosea. Ndiye yeye, lakini alijuaje 'move' hii ya Miranda na BC?
Turudi nyuma kidogo, si mbali sana, bali usiku wa kuamkia leo.
Baada ya taarifa kufika kwake kuwa wamevamiwa, watu kadhaa wameuawa na pia kusababisha hasara kubwa, Sheng hakufurahishwa kabisa na hili. Alikuwa mwekundu kwa hasira, na kwa mkono wake wa kulia akawamiminia risasi wanaume kumi waliokuwa wanahusika na lindo.
Ilikuwa awamalizs wote ila jamaa yake akamsihi asifanye hivyo maana itakuwa hasira ya samaki kujitumbukiza mtegoni. Atamaliza nguvu kazi ambayo bado ingemea matunda.
Lakini haikuwa rahisi hata kidogo kwa Sheng kuwabakizia uhai. Ilibidi mawazo mbadaka yatumike kumshawishi kwamba bado adui anaweza kutiwa mkononi. Hajatokomea kama alivyowaza.
Kwa kuwa, maadui hao waliowavamia waliiba chemical ndani ya maabara basi ni wazi watakuwa washirika wa Jona wakihaha kumtafutia ahueni. Kwahiyo, moja, Jona yu hai.
Na basi kama watu hao watakuwa wana ujuzi wa kemia, watatambua kuwa chemical waliyoichukua, haitakuwa suluhisho, bali kipande chake. Kwa hivyo, watataka kukamilisha antidote. Hapo watatafuta kipande kilichokosekana.
Na kwa mawazo ya haraka, sehemu ya kuipata ni MSD. Watege hapo, watawakamata wahitaji wao. Watu waliowatia hasara kubwa. Watu watakaowasaidia kumpata Jona na kummaliza 'for good'.
Ila likatoka onyo toka kwenye kinywa cha Sheng. Kama mpango huo hautafanikiwa, kama mpango huo hautamea matunda, basi atamwaga damu za wale wote aliotaka kuwamaliza pasi na simile.
Hivyo, ndiye wewe uliyetumwa hapa kuhakikisha unafanikisha kazi, ukitambua kuwa roho yako ipo rehani, utafanya mzaha?
"Itawachukua kama dakika tano tu kufika mahali wanapopataka," alisema Dereva akitazama saa yake ya mkononi. "Kwa makadirio mepesi, baada ya dakika ishirini, inabidi tujiandae. Haijalishi watatokea wapi, ila lazima watarejea kwenye chombo chao cha usafiri."
Huyo dereva aliponyamaza, alimtazama mmoja wa jamaa aliongozana nao, pasipo kusema neno, jamaa huyo akafungua mlango na kutoa begi jeusi, ndani yake akatoa kifaa fulani cheusi chenye umbo la duara.
Akasonga karibu na gari la wakina Miranda, akalala chini na kupachika kifaa hicho uvunguni. Alafu akakibonyeza tip! ... tip! Ikasikika sauti kama ya kitu kinachozunguka kwa kasi, kisha ikanyamaza.
Jamaa huyo akanyanyuka na kurejea garini. Yule dereva akanyoosha mkono wake ndani ya gari, akatoa kifaa kipana mithili ya tablet. Akakibofya bofya mara tatu, mara kiooni ikaonekana ramani, na mahali pale palipokuwa gari la wakina Miranda.
Kumbe walikuwa wameliwekea 'tracking chip'. Sasa hata gari hilo litakapoenda popote pale wataliona na kulifuatilia vema.
Ikapita muda kidogo wakakwea gari lao na kusogea mbali kidogo na hilo eneo.
**
Ndani ya Bohari ...
Miranda akatoa ishara ya mkono, Marwa akasimama upesi akimtazama kwa umakini. Mwanamke huyo akachungulia, akaona mwanaume mmoja aliyevalia ovaroli la bluu na kofia, akikatiza.
Mwanaume huyo alipoyoyoma, Miranda akampa ishara Marwa, wakaendelea kutembea.
Majengo haya yanayohifadhi dawa, yalikuwa yamepangwa katika mistari kana kwamba bweni. Na kila jengo lilikuwa lina milango miwili, mmoja mbele, mmoja nyuma.
Miranda alikuwa anafahamu ni jengo gani wanaliendea, walishayavuka mawili, na lile moja kabla ya la mwisho ndilo alilokuwa analitaka.
Basi wakaendelea kunyata. Walikuwa makini maana si tu walinzi ndiyo waliokuwepo humo, bali pia na baadhi ya wafanyakazi, ambao wengi wao walikuwa wamevalia ovaroli na kinyago cha kuziba pua na mdomo.
Hawakuwa wengi, ila kikwazo kikubwa kilikuwa ni mataa yaliyokuwa yanamulika huku na kule. Mataa makubwa yenye nguvu ya mwanga.
"Tutaingia mule ndani," alisema Miranda akinyooshea kidole jengo la mbele. "Nadhani unajua cha kufanya. Kama kawaida, hatuna muda wa kuchomesha!"
Miranda akachungulia tena, njia ilikuwa nyeupe, akachoropoka haraka akitembea asitoe kelele. Alipofika jengoni, akatazama nyuma. Alikuwa amemwacha Marwa. Upesi akampa ishara ya kumtaka aje.
Marwa akachungulia, kulikuwa shwari. Akatoka mbio, ila akiwa katikati, akajikwaa na kudondoka chini. Akaguna kwanguvu kwa maumivu maana alidondokea sakafuni.
Kishindo chake na sauti ya kugugumia, ikamshtua mmoja wa wafanyakazi wa Bohari aliyekuwa amesimama kwa mbali, akiwa kwenye bomba akinawa mikono yake.
Akatazama na kumwona Marwa akijinyanyua. Akapata shaka. Uso wa Marwa ulikuwa umefunikwa na barakoa. Na hata nguo alizokuwa amevaa, hazikuwa zile za walinzi wala wafanyakazi.
Basi akasonga karibu na lile jengo, akibeba kila tahadhari pamoja naye. Aliposimamisha masikio yake, akasikia lango likifunguliwa, na pia sauti ya watu wawili wakinong'ona.
Akapata shaka zaidi. Kwa hofu, asije jitia hatarini zaidi, akachomoka mpaka kwenye kibanda cha walinzi akatoa taarifa kuwa kule ameona wezi, wamevalia barakoa na nguo nyeusi. Wanazama ndani ya ghala pili toka mwisho!
Ndani ya kibanda hicho cha walinzi, kulikuwa kuna walinzi takribani watatu. Mmoja mwanamke. Mezani kwao kulikuwa kuna bunduki mbili kubwa kuukuu, daftari na virungu viwili.
"Wana silaha?" Akauliza mlinzi akitoa macho kana kwamba pera.
"Niliyemwona mikono yake ni tupu," akasema yule mfanyakazi, na pasi kupoteza muda, wakatoka walinzi wawili waliobebelea silaha, wakaongozana na bwana yule aliyewaletea silaha.
Wakasonga mpaka eneoni.
Walipofika wakanyamaza na kutumikisha masikio yao. Hawakusikia jambo. Wakatazama mlango, ulikuwa umetenguliwa kufuli. Hapa wakaamini wamevamiwa.
Basi wakatumia mafunzo yao ya kijeshi, wakazama ndani ya jengo na kutanguliza midomo ya bunduki. Wakaangaza, hawakuona kitu!
"Wako wapi?" Akauliza mlinzi mmoja akipepesa macho yake makubwa.
Punde, wakasikia sauti huko nje, ya yule bwana aliyekuja kuwapasha habari,
"Wale kulee!"
Basi haraka wakatoka ndani na kwenda huko nje. Yule bwana akawaelekeza, kule mbali kwenye makontena. Ameona kitu huko. Basi walinzi wakakimbilia huko upesi.
Sekunde tano mbele ...
"Twende," sauti ya Miranda ikasema kwa kunong'ona. Kumbe hawakuwa kule ambako walidhaniwa wapo. Ulikuwa ni mtego. Walikuwa wapo nyuma ya jengo walilotoka kukwapua walichokifuata, na walitazama wale walinzi wanapoelekea.
Wakatoka hapo mafichoni, na haraka wakakimbia kwa muda wa sekunde kumi na tano, Miranda akadanda ukuta na kujivuta juu. Akamvuta pia na Marwa wakadondokea nje ya eneo la Bohari!
Hawakupoteza muda, wakaendea usafiri wao. Wakakwea na kutimka.
Sekunde kumi mbele ...
Gizani ndani ya gari, kifaa kikawaka na kuonyesha 'tracking chip' ikiwa inatembea. Dereva akaguna puani. Kisha akasema,
"Wameshatoka.
Gari likawashwa na taratibu likaanza kusonga.
**