Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

bro stive popote ulipo agiza soda unywe kisha tuma story nakuja kulipa
 
*ANGA LA WASHENZI II -- 40*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Basi wale wavamizi, wakahesabu mpaka tatu, wakazama ndani kwa kuvunja mlango kwa mateke yao mazito.

Wakaangaza huku na kule. Hamna kitu! Ila bado ile sauti ya kike ilikuwa inasikika.

ENDELEA

Wakatazamana kwa duwazo. Kisha wakiwa wamebebelea silaha zao, wakasonga kwenda mavyumbani. Wakapekua kivita, hawakuona kitu! Ila mule chumbani sauti ilipokuwa inatokea, wakaukuta mdoli kitandani.

Aaagh!

Mdoli ulikuwa umerekodiwa na kuachwa hapo ucheze wenyewe. Wote wakakusanyika na kuutazama mdoli huo. Ulikuwa ni wa kike, nywele ndefu za kupendeza na macho makubwa yenye nyusi ndefu.

Nyuma ya mgongo wake alikua ana kitu fulani kigumu. Wakamfunua nguo na kumtazama. Ilikuwa spika! Basi bwana yule aliyemshikilia mdoli huyo akasonya na kumminya huyo mdoli kwa mkono wake mpana.

Yule mdoli akasinyaa na kuvunjika. Ila baada tu ya sekunde nne, wakaanza kukohoa mno. Kumbe yule mdoli alitoa hewa fulani na hiyo hewa kwa upesi ikasambaa ndani ya kile chumba.

Hao mabwana wakakohoa sana. Wakatoka ndani ya chumba wakiwa wanajikokota wakipaliwa na kikohozi. Hata macho yakawa mekundu kwa kukohoa!

Hawakupata wanachokitaka, na zaidi wakapata matatizo. Walijikokota mpaka kwenye gari yao wakazama ndani. Wakaendelea kukohoa sana kiasi cha kushindwa kuongea.

Baada ya dakika kama kumi, bado wakiwa hapohapo hawajaenda popote, angalau wakapata ahueni. Wakamweleza yule dereva kuwa mule ndani hamna mtu! Hawajamwona yoyote yule na huenda kabisa likawa tego. Walengwa wao watakuwa waligutuka mapema kuwa watakuja kuwatembelea.

Basi dereva akaleta ubishi. Akawauliza kama kweli walipekua vema. Wale mabwana wakasema walitazama kila eneo na walichokiambulia ni mdoli tu kitandani ukiwa umerekodiwa sauti!

Sasa kukawa hamna namna. Ikabidi waende zao, wale mabwana wakiendelea kukohoa sana na sana.

**

Basi zikapita kama dakika chache. Ndio, ni chache si nyingi, Miranda na Marwa wakawa wamezama ndani ya jengo lao ambalo lilitoka kupekuliwa muda si mrefu.

Walifika katika kile chumba, kile ambacho kilikuwa na mdoli, Miranda akamwokota yule mdoli chini akitabasamu. Akamtazama Marwa na kumwambia kwamba mpango wao umeitika. Kile walichokipanga kimezaa matunda.

Wasipoteze muda, wakaondoka hapo isijulikane wameenda wapi.

**

Baada ya mlango kuita mara moja tu, Shao akafungua na kukutana na kikohozi cha watumishi wake. Hata ndani hakuwakaribisha akawauliza kwa pupa imekuwaje?

Wakamweleza ya kuwa kule hawajapata kitu chochote, zaidi wameambulia maradhi! Shao afanye nini zaidi ya kukasirika?

Alikasirika mno, akang'ata meno yake na sasa akaridhia na akili yake kwamba maadui zao watakuwa walishatambua kuwa watatembelewa.

Sasa afanyaje? Akajiuliza. Akawataka wale watu waende zao wamwache afikiri na kupanga lingine. Asubuhi na mapema atawajuza namna ya kufanya.

Basi wale wajakazi wakaenda zao.

***

Hali haikuwa nzuri kabisa kwa usiku huu mzima. Wale mabwana wanne walikohoa sana na hawakupata nafasi haya ya kufumba macho kufurahia lepe la usingizi.

Walikohoa mno. Kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo walivyozidi kukohoa, mwishowe wakakosa pumzi na kujifia!

Yani kama vile mchezo. Mpaka jua linachomoza kesho asubuhi yake, watu hao wakawa wamekauka kaukau!

Maiti zao zilikakamaa kama mibuyu! Shao akapewa taarifa na akaenda kuwaona kabla hawajawazika. Akatahamaki na akasihi mwili mmoja ubakizwe kama sample watazame ni nini kiliwakumba.

Baadae walipofanya hivyo, wakagundua kuwa watu hao walikuwa wamevuta hewa mbaya ya ukaa. Mapafu hayo yalikuwa meusi kama mkaa na koo lao la hewa lilikuwa limetobokatoboka!

Hapa Shao akatambua kuwa hata wale wakina BC wako vema kwenye 'chemical weapon'. Ilimpasa awe makini zaidi.

Ila kama kuna kitu ambacho alikuwa anaridhia na nafsi yake ni kwamba hajashindwa vita.

Bado ana uwezo wa kumpata na kummaliza Jona. Cha kufanya ni kuja tena na mpango mwingine. Na sasa anatakiwa kutumia sana maabara kumaliza kazi yake.

**

Majira ya kumi na moja jioni ...

Shao alizama maabara na kuvalia mavazi yake ya kazi. Koti jeupe na maski ya kubana pua na mdomo, pia na glovu za mikononi kujilinda.

Akatumia kama masaa matatu akiwa humo maabara. Alikuwa peke yake. Na macho na mikono yake ikafanya kazi barabara kuitikiwa wito akili yake. Alichukua hiki akachanganya na kile, kile akachanganya na hiki na mwishowe akajikuta anapata kimiminika cha kijani iliyokolea.

Akakitikisa na kukitazama kikiwa ndani ya tube. Kukihakiki, akatwaa panya watatu wakubwa, na mmoja wao akamminyia kemikali hiyo mwilini akitumia bomba la sindano.

Yule panya akadumu kwa sekunde moja, mara akaanza kutapatapa akimimina damu. Na isichukuwe muda akafa! Ila hata baada ya kufa, Shao hakumtoa, badala yake akaendelea kuwatazama wale panya mpaka zilizopohitimu dakika tatu.

Hakuona mabadiliko! Akasonya. Si hicho alichokuwa anataka. Basi akamtoa panya yule aliyekufa kisha akawabakiza wale wawili.

Akarudi tena kwenye 'experiment' zake na baada ya punde akawa amepata mchanganyiko mwingine ambao ulikuwa ni wa kijani kupitiliza hata kuelekea kuwa nyeusi!

Akaifyonza na bomba la sindano na kumdunga panya mmoja, kisha akatulia na kuangaza.

Yule panya akadumu kwa sekunde tano tu, na tofauti na yule wa kwanza, huyu hakutapatapa kabisa, alidondoka chini ghafla baada ya moyo kusimama!

Ila Shao hakumtoa na badala yake akaendelea kumtazama panya huyo. Na kama vile dakika moja, yule panya mwingine ambaye hakuwa amedungwa kemikali, akaanza kudhoofu! Alianza kuyumba kama chombo kiendacho mrama, na mara akadondoka na kufa!

Shao akatabasamu. Sasa alikuwa amepata anachokitaka.

**

Majira ya saa mbili usiku ..

Kwa huku nje kulikuwa kumetulia tuli. Ni hatua tu nzito za walinzi hapa na pale ndizo zilikuwa zinasikika.

Ni hapa karibu na ofisi ya Sheng.

Taa za ndani ya ofisi zilikuwa zimezimwa kuashiria hakuna mtu humo ndani. Ila ...

Ni kama vile ungetulia vema ungesikia sauti za watu kwa mbali. Labda ungewaza ni masikio yako ila ndani ya muda mfupi sauti ya kitasa ilijita, na mlango ukafunguliwa kistaarabu akatoka bwana mmoja aliyekuwa amevalia nguo nyeusi kama walinzi wengine wazungukao eneoni.

Bwana huyo alitoka kwa tahadhari, na baada ya punde akanyanyua miguu yake kutokomea.

Lakini ...

Huyu bwana hakuwa mgeni machoni petu. Kama kumbukumbu zi vema, huyu bwana ni mmoja wa wale wateuzi kumi wa bwana Shao kwa ajili ya kazi yake. Sasa nini alikuwa anafanya ofisini kwa Sheng tena wakiwa kizani?

Vilevile taa ikiwa haijawashwa, mule ndani ya ofisi ya Sheng, simu ya mezani ikanyakuliwa na kupachikwa sikioni kisha punde sauti ya Bwana Sheng ikauliza kama aongeaye naye ni makao polisi.

Baada ya hapo, akatoa taarifa ya kwamba Jona anashikiliwa na mwingereza bwana Brown Curtis hivyo wakafanye msako kwenye nyumba yake haraka iwezekanavyo!

Aliposema hayo akapachika simu mezani. Tulipata kutambua hilo kwa sauti, kisha akaketi na kusema kwa lugha ya kichina, acha tuone nani atakayekuwa ndege wa alfajiri.

**
 
Noma sana , bila shaka Stive utaongeza antidote, homa imekuwa Kali sana hii.
Nasubilia ingine.
 
Acha picha iendeleee[emoji91][emoji91][emoji91] naona sheng vita imemshinda na kaamua kurudisha usukani serikalini
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…