*ANGA LA WASHENZI -- 67*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Punde simu yake ikaita. Alikuwa ni Kamanda. Akajiuliza anataka nini? Alipopokea Kamanda akamuuliza kama amesikia ya Boka.
"Ndiyo nimetoka kuona kwenye habari," Jona akajibu.
"Ok," Kamanda akaitikia. "Sasa hiyo kazi nimekupatia uifanye. Nataka huyo muuaji apatikane. Sawa?"
Kimya.
"Sawa?"
"Sawa, mkuu!"
ENDELEA
"Utaonana na Inspekta Geof, atakupatia alipofikia."
Baada ya hapo Kamanda akampatia Jona namna ya kumpata Inspekta Geof, alafu akakata simu.
Jona akaweka simu yake kando na kuanza kuitafakari simu hiyo ya Kamanda. Akatafakari na kazi aliyopewa. Hakuwa na kitu kichwani na hakuwahi kujisumbua na Boka.
Ndio alikuwa anajua mwanaume huyo ni waziri ila hakuwahi kumfuatilia wala kuwa shabiki wake. Kwanini mkewe auliwe? Akabinua mdomo.
"Huwezi jua ya wanasiasa!" Akajipa pumziko kwa kauli hiyo kisha akapuuzia. Lakini hakudumu muda mrefu, akili yake ikamrudisha tena kwenye hilo tukio.
Vipi kama haya yakawa ni mwendelezo wa mauaji ya watu mashuhuri na maarufu kama ilivyokuwa hapo nyuma? Akawaza.
Inawezekana Boka akawa ameingia kwenye Anga lile la Washenzi? Alifikiri sana lakini akajitahidi tena kupuuzia apumzishe kichwa.
Aliamini atakapokutana na Geof atajua wapi pa kuanza kutia mguu wake. Akanyanyuka na kujipatia chakula akishushia na juisi ya embe.
Kabla hajalala akaamua kushika kitabu kikubwa cha riwaya apate kupitia kurasa kadhaa kuhadaa kichwa alale. Alikuwa anasoma riwaya iitwayo THE BIG SLEEP cha mnamo mwaka 1939 kilichoandikwa na mwandishi nguli Raymond Chandler.
Riwaya hii ilikuwa ni ya mambo ya kijasusi. Ndivyo ambavyo Jona anapenda kuvipitia pale apatapo muda. Vitabu vya kufikirisha akili. Vitabu vya kuchemsha ubongo na kupanua mawazo.
Mbali na hiki cha Raymond Chandler, pia kwenye maktaba yake kulikuwa na vitabu vingine maarufu vya kijasusi vilivyoandikwa kwa mkono mtamu na akili zilizopevuka.
Kuvianisha kadhaa vilikuwa kama: THE HOUND OF THE BASKERVILLES cha mwaka 1902 kikiandikwa na Arthur C Doyle, THE MOONSTONE cha mwaka 1868 kikiandikwa na Wilkie Collins na cha bwana Dashiel Hammett kiitwacho THE MALTESE FALCON cha mwaka 1930.
Ingawa vitabu hivi vilikuwa vya kale, ila vilikuwa na thamani ya kusomwa tena na tena. Haswa kwa watu wa kariba ya Jona, wapendao kudadisi, kufuatilia na kupembua.
Kweli, baada ya muda wa dakika kadhaa Jona akiwa amesogeza karatasi kama kumi hivi, akaanza kusinzia. Mwishowe akalala kabisa.
Leo akawa anauendea usiku pasipo kutumia kilevi. Akalala kwa muda wa nusu saa tu, kabla hajakurupushwa na simu. Akalalama sana.
Alikuwa ameshapotelea usingizini. Alikuwa anafahamu ni namna gani atahangaika kupata nafasi hiyo tena. Na kwa mawazo yake yote alijua Kamanda ndiye aliyemtafuta.
Akasonya akiivuta simu na kuitazama. Alikuwa ni Marwa! Akawaza anataka nini muda huo? Akapokea simu.
"Yes,Marwa ... niko poa, wewe? ... yah nlikuwa nshalala ... bila samahani ... sasa hivi? ..." Jona akatazama saa kwenye simu, ilikuwa saa tatu usiku na dakika kichele, akairudishia simu sikioni. "Ok, basi nakuja."
Punde akanyanyuka na kuvaa, akaenda zake.
Akiwa njiani kwenda huko, sie twende huku ...
"Kwahiyo umeamuaje sasa?" Aliuliza shoga yake Glady akimtazama mwenzake kwa macho ya mtindio wa urembo. Mwanamke huyu hakuwa mwingine bali yule aliyebananishwa siku ile na Alphonce ndani ya gari, akajichafua na mkojo.
Alikuwa amevalia tight nyekundu na blauzi nyeusi isiyo na mikono. Kandokando yake bibie Glady alikuwa bado amevalia taulo anajikwatua kabla ya kwenda kazini.
"Sasa shoga yangu, niamue nini sasa hapo unadhani?" Akauliza Glady akipaka wanja. "Mtu mwenyewe ndo ashakufa hivyo. Sasa mimi si kaniachia mzigo tu hapa!"
Kukawa kimya kidogo. Glady akauvunja:
"Yani mimi hapa ndipo ninapokereka na maisha. Unajikinga na UKIMWI eeeeenh miaka nenda rudi kutumia marambo alafu unakuja kuuawa au kufa ka siku ka moja tu!"
Akasonya.
"Ila mwanamke wewe una bahati sana!" Shoga akamwambia. "Yule jamaa kama asingekufa alikuwa anakuua wewe nakwambia!"
"Aanzie wapi?" Glady akajivuna akipakaa rangi ya mdomo. "Kama alishindwa nilivyokuwa naye chumbani angeniwezea wapi?"
"Haya, bana! Mie sina neno. Niuzie basi hii simu," Shoga akapendekeza akiitazama simu ya marehemu Alphonce.
"Ishia hapo hapo!" Glady akamkemea. "Huoni choo ukapita?"
"Sasa shosti ya nini na mtu mwenyewe keshajiendea kwa mola wake? We sema hapa nikupatie laki moja unipe!"
"Fala kweli wewe. Laki moja unampa nani labda? Umeona simu ya laki moja hiyo?" Akamtazama Shoga yake. "Eti?"
"Unataka shingapi sasa?"
"Sitaki chochote we bwana we!" Akasema Glady akimalizia kujipara. Akajipulizia marashi na kujiveka nguo, gauni jeusi la lawama mtaani.
Akaketi kitandani.
"Hiyo simu itanipa pesa zaidi ya hiyo, tena mara kumi yake!"
"Wapi sasa?"
"Tatizo wewe akili yako tope. Nishapata wazo hapa mwenzako. Wazo la kupiga pesa ya maana niache kuuza uchi."
"Wewe hata upate milioni utauza tu. Iko damuni!"
"Ebu skiza nyoko wewe n'kupe mawazo ya maana, acha kuongea mashudu. Hizo picha zilizokuwepo humo ni pesa. Cha kufanya tunawatafuta wanaohusika na picha hizo tunawaambia watoe pesa tukae na siri, la sivyo mambo kweupee mitandaoni."
"Mh! Wakikataa?"
"Unaona sasa? Tatizo lako wewe unadhani kila mtu ananuka shida kama wewe. Watu wana pesa zao bwana. Unadhan mke wa mbunge, au mke wa waziri atakubali picha zake za uchi zisambazwe?"
Shoga kimya.
"Ohoo!" Glady akasimama. "Ngoja nkuonyeshe nitakavyotajirika mbele ya macho yako."
Akavaa viatu akamtaka mwenzake anyanyuke waende.
**
Baada tu ya kuketi, Marwa akamwambia usiku huo umekuwa wa kipekee kwani kuna mambo kadhaa muhimu amepata kuyadukua toka kwenye zile links, akaona si mbaya akamshirikisha kwenye taarifa.
Jona akakaa tenge apate kusikia. Marwa akiwa amemsogezea tarakilishi yake, akamwonyesha Jona jumbe kadhaa toka katika hizi pande. Hazikuwa na maana sana, ila moja.
Jona akatabasamu. Ujumbe huu ulikuwa umeanishwa kama ifuatavyo:
*From : Second Wave, Nairobi.*
*To: First Wave, Dar.*
*Content: Help for an ambush for killing and framing*
*Place: Karen and Langata.*
*Aim: Kamau Githeri and Wachuku Otieno.*
*Time: immediately!*
Ujumbe huo ukawapa mawili, mosi wakatambua 'nguvu moja ya bahari' ipo Dar na ya pili ipo Nairobi. Hii kumaanisha huko kuna matawi ya ulinzi yanayolinda kisiwa. Je, ya tatu itakuwa Dodoma? Hawakuwa na uhakika bali makisio.
Lakini pili na zito zaidi ni mpango wa kuuawa kwa viongozi wa kiserikali wa huko Kenya, bwana Kamau na Wachuku. Na si kuwaua tu, bali kufanya pia 'framing'.
Framing ni nini? Kwa kifupi ni zoezi la kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya mtu asiye na makosa (an innocent person) ili aonekane mkosefu mbele ya watu ama mahakama, ama kote.
Njia hii imekuwa ikitumika sana ulimwenguni na kuwatia watu hatiani kwa makosa ambayo hawajatenda. Kwa ustadi jambo linatengenezwa na kuhusanishwa na fulani huku mtendaji akibaki salama.
Na mtendaji huyu hufanya hivi kwakuwa huyo aliyemfanyia jambo na huyo anayesingiziwa kitaalamu kuwa yeye ndiye ametenda hilo jambo wakiwa wote ni maadui zake.
"Sasa tunafanyaje?" Akauliza Marwa.
"Inabidi tutoe taarifa kwa vyombo vya usalama vya Kenya," Jona akashauri.
"Kwa namna gani?" Marwa akauliza.
Hapo Jona akasita kidogo. Alifahamu jambo hilo litampatia shida kupata 'access'. Akafikiria sana namna ya kufanya, lakini kila njia aliyoipata haikumridhisha kwa umakini wake.
Mwishowe Marwa akamuuliza kama viongozi hao wana nyadhifa ya ubunge pia?
"Ndio," Jona akajibu. "Vipi kuna wazo umepata?"
"Haswa!" Marwa akamshauri waingie kwenye tovuti ya bunge la Kenya kisha kule wakapekue orodha ya wabunge na taarifa zao.
Jona akaafiki hilo wazo, wakazama mtandaoni na isipite muda wakawapata walengwa wao wanaowatafuta. Wakatazama 'additional info' wakapata akaunti ya barua pepe ya Kamau Githeri lakini kwa Wachuku Otieno wakaambulia patupu!
"Sasa ukimtumia barua pepe, haitachukua muda, ikakawia, mwishowe akauawa?" Jona akauliza.
Marwa akamtoa hofu, akamwambia atatuma barua pepe hiyo kwa njia ya kirusi bandia. Kama kawaida itafika kwa mlengwa, na kama huko atakuwa ameweka anti-virus itakuwa bora zaidi kwani itapiga kelele kumshtua.
Hivyo akasoma kwa wakati! Na kwa wakati huo bado simu yake ikibakia salama.
Jona akapenda hilo wazo. Na kwa upande wa Wachuku Otieno?
"Acha tuwasiliane na karani wa bunge kwa hizi namba walizozianisha kwenye tovuti," Marwa akapendekeza.
"Huoni itaweka taarifa zetu wazi tukitumia namba zetu binafsi?" Jona akauliza.
"Hapana," Marwa akamjibu. Akamwambia wataweka 'chip' kwenye mashine yake alafu atafanya kautundu wapige kwa 'private number'.
Wakafanya hivyo, ila hawakufanikiwa kumpata karani. Mwishowe wakaamua kutuma ujumbe wa kumtaarifu wakitumai atausoma kwasababu ya zile 'missed calls'.
***
- WATAFANIKIWA KUWAKOMBOA VIONGOZI HAO? KWANINI WAUAWE NA NANI ASINGIZIWE?
- JONA ANA MPANGO GANI WA KUMALIZA MAWIMBI YA SHENG?
- GLADY ATAFANIKIWA KWENYE UDHALIMU WAKE?
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app