Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI -- 68*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Huoni itaweka taarifa zetu wazi tukitumia namba zetu binafsi?" Jona akauliza.

"Hapana," Marwa akamjibu. Akamwambia wataweka 'chip' kwenye mashine yake alafu atafanya kautundu wapige kwa 'private number'.

Wakafanya hivyo, ila hawakufanikiwa kumpata karani. Mwishowe wakaamua kutuma ujumbe wa kumtaarifu wakitumai atausoma kwasababu ya zile 'missed calls'.

ENDELEA

Walipomaliza kazi hiyo wakatulia sasa na kufanya mambo mengine. Marwa akampata kumkaribisha Jona vitafunwa vya kusogezea muda huku wakipiga soga za hapa na pale.

"Umeonana na Panky leo?" Jona akauliza.

"Kiasi chake," Marwa akajibu akitafuna. "Ilikuwa ni asubuhi tukasalimiana na kuteta mambo kadhaa kabla hatujaachana."

"Kuachanaje?" Jona akastaajabu. "Hamfanyi kazi sehemu moja?"

Marwa akameza kwanza kabla ya kutia neno.

"Asubuhi nilipoongea naye aliniambia wanataka kumbadilisha kitengo, wamtoe SPACE BUTTON."

"Wampeleke wapi?" Jona akauliza.

Marwa akapandisha mabega. "Sijajua. Hatukuwa na muda wa kuongea naye sana kabla hatujaachana."

Jona akawaza kidogo.

"Haiwezekani wakawa wametambua na kuyatilia shaka mahusiano yenu?"

"Sidhani!" Marwa akawahi kujibu. "Huwa ni taratibu yao kubadilisha watu vitengo kila baada ya muda fulani. Ila ni kwa mara chache sana hutokea kwa SPACE BUTTON."

"Sasa mbona imetokea kwa Panky?"

Marwa akabinua mdomo. "Sijajua lakini nadhani ni kwasababu ya kifo cha mmoja wa wafanyakazi wa kitengo cha uhasibu kilichotokea hivi karibuni. Panky atakuwa amepelekwa huko kukaimu nafasi yake."

"Kwanini Panky, si mwingine?" Jona akaendelea kuuliza maswali.

"Unanifanya nijihisi nipo kituoni," Marwa akasema na kucheka. Jona naye akacheka.

"Anyways, kwa hisia zangu Panky atakuwa amehamishiwa huko kwasababu ya hali ya hewa. Ofisi ya huyo marehemu haikuwa na kiyoyozi kwasababu alikuwa na tatizo la asthma," Marwa akadadavua.

"Kwani Panky ana asthma?"

Marwa akacheka.

"Hana, ila aliigiza anayo. Imemgharimu sasa."

"Huyo marehemu ulijuaje ana asthma?"

"Ni mmojawapo wa wafanyakazi wa muda mrefu sana, actually nilimkuta akiwa hapo. Watu hawa wazamani wengi nawafahamu."

Jona akaridhika na maelezo haya Marwa. Lakini akapata wazo hapa, kama kweli Panky atakuwa amehamishiwa kwenye hiyo ofisi aliyosema Marwa, hamna namna akapata kuwatambua wanaume watakaotumwa Nairobi kusaidia Second wave?

"Kivipi?" Marwa akamuuliza Jona baada ya mwanaume huyo kumshirikisha wazo hilo.

"Watu hao hawaweza wakatumwa pasipo kupewa fedha za usafiri, makazi na kujikimu. Pesa zinatoka wapi?"

"Kwa mhasibu!" Marwa akajibu kisha akatabasamu. "Kweli inawezekana."

Hii ilikuwa hatua tamu sana kwa Jona kuwang'amua baadhi ya wahusika wa 'the first wave' na kisha kuwashughulikia.

Wakafanya mpango wa kumtafuta Panky lakini simu ikaita pasipo mafanikio.

"Ana mke, anaweza akawa anahudumia nyumba," Marwa akapendekeza wasitishe zoezi hilo. Jona akamsihi kesho asubuhi atakapokutana naye ahakikishe anamuuliza na kufanya namna.

Marwa akamtoa shaka Jona.

Wakapumzika sasa Marwa akimsihi Jona alale nyumbani kwake kwani muda umeshaenda.

***

Saa nne asubuhi ...

Gari Rav4 rangi ya damu ya mzee ilikuwa imepaki pembeni kidogo mwa njia itumiwayo na daladala kuingia ndani ya kituo cha daladala cha Makumbusho.

Ndani ya gari hiyo alikuwamo Inspketa Geof na Jona wakibadilishana ndimi. Geof alikuwa akimweleza Jona yale aliyoyapata toka kwenye ajali ya mke wa Boka, Jona naye akiuliza maswali kadhaa.

"Gari lilitokea kwa kasi huku stendi, Chaser nyeupe, ikikwepa daladala kwa pupa. Ilipofika hapo kwenye maungio ya barabara ya lami, ikasogea kidogo na kuibamiza gari ya marehemu kwa upande wa dereva! Kisha ikayoyoma," Geof alielezea hayo akitumia mikono yake kuonyeshea uhalisa wa matukio na mahali yalipotukia.

Akamweleza pia Jona kuhusu shoga wa mke wa Boka aliyelazwa hospitali kisha akamkabidhi Jona faili lake.

"Mpaka hapo tutakuwa tumemalizana," alihitimisha Geof.

"Nashukuru sana," akasema Jona. "Ila nina ombi dogo kwako."

"Karibu."

"Nisaidie kunisogeza kwa Boka mara moja."

Geof akamtimizia haja yake. Jona akashuka mbele ya nyumba ya Boka na kuzama ndani.

Kulikuwa kuna watu kadhaa. Turubai limefungwa likitoa kivuli kwa viti kadhaa vya plastiki vilivyozagaa.

Akafanya mpango wa Kuonana wa Boka. Haikupita muda mrefu akawa ameketi kando na mwanaume huyo. Akajitambulisha yeye ni nani, ametoka wapi na hapo anafanya nini.

"Ooh! Nilikuwa natarajia ujio wako," akasema Boka. "Kamanda alinambia atanibadilishia mpelelezi. Bila shaka wewe anakuamini."

Jona akajibu kwa tabasamu kisha akaanza kutekeleza kazi yake. Akamuuliza Boka maswali kadhaa, na kati ya hayo taarifa iliyokamata sikio lake ilikuwa ni hii.

"Siku hizi mbili au tatu za mwishoni, hakuwa sawa. Hakutaka kuongea na mimi na wala hakunieleza nini tatizo hata nilipojaribu kumuomba."

Jona akahisi hapa patakuwa chemchem yake ya mfanikio.

"Haukuwa umemkwaza au kugombana kwasababu yoyote ile?"

"Hapana. Hatukuwa na ugomvi japo niliona amebadilika ghafla. Lakini sijui, labda nilikuwa nimemuuzi, ila hakunambia."

Jona alipotoka hapo akazuru pia kazini kwa mwanamke huyo, huko akakutana na mkurugenzi msaidizi, bwana Liundi akiwa hae hae anataka kutoka aende msibani.

Akamwomba muda kidogo watete.

"Imekuwa ni ghafla mno, amefariki akiwa kwenye projekti kubwa ambayo ingejenga jina la Tanzania na hadhi yake kwa ujumla," alielezea bwana Liundi.

Jona akataka kujua zaidi kuhusu projekti hiyo. Liundi akaeleza kinaga ubaga, akitoa mpaka na mpango kazi na hata hatua waliyokuwa wamefikia kwenye kusambaza vipodozi vyao vya kiasili nchini Kenya.

Wakiwa humo wanaelezeana, Jona akastaajabu kuona picha ya Miranda! Aliitazama picha hiyo kwa umakini kisha akauliza:

"Huyu ni nani?"

"Aaahm ... alikuwa kama patna wa mama kwenye hii projekti."

"Tangu lini alianza kufanya kazi na mama na unafahamu walijuanaje?"

Liundi akajibu swali la kwanza ila la pili akashindwa. Hakujua Miranda alikutana wapi na aliyekuwa bosi wake.

"Nitakichukua hiki kipeperushi," akasema Jona.

"Hamna shida, viko vingi waweza chukua," Liundi akamtoa shaka. Jona akaaga.

Sasa kichwani akawa anamuwaza Miranda tu. Imani yake yote ilimwangukia mwanamke huyo maana anamjua vema. Alijikuta anakubaliana na nafsi yake kabisa kuwa mwanamke huyo atakuwa mtuhumiwa wake wa kwanza!

Anahitaji kumtafuta haraka iwezekanavyo.

Akampigia simu, ikaita mara mbili kabla haijapokelewa.

"Unaongea na --"

"Jona!" Sauti ya Miranda ikamkatiza.

"Ndio, Jona hapa, nina shida na wewe haraka iwezekanavyo."

"Nini shida Jona? Mbona upesi hivyo? Ni mambo ya ile picha?"

"Hapana! Ni kuhusu ajali ya mke wa mheshimiwa!"

"Ooh! My God. Jona, I didn't do it. Honestly!" (Ooh! Mungu wangu. Jona, sijalifanya hilo. Ukweli kabisa!)


****

- MIRANDA ANASEMA UKWELI? KAMA SI YEYE NANI BASI?

- VIPI MARWA ATAFANIKIWA KUONANA NA PANKY WAKAMILISHE MPANGO?
 
AHAAAA!!!! HAYO NDO MAMBO YA STEVE SASA YAANI HAPA NILIPO MPAKA NATAMANI KUINUKA KWENYE KITI NISHANGILIE (WE STEVE UNALETA MAMBO GA KUJUANA WEWE) NAFASI YA MBELE JONA KAZI KAMA KAWAIDA YETU
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…