*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 15*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Kufanya nini huko saa hii?" Kinoo akauliza.
"Nataka nikalale huko leo. Sina hamu kabisa ya kuwa na wewe."
"Eh!" Kinoo akaguna.
ENDELEA
Hakutaka kusema jambo akaamua kutimiza agizo la mpenzi wake huyo kuepusha maneno. Lakini bado alikuwa amekosea. Sarah akawaza pengine Kinoo alikuwa amemchoka.
Yani amemwambia akalale kwa dada yake alafu anakubali pasipo hata kubisha? Akavuta mdomo mpaka wanawasili. Walipofika ndipo akatoa ya moyoni.
"Naona umefurahi mimi kuja huku!"
Kinoo akatikisa kichwa asiseme jambo. Aliona angeongea angesababisha vingine ambavyo hakuvitarajia. Akaongoza njia mpaka getini, akagonga na wakakaa kungoja.
Ndani ya muda mfupi geti likafunguliwa na akatoka mwanamke mmoja mtu mzima. Wakamsalimu na kumwambia haja yao, kumwona Sasha.
"Mbona amehama hapa siku nyingi!" Mwanamke huyo akawaeleza. Sarah akastaajabu. Inawezekanaje dada yake akahama hapo makazi yao ya muda mrefu pasipo kumwambia??
Lakini pia atakuwa ameenda wapi na ilhali pesa hakuwa nayo? Hakupata majibu.
"Amehamia wapi?" Sarah akauliza. Yule mwanamke akamwambia hafahamu. Kitu pekee anachojua ni kwamba mwanamke huyo amehama.
"Ahsante sana," Kinoo akashukuru na kumtaka Sarah warejee kwenye usafiri waondoke zao.
Lakini wakiwa wapo njiani, Sarah hakuwa na amani. Alikuwa anamuwaza pacha wake. Alihisi atakuwa shidani. Alikosa kabisa furaha.
"Usijali, ni mtu mzima yule. Hawezi akawa amepotea," Kinoo akamtoa hofu.
Angalau hili swala likawaleta pamoja baada ya kuhitilafiana hapa nyuma.
"Mara yake ya mwisho kuonana naye alinambia hayuko vizuri kifedha. Hata nikamtoa nauli. Leo naambiwa amehama. Inashangaza!" Sarah aliongea kwa hisia.
"Au kafukuzwa kodi?" Kinoo akauliza. Lakini kabla Sarah hajajibu, Kinoo akapuuza wazo lake hilo. "Ila haiwezekani! Si angekuja pale nyumbani??"
Sarah akabaki kimya. Punde akatafuta simu yake na kumpigia dada yake. Sijui alikuwa anawaza nini akachelewa kufanya hilo. Aliweka simu sikioni kusikilizia, baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, sauti ikamwambia anayempigia hapatikani!
Akajaribu kama mara nne, yote majibu yakiwa hayohayo, HAPATIKANI!! Sarah akazidi kujawa na hofu.
Mpaka wanafika nyumbani alikuwa kimya. Ila kheri alipokuwa anaingia ndani, simu yake ikaita. Kutazama alikuwa ni Sasha! Mwanamke huyo alimtafuta baada ya kukuta taarifa ya kutafutwa punde baada ya kuwasha simu yake.
"Hallow!"
"Hey nambie sis!"
"Mambo?"
"Poa. Unaendeleaje dear?"
"Safi tu. Upo wapi?"
"Mie? Ntakuwa wapi pengine zaidi ya nyumbani saa hii?
"Nyumbani?"
"Ndio. Nipo kwa bi Mwenda hapa."
Bi Mwenda alikuwa ni yule mwanamke aliyewafungulia geti Sarah na Kinoo walipoenda kumtembelea Sasha kule makazini.
"Sasha," Sarah akaita. "Kwanini unaniongopea?"
"Nakuongopea? Kivipi dear?"
"Umehamia wapi?"
Kidogo kukawa kimya.
"Najua umehama. Nambie umehamia wapi?"
"Sarah, yah nimehama. It's a long story. Ntakutafuta tuongee."
Simu ikakata. Sarah akaachwa na bumbuwazi. Akajaribu tena kupiga akaambiwa haipatikani!!
Sasha ana nini?? Akajiuliza akiduwaa.
**
Usiku mzima alikuwa analia kwa maumivu makali! Mifupa ilikuwa inamuuma mwili mzima. Kichwa bado kinagonga na pua inamimina damu!!
Kila alipotaka kusogeza kiungo chake cha mwili, akaishia kulalama na kushindwa. Haki mateso yalikuwa makali mno. Hakuwahi kujihisi mdhaifu kiasi hiki tangu azaliwe.
Hakuwahi kuhisi maumivu makali kiasi hiki tangu atambulishwe duniani. Haya yalikuwa kiboko!! Ni kama vile alikuwa amevunjwavunjwa mwili mzima kisha akadumbukizwa kwenye bwawa la barafu akae humo kwa masaa!
Hakuwa anahisi chochote kwa ngozi yake. Kichwa kilikuwa hakigongi tena bali kinampigia kelele kali! Ushawahi kusikia paka akikwarua bati? Ndivyo Jona alivyokuwa anasikia makelele sikioni!!
Meno yalikuwa yanamuuma. Jasho lilimwagika.
Wenzake hawakuwa na la kumsaidia zaidi ya kumtazama tu kwa huruma. Japo hawakuwa wanajua nini Jona anahisi mwilini, walimwona anateseka sana.
"Jooonnnaaaa!" Sauti kwa mbali ilimfikia masikioni. Kama kawaida sauti hii alikuwa anaisikia kwa mbali sana. Kwa taratibu sana.
Alitamani ajue sauti hii ni ya nani ila hakuweza. Maumivu alikuwa anayasikia. Kelele sikioni iliyokuwa inamuumiza, ilimnyima nafasi hiyo.
Langoni alikuwa amesimama Kamanda mkuu. Alikuwa yu ndani ya sare yake ya jeshi iliyokuwa imechafuka kwa urembo na vyeo. Macho yake yalikuwa yanamtazama Jona aliyekuwa amelala chini.
Kidogo akaungana na vijana wawili waliokuwa wamevalia kiraia. Walikuwa ni maaskari pia. Miongoni mwa vijana hao alikuwa ni yule 'jamaa' aliyemfuatiliw Marwa kuyafahamu makazi yake.
Wote wakamtazama Jona kwa muda mchache kabla Kamanda mkuu hajaagiza wamlete ofisini kwake ana maongezi naye.
**
"Jona!" Kamanda akaita akimtazama Jona kitini. Jona alikuwa amekaa hapo akiendelea kuchuruza damu puani. Alikuwa ameketi kana kwamba mgonjwa wa utindio wa ubongo. Alikuwa ameng'ata meno, amekunja ndita, mabega ameyapandisha juu. Macho amefumba kusikilizia maumivu pomoni anayosikia.
Kwa mbali sauti ya Kamanda ikamfikia:
"Jona, utaendelea na mateso haya mpaka lini? Kubali yaishe. Si kila mara utaibuka kuwa mshindi! ... naweza nikakusaidia. Nipatie nafasi."
Jona hakuwa na uwezo wa kujibu. Aliendelea kukaa vilevile kana kwamba hajasikia kitu.
"Ukifanya mchezo utafia rumande kwa ubishi wako!" Kamanda akatishia. "Sasa chagua moja nikakutupie huko uendelee na maumivu yako ama nikusaidie upate unafuu??"
Japo Jona hakuwa na uwezo wa kupambana, na alikuwa anasikia maumivu yasiyo na mithili, akafungua macho na kumtazama Kamanda. Macho yake yalikuwa mekundu mno!
Alimtazama Kamanda kwa macho ya umauti. Macho ya kisasi!!
Akiwa anahisi maumivu ya kufa, akanyoosha mkono wake akitaka kumkamata Kamanda. Ila haukufika, akashindwa kustahimili maumivu.
"Unajifanya mgumu eenh?" Kamanda akamuuliza akibinua mdomo wake. Akagonga meza mara mbili.
Puh! Puh!
**
Mlango wa ofisi ukafunguliwa, wakatoka vijana wawili wa Kamanda wakiwa wamembelelea Jona. Kwa upesi wakayoyoma naye wakielekea rumande kwenda kumtupia huko.
Mlango wa ofisi ulipofunga, Kamanda akanyaka simu yake na kupiga.
"Bado ni mgumu. Nadhani tuangalie namna ya pili sasa," Kamanda alisema kwa hakika.
"Hapana," sauti ikavuma simuni. "Ngoja tutazame na kesho kama bado ataendelea kuvumilia. Virus hao wanatafuna kila siku inavyokwenda. Hataweza kuvumilia zaidi ya kesho. Na itapendeza zaidi kama yule rafiki yake atamletea antidote!"
"Kivipi?" Kamanda akauliza.
"Hao virus ambao wapo mwilini mwake hawaondolewi na antidote waliyonayo. Endapo atakampopatia, basi ataharibu mambo zaidi. Atapata maumivu maradufu!!"
Kamanda akaridhika na hayo maelezo. Akakata simu.
**
"Nipo tayari kwa kila kitu," alisema Marwa akimtazama Miranda. Walikuwa wapo ndani ya nyumba ya Jona majira haya ya mchana. Miranda alifika hapo muda si mrefu hapo nyuma akiwa katika harakati zake za kuwezesha zoezi la kumtoa Jona kituoni.
"Sawasawa!" Miranda akatikisa kichwa. "Hili zoezi inabidi lifanyike kesho kwa namna yoyote. Wewe kazi yako ni ndogo sana. Kule kituoni wameshakuzoea sasa kuwa unaleta chakula mara kwa mara.
Sasa kesho yake nitakupatia hotpot la chakula ulipeleke huko. Utakapofika, utafanya njia zozote ulifungue pale kaunta, kwa muda wa sekunde kumi tu. Kisha ukifanikiwa kulipeleka kwa Jona, umtahadharishe asile.
Ataliweka wazi kwa dakika moja, inatosha. Mengine mimi na Kinoo tutamalizana nayo."
"Sawa, hamna shida," Marwa akapokea maelekezo. Kisha pasipo kupoteza muda akamwambia Miranda kuwa anataka kwenda kituoni kumpelekea chakula Jona.
Na pia vilevile antidote!!
"Hamna shida, naweza kukuwahisha," Miranda akamkarimu. Wakanyanyuka toka sebuleni na kwenda nje walipodumbukia ndani ya Range Rover sport nyeupe na kutimka.
**
- JE MPANGO WA PILI WA KAMANDA KAMA JONA ATAENDELEA KUWA MKAIDI NI UPI?
- MIRANDA ATAFANIKIWA ADHMA YAKE KUMTOROSHA JONA KITUONI?
- UHAI WA MARWA UPO KWENYE KITUFE CHA BUNDUKI, KITABONYEZWA?
- SASHA ATAMWAMBIA SARAH JUU YA MPANGO WAKE? VIPI UTAWABAKIZA WAKINA MIRANDA SALAMA?