*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 16*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Na pia vilevile antidote!!
"Hamna shida, naweza kukuwahisha," Miranda akamkarimu. Wakanyanyuka toka sebuleni na kwenda nje walipodumbukia ndani ya Range Rover sport nyeupe na kutimka.
ENDELEA
Kwa kasi waliyoitumia hawakuchukua muda kuwasili, Marwa akashuka garini na kwendaze kituoni baada ya kuagana na Miranda aliyesema anaenda kushughulikia na kuweka mambo sawa.
Marwa akaingia mapokezi na kukutana na afande Devi aliyempokea kwa ukarimu na kumjulia hali.
"Nimekuja kumletea chakula jamaa 'angu," alisema Marwa kisha akafungua chakula na kukionyesha.
"Najua umekuja sababu hiyo," alisema afande Devi pasipo kutazama chakula hicho. Ni kheri akuwapo koplo Massawe, basi akamruhusu akamwone mtu wake upesi huko rumande.
Chap Marwa akafika huko na kumkuta Jona akiwa amejilaza hoi. Akamuita mara tatu akisaidiwa na mahabusu wengine. Jona akaamka na akiwa hajiwezi kwa lolote, wenziwe wakamburuta kusogea langoni.
Kwa namna ambavyo Marwa alimwona Jona, akashindwa kuzuia machozi machoni mwake. Jona alikuwa amepungua. Ni mdhaifu. Hana afya wala havutii kumtazama.
Si Jona yule umjuaye.
"Jona," Marwa akaita. "Kula angalau." Akambembelezea chakula. Jona akatamani sana kumjibu lakini hakuwa anaweza.
Alimtazama Marwa akamwona kwa mbali. Alitabasamu kumpa matumaini lakini Marwa akaishia kulia.
"Nitashinda," Jona alisema kwa sauti ya chini. "Usijali, Marwa."
Akala tonge mbili tatu, akashindwa kuendelea. Alilalama anasikia kichefuchefu, na kadiri anavyotafuna anasikia kichwa kinamuuma maradufu!!
Japo ni kweli alitamani kula, tumbo lilikuwa tupu, hakuweza abadani!
"Nimekulete antidote!" Marwa alimwambia kwa macho ya furaha. Alikuwa amemshikilia na mkono wake kumzuia aketi.
Kabla Jona hajasema kitu, Marwa akatazama kushoto na kulia alafu akachonoa kichupa kidogo mfukoni, akamtaka Jona afungue mdomo.
Akamminia chote kisha akamruhusu ajilaze chini.
"Utakuwa sawa," Marwa aliamini.
Jona akalala asiseme kitu. Muda si mrefu akakata fahamu kabisa!! Hakuwa anasikia, kuona wala kuhisi chochote.
Maumivu yalizidi mwilini mpaka fahamu ikashindwa kustahimili. Marwa asiwe anajua hilo, akamtazama Jona kwa sekunde kadhaa. Na hata alipoona kimya akatambua mwanaume huyo atakuwa katika hatua za kuwa sawa. Hivyo hana haja ya kuhofu.
Akamuaga Jona na kisha kwenda zake.
**
"Afandeee!" Sauti ikavuma ndani ya rumande. Si kwamba kulikuwa kimya, bali sauti hii ilikuwa kubwa kupita kiasi.
"Afandee, kuna mtu anakufa huku!" Alipaza sauti jamaa mmoja aliye ndani ya chumba kimoja na Jona.
Jona alikuwa anatoa damu masikioni, puani, mdomoni na machoni kama machozi!! Hakuwa anatikisika hata kidogo. Hakuonyesha dalili zozote za uhai.
Hata mwili wake ulikuwa wa baridi kana kwamba ametoka kwenye jokofu!!
Haraka afande Devi aliwasilia akamtazama Jona. Mahali alipokuwa amelaza kichwa chake palikuwa pametapakaa damu.
Hata afande huyu akashtushwa sana na hili. Upesi akamweleza na kumsisitiza Massawe akamwambia mkuu wa kituo kuwa wanatakiwa kuchukua hatua upesi la sivyo mtu atawafia rumande iwe tabu!
Taarifa zikafika kwa OCD, ila ikawa bure. Jona hakuruhusiwa kutoka kituoni kwa namna yoyote ile labda awe mfu tu!!
"Nenda kaendelee na kazi yako. Kama kufa mwache afie humo. Alivyomuua RPC alidhani atastarehe??" Alisema OCD akiwa anachokonoa meno yake kwa toothpick.
**
"Ewaah ... naona ameshapatiwa ile antidote!" Alisema Kamanda mkuu akitabasamu na simu.
"Yes ... he is in critical situation ... hawezi akafa? ... ooh sawa. Hamna shida nitafanya hivyo."
Kamanda akakata simu kisha akacheka. Alipewa maagizo ya kuyatimiza.
**
"Naomba uningoje hapa," alisema Sarah kwa sauti ya kuamuru. Macho yake yalimtazama Kinoo kabla hajabanduka toka kwenye kiti cha gari na kwendaze ndani ya jengo maeneo ya Msasani.
Kinoo akamtazama mwanamke huyo akizamia humo aliposema anaenda kukutana na dada yake, Sasha, kama walivyopeana maelekezo.
Akawaza kidogo akijiuliza maswali kadhaa. Sasha alikuwa anafanya nini katika hilo jengo maeneo ya Msasani na kwanini Sarah hakutaka kuongozana naye kwenda humo.
Kwani Sasha si shemeji yake??
Hakuwaza wala kujihangaisha sana kwani alidhani pengine Sarah anataka tu kulipiza kisasi kwa vile anavyomfanyia akiwa anaongea na Miranda akimtaka atoke nje.
Akajikuta anatabasamu na kupuuza. Kosa ambalo hakutakiwa kulifanya hata kidogo.
Kwenye ulimwengu wa kijasusi, hakuna kitu kidogo hata siku moja. Kila tendo laweza kugeuka na kuwa sumu kali ys kumshusha tembo ndani ya sekunde kadhaa tu!!
Kusogezea muda wake wa kungoja, akawasha redio na kulaza kiti, akajilaza.
**
"Kwanini haukunambia siku zote hizo Sasha?" Sarah aliuliza akimtazama dada yake kwa macho ya ndita.
"Niliogopa," Sasha akajibu. "Ningeanzia wapi na wewe tayari umebeba mimba yao??"
Sarah akabaki njia panda. Hakuwa na neno la kusema. Sasha akamshika bega na kumuuliza:
"Utanisaidia?"
"Hapana!!" Sarah akajibu akisimama. "Nitawezaje kufanikisha hilo?? Mwanangu atatolea wapi baba mwingine kama ikatokea Kinoo akafa??"
"Ssshhhhh!" Sasha akaweka kidole mdomoni. "Punguza sauti yako, tutasikika!"
Akatazama dirishani kisha akarudisha macho yake kwa Sarah.
"Sijasema tumuue yeyote yule, Sarah!"
"Sasa unadhani hizo taarifa utakazokuwa unapeleka huko zitaishia kwenye nini?" Sarah akamkatiza.
Hakutaka kumwelewa dada yake hata kidogo. Alitoka zake ndani ya nyumba pasipo kuaga akamwacha Sasha akiwa ameduwaa.
Akang'ata meno na kukunja ngumi kwanguvu. Mpango wake ulikuwa umefeli!!
Sasa atafanyaje?? Kichwa chake kilikuwa moto. Hakuna mtu yeyote anayetakiwa kujua siri hiyo ila tayari ashamweleza dada yake.
Hapa akapata shaka kubwa. Hakuamini kama Sarah atautunza mdomo wake asiseme kitu. Kama tu akiufungua mdomo wake basi kazi itakuwa imekwisha!!
"Damu nzito kuliko maji," alijipa moyo. Ila kama mambo yasipoenda kama inavyotakiwa, basi hamna budi.
Hamna budi.
Itabidi amtoe sadaka dada yake!!
Aliwaza.
**
Usiku mzito, ndani ya chumba chenye giza ...
Waaaaa!! Jona alimwagiwa maji ya baridi na kuamriwa aamke upesi. Hakujua hapo alipo amefikaje. Alijaribu kufungua macho yake kutazama lakini hakuwa anaona kitu.
Si tu kwamba kulikuwa ni giza, hakuwa na uwezo wa kuona kabisa mbali na kutokuwa miwani. Hata masikio yake yalikuwa yamepoteza uwezo wake wa kawaida. Pia ngozi yake yake, ilikuwa hafifu kwenye kuhisi.
Lakini ajabu alipomwagiwa maji hayo ya baridi, alilia kwa maumivu makali ambayo hajawahi kuyapata!!
Ni kama vile maji hayo yalikuwa na visu ama viwembe. Yalimfanya ang'ate meno kwa ukali wa maumivu yaliyopitiliza. Alihisi amechanjwa chanjwa kila sehemu ya mwili wake iliyoonja maji hayo ya baridi.
Alihisi maji hayo yameingia mifupani. Yanamtafuna!!
Japo alikuwa dhaifu, akatapatapa kujinasua. Akahangaika huku na kule lakini hakuweza kufua dafu kwenye kamba ngumu alizokabwa nazo kitini.
Lakini kama haitoshi, ndani ya chumba hicho kulikuwa na ndoo tatu za maji baridi kabisa. Zote zilikuwa zinamgojea yeye.
Zinamngoja akileta ukaidi.
"Mzee, hatuna muda wa kupoteza hapa na wewe. Tunataka kitu kimoja tu. Kiri na sisi tutaenda zetu. Ukileta ujuaji, tutasema na wewe usiku huu mzima."
Jona alisikia sauti hiyo kwa mbali mno. Hakumjua anayemwongelesha ni nani. Alikuwa amekunja shingo yake kana kwamba kaelemewa na kichwa.
"Sisemi kitu," akasema kwa kunong'oneza. Mtesi wake akatabasamu kuonekana meno kizani.
Baada ya hapo Jona akamwagiwa ndoo mbili za maji baridi. Maji haya si kwamba yalimfanya asikie baridi, ila mchanganyiko wake na virusi vilivyomo mwilini mwa Jona, ulizalisha maumivu makali yasiyomithilika!!
Haikupita muda mrefu, Jona akazima.
Simu ikapigwa.
"Hatujafanikiwa, mkuu."
"Sawasawa," sauti ikatoka simuni. Sauti nzito ya Kamanda mkuu ikiashiria kutoka usingizini. Mwanaume huyo alisafisha koo lake kisha akasema:
"Sasa tuhamie kwenye njia ya mwisho. Kesho hakikisha mnamteka yule kijana anayemletea chakula kisha mumpatie machaguzi mawili, aidha tumuue huyo kijana ama afanye tunachokitaka."
**