Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 18*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Sheng, kwa hasira, akavuta droo na kutoa bunduki yake ndogo. Pasipo kujiuliza mara mbili, akamtwanga risasi tatu mwanadada huyo, akafa papo hapo!!

Mwanadada ambaye hakuwa na hatia bali akitimiza tu kazi yake.

ENDELEA

Punde wakaingia wanaume wawili na pasipo kuuliza wakanyanyua maiti na kuipeleka inapotakiwa kuwapo.

Sheng akabaki akizunguka kitini kwake akiwa na mawazo makali sana. Hakujua namna ya kufanya. Alihisi kichwa chake kimeganda. Amechanganyikiwa. Hakupata cha kufanya japo aliwaza sana.

Mwishowe akaamua kunyanyua simu na kupiga. Simu ikaita mara mbili kabla ya kupokelewa. Akasemakwa ufupi, nakuhitaji ofisini na punde muda usiende sana hapo ofisini akaingia mwanaume mmoja mwenye asili ya China.

Alisalimu na kuketi. Mwanaume huyu alikuwa ndiye yule waliyejadiliana na Sheng kipindi kile mpaka kufikia kumpelekea pesa Kamanda mkuu hotelini.

Alikuwa amevalia suti yake nyeusi. Imemkaa vema japo hakupendeza. Alikaa kitini kwa muda kidogo kabla Sheng hajamwongelesha.

Kwa muda wote huo Sheng bado alikuwa anawaza tu lakini kitu kisichoeleweka. Unajua namna mtoto mchanga aandikavyo karatasini?? Ndivyo Sheng alivyokuwa anahisi kichwani.

Yaani vuruguvurugu tupu!

Baada ya muda kidogo, akanyanyuka na kuendea jokofu. Akatoa maji madogo na kuyanyonya kama ndama afanyavyo ziwa la mamaye. Si kwamba alikuwa anahisi kiu kali, hapana. Alitaka angalau kifua chake kipoe.

Kwani la sivyo angeweza hata kuchojoa bunduki kwenye droo na kumtwanga mtu aliyemuita mwenyewe hapo.

Alipokunywa na kumaliza maji hayo, angalau kwa mbali akapata ahueni. Akamweleza yule jamaa, jinale Shao, juu ya kikichotokea. Na hakika hata Shao akapigwa na bumbuwazi zito!

Ila akatafuta namna ya kukabiiana nalo apate kumshauri mkuu wake ambaye alikuwa amekwama. Kwanza akamtoa hofu juu ya Jona.

"Wǒmen huì dédào tā!" (Tutampata!) Akasema kwa kujiamini.

"Rúguǒ wǒmen bù yuànyì dehuà, tā huì sǐ de!" (Na kama tusipofanikiwa basi atajifia)

Kwa minajili kwamba virusi waliomuingizia mwili hawatadumu naye kwa muda mrefu. Kadiri anavyokaa navyo ndivyo watakavyomdhoofisha na mwishowe kufa!!

"Tāmen yǒngyuǎn bù zhīdào cóng nǎlǐ dédào jiě yào!" (Kamwe hawatajua wapi pa kupata antidote!) Akasema Shao kwa msisitizo. Maneno hayo yakaingia ndani ya kichwa cha Sheng lakini bado hayakumkosha. Akauliza kama antidote ipo ndani ya kambi yao.

Shao akamjibu ni kiasi kidogo sana kilichopo. Hakiwezi kudumu hata zaidi ya juma moja.

"Méiyǒu! Wǒ yào lìjí mái xià suǒyǒu de jiědú jì!" (Hapana! Nataka antidote zote zifukiwe mara moja!) Sheng akabweka akigongesha kidole chake mezani. Alihofia pengine antidote hizo zinaweza kupatikana na kumsaidia Jona.

Shao akalipokea hilo agizo na kuapa kulitekeleza. Kisha akamsihi mkuu wake kutumia fedha yake sasa kama chambo cha kumpatia Jona. Aweke matangazo kote mitandaoni akitangaza kutafutwa kwa mwanaume huyo na mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha upatikanaji wake basi apatiwe donge nono la pesa.

Sheng akaridhia hilo wazo kwa moyo mkunjufu. Lakini pia akaagiza vijana wake wote wa vitengo vya usalama wakutane naye usiku wa saa nne. Ana mambo kadhaa anataka kujadili nao.

**

"Hatujafanikiwa mpaka sasa, mkuu!" Sauti ilivuma kwenye simu ya Kamanda. Alikuwa amesimama koridoni akiwa amevalia taulo. Ameshikilia kiuno chake kipana.

Si sebuleni wala chumbani kulipokuwa kunakalika. Tumbo lilikuwa joto. Kama kuna kipindi kigumu alichowahi kupitia akiwa kazini, basi ni hiki.

Mwili ulikuwa unamtetemeka na kila simu iliyokuwa inapigwa alikuwa akiidaka upesi na kuiweka sikioni. Zaidi ya hapo alikuwa mbogo haswa. Hata mkewe na watoto walienda kujifungia ndani baada ya kuona hapakuwa panakalika.

"Hamjafanikiwa mnafanya nini sasa huko??" Akafoka. "Ni kazi gani mwafanya huko ina maana mmeshindwa kui-trace hiyo ambulance mkajua imeelekea wapi??"

"Tumefanya hivyo mkuu," sauti ikajitetea simuni. "Tumefuatilia na hata kwenda mpaka hospitali ambayo jina lake lilikuwa ubavuni mwa ambulance hiyo ..."

"Wakasemaje??" Kamanda akakatiza.

"Hawaitambui hiyo ambulance! Haipo kwenye orodha ya usafiri wao. It means ilifojiwa tu!"

"Na namba?? ... hizo plate nu-number je??" Kamanda akauliza upesi.

"Namba tumezifuatilia, ni za biashara. Gari lilisajiliwa kama daladala ila kuhusu mwenye mali nayo alikwisha fariki muda sana. Hata hili gari halikuwa likifanya kazi hiyo ya daladala kwa muda mrefu hapa jijini kutokana na marufuku ya vyombo vya aina hiyo kufanya kazi hiyo jijini."

Kamanda akashusha pumzi ndefu kisha akauliza:

"Sasa mmefanyaje?"

"Bado tunaendelea na upelelezi mkuu, tutakapopata chochote kitu basi tutakutaarifu."

Kamanda akakata simu na kurejea sebuleni. Akakaa hapo akiwaza na kuwazua nini afanye. Akiwa hapo, mara simu yake ikaita. Akatazama alikuwa ni Sheng. Akapokea simu na kuiweka sikioni.

Sheng akampa taarifa ya kumhitaji ofisini kwake majira ya saa nne usiku.

**

"This is disgrace to Wu family!" (Hii ni fedheha kwa familia ya Wu!) Sheng aliwaka. Macho yake yalikuwa mekundu. Hakuketi kitini, alihisi hataeleweka. Aliongea kwa hasira na jazba.

"Siwezi kukubali kudhalilishwa kiasi hiki na kikundi kidogo cha watu. Kamwe!"

Akatazama kushoto na kulia akipekua rundo la wafanyakazi wake wanaomtazama kwa umakini. Ukumbi ulikuwa kimya. Hata mbu angelikatiza hapo angelisikika.

Vijana watabe, vijana wa kazi, wachina kwa weusi, walikuwa wametega sikio kumsikiliza mkuu wao. Na wakiwa tayari kubeba agizo lolote lile watakalokabidhiwa.

"Sasa ni hivi," Sheng akaelekeza kwa mkono. "Kwa sasa kazi zote zitasitishwa. Hakuna kufanya kazi nyingine yoyote isipokuwa moja tu! Kumtafuta Jona popote alipo. Yeyote atakayeleta kichwa chake ofisini kwangu, nitampatia cash shilingi milioni mia nane!

Zoezi hili lisizidi mwezi mmoja tangu sasa."

Baada ya hayo akawataka waende. Akabaki na Shao aliyejadiliana naye kwa sekunde kadhaa kabla hajamuuliza kumhusu Lee.

"Tā zài nǎlǐ?" (Yuko wapi?)

Shao akapandisha mabega akisema hana taarifa naye.

Kabla hawjajadiliana zaidi, kijakazi akaja na kumpasha habari Sheng kuwa ana mgeni. Kamanda mkuu ameshafika ofisini kwake.

**

"Nimekuita hapa kwa jambo moja," Sheng alifungua kijikao chake cha dharura. Mbele yake alikuwa ameketi Kamanda mkuu akiwa ndani ya shati la kitenge na suruali nyeusi ya kitambaa.

"Nahitaji silaha zaidi kwa ajili ya kazi zangu. Nataka unisaidie kwenye hilo."

"Silaha?" Kamanda akadakia. "Nitakusaidiaje bwana Sheng. Ni ngumu kutoa silaha stock na kukupatia. Itaweza leta suspicions!"

"No! No! No!" Sheng akatikisa kichwa. "Sihitaji silaha zako. Kuna mzigo mkubwa utafika bandarini ukiwa kwenye meli ya wauguzi wanaokuja kutoa huduma ya matibabu bure hapa nchini. Ndani ya meli hiyo kubwa kuna kontena zangu mbili za silaha. Ninachojitaji wewe ufanye ni kuzipitisha kwa kutumia jina la jeshi. Basi!"

Kamanda akameza mate.

"I need them kwa ajili ya kumsaka Jona!" Sheng akamalizia habari.

**

Sasa shauri lilikuwa limekatwa na kesi imefikishwa mahakamani. Boka na Miranda wakataarifiwa kuhitajika kituo cha polisi mara moja.

Ikiwa ni majira ya jioni, Miranda na Boka wakawasili hapo kila mtu akija na usafiri wake lakini ikionyesha bayana kuwa walikuwa na mawasiliano.

Boka alikuwa ameongozana na mwanasheria wake, Bwana Manyanja Mayanja, ambaye yeye ndiye alikuwa akihusika na kila kitu hapo huku mteja wake akiwa msikilizaji tu.

Kwa msaada wa mwanasheria bwana Mayanja Mayanja, wakapewa dhamana na zaidi tarehe za kuhudhuria mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.

"Tutakaposhinda kesi hii, jamhuri italazimika kulipa fidia ya muda na usumbufu na pia kusafisha taswira ya mteja wangu kwa kupitia vyombo vyao vyote vya habari!" Bwana Mayanja Mayanja alinguruma.

Baada ya hapo wakatoka kituoni, ila kabla hawajakwea kwenye vyombo vyao vya usafiri, mara Miranda akaitwa.

Alipogeuka akakutana uso kwa uso na Koplo Massawe.


**

Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
 
*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 19*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Baada ya hapo wakatoka kituoni, ila kabla hawajakwea kwenye vyombo vyao vya usafiri, mara Miranda akaitwa.

Alipogeuka akakutana uso kwa uso na Koplo Massawe.

ENDELEA

Moyo wake ukashtuka. Macho ya koplo Massawe yalikuwa yanamtazama kwa yamkini.

Akageuza shingo yake kumtazama Boka kisha akamsihi amngojee yeye akienda kukutana na koplo Massawe.

"Habari yako?"

"Safi, afande."

Massawe akamtazama Miranda machoni. Miranda naye akajitahidi kuyakaza macho yake. Ila moyo ulikuwa unampwita haswa. Kama koplo Massawe angeligundua hilo, basi angeliweza kumshukumu kindakindaki.

"Kama nishawahi kukuona hapa, bibie," alisema Massawe kwa uso wa mashaka. "Ndiye wewe?"

"Mimi?" Miranda akajiwekea kiganja kifuani. Akabinua mdomo wake na kusema: "labda, inawezekana ikawa ni mimi ... kuna kesi yangu nafuatilia hapa kwa inspekta."

"Oooh!" Massawe akatikisa kichwa. "Basi sawa. Unaweza tu ukaenda."

Miranda asiamini macho yake, akageuka na kuenda zake. Massawe akamtazama akiyoyoma kichwani akijaribu kukumbuka alipomuonea mwanamke huyo.

Alikuwa tayari ameshamtilia mashaka akidhani anaweza kuwa na mahusiano na Jona. Na kama angelithibitisha hilo basi Miranda angekuwa na mashtaka ya kujibu. Asingelitoka hapo kituoni kwendaze.

Ni kama bahati Miranda kuwa na kesi mbadala hapo kituoni. Alichoropokea tundu la sindano.

**

Mikono yake ikiwa ndani ya mifuko ya koti la ngozi, Lee alitazama huku na huko kukagua majengo marefu ndani ya Hongkong.

Macho yake yalikuwa yamezibwa na miwani ya jua. Mdomoni alikuwa ana pipi ndogo ya kijiti akiimung'unya taratibu.

Kuna kitu alikuwa anatafuta. Mkononi mwake alikuwa ana karatasi ndogo nyeupe yenye 'address' ya kufika mahali anapopataka. Na huko si kwengine bali kumfuatilia Chen Zi!!

Wamkumbuka mwanaume huyo?? Mwanaume wa mwisho kuwasiliana na kutumiwa nyaraka kwa njia ya mtandao na yule mchina aliyekwiba nyaraka ya siri ya Lee??

Sasa Lee alikuwa ndani ya Hongkong kumtafuta na hata kumuangamiza kwa mkono wake mwenyewe!! Alifanya yote haya kwa siri kubwa asiwataarifu hata wenzake. Aliona huo ndiyo muda wa kufanya hivyo, la sivyo hatalifanya hilo milele!

Tangu Jona alipotiwa gerezani, alidhani angeweza kufanya misheni yake hii pasipo kusumbuliwa na Sheng. Hivyo mpaka sasa hakuwa anajua chochote kile kuhusu yaliyotokea kwa Jona.

Hakuwa anajua kuwa mambo hayapo tena 'under control' bali 'over control'. Anahitajika na kutafutwa na mkuu wake huko nchini!

Alikuwa anatimiza siku ya tatu akiwa Hongkong. Katika upelelezi wake wa akitumia mtandao wa Facebook alikuwa amepata pa kuanzia kumtafuta na kumpata Chen Zi amtakaye.

Chen Zi ambaye anadhani anaweza akawa ni shabiki wa mwanamuziki Chen Zi halisi ambaye alikuwa mwanamuziki maarufu chini China aliyeripotiwa kufa kwa kuzidisha dozi ya madawa ya kulevya.

**

Ngo! Ngo! Ngo! Lee alibisha hodi kisha akatoa pipi yake mdomoni. Punde akafunguliwa mlango na kikongwe wa kichina aliyemkarimu kwa upole.

Akazama ndani na kuketi. Akafanya 'survey' kukagua sebule ya bibi huyo. Ilikuwa hafifu na yenye vitu vya kale na haikuchukua muda akagundua kuwa bibi huyo anakaa hapo na binti mdogo anayetunza.

"Wǒ zhǎo chén Zi!" (Namtafuta Chen Zi!) Lee akasema hitaji lake. Yule kikongwe akafikiri kidogo kisha akatikisa kichwa chake.

Chen Zi yupi unayemuongelea? Akauliza. Lee akafungua simu yake na kumwonyesha kikongwe yule picha aliyoipakua toka kwenye mtandao wa Facebook.

Kikongwe akavalia miwani na kuitazama picha hiyo kwa ukaribu. Akamuita na yule dada anayekaa naye, akamkabidhi picha hiyo aitazame. Dada akaiangazia na punde akatikisa kichwa.

"Wǒmen bù rènshì tā!" (Hatumjui!)

Lee akaitazama tena ile picha kisha akairejesha simu yake mfukoni.

"Nǐ shì shéi?" (Wewe ni nani?) Akauliza yule kikongwe akimtazama Lee kwa umakini.

"Wǒ shì tā de péngyǒu," (Mimi ni rafiki yake,) Lee akajieleza. "Tā gàosù wǒ tā zhù zài zhèlǐ." (Aliniambia anaishi hapa.)

Kikongwe yule akatikisa kichwa. Basi Lee akashukuru na kwenda zake. Kichwani akiwa anawaza pengine mtu huyo aliyechat naye alimlaghai kama ilivyokuwa kwa mtu yule wa mwisho kumfuatilia jana yake.

Hii ndiyo shida ya Facebook. Watu hata mia wanaweza wakawa wanatumia jina moja. Kwa kupitia mtandao huo, Lee aliwang'amua watu wanne wakitumia jina la Chen Zi na wote wapo China!

Tayari mmoja ashamwendea na kukuta sipo anapoishi. Alipofuatilia address' aliyopewa na mtu huyo akajikuta anafika nyumbani kwa mwanamke mmoja mjane!

Na leo amefuatilia address ya mtu mwingine wa pili, ameishia kufika mlangoni mwa kikongwe! Akawaza nini shida. Lakini hakujali sana. Alikuwa ana muda wa kutosha siku hiyo hivyo hivyo atawamalizia na hao wawili aliowabakiza kwenye orodha.

Akiamini kati ya hao basi mmojawao atakuwa ni Chen Zi anayemtafuta yeye. Moyoni akiwa anaomba nyaraka hiyo isiwe imezagaa ama kufika kwenye mikono ya maadui.


**

"Huānyíng!" (Karibu!) Sauti ya kiume ilifika masikioni mwa Lee. Hakupata wasaa wa kuitafakari sauti hiyo, mara mlango ukafunguliwa na mwanaume mwenye umri wa makadirio 40 - 45. Mwanaume huyo alikuwa amekalia 'wheel chair'. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umelemaa na mdomo wake ulikuwa umepindia kushoto pia.

Akamsalimu Lee na kumuuliza ni kwa namna gani atamsaidia. Lee akaeleza haja yake, kumtembelea rafikiye aitwaye Chen Zi.

Mwanaume yule aliyemkarimu akatahamaki. Hakuwa anamjua mtu huyo. Kwa mujibu wa maelezo yake anaishi na mkewe anayefanya kazi kiwandani, hata simu hana, na huwa yupo bize sana kumhudumia akiwa nyumbani.

"Wǒ hěn bàoqiàn rǎoluàn!" (Samahani kwa usumbufu!) Lee akaenda zake. Kichwani akiwaza haya matukio. Ina maana Chen Zi wote aliochat nao wamemlaghai??

Alitoa simu yake akaitazama. Akairudisha tena mfukoni.

**

"Wǒ bù rènshì tā!" (Simjui!) Alisema mwanamke mwembamba mwenye tumbo kubwa la ujauzito. Alikuwa amesimama mlangoni akimtazama Lee machoni.

Nywele zake zilikuwa hovyo. Alionyesha kuchoka. Kama si wa kushusha vitu kesho basi keshokutwa haipiti.

"Wǒ yīgè rén zhù zài zhèlǐ!" (Naishi peke yangu hapa!) Alisema mwanamke huyo mjamzito akizika matumaini yote ya Lee! Sasa rasmi idadi ikawa imetimia ya watu wanne aliochat nao na kati ya wote hao hakuna Chen Zi anayemtafuta.

Ilimshangaza hili. Lakini ilimshangaza zaidi kwa namna alivyokuwa anakutana na watu wasiojiweza kwenye kila pango alilokwenda kumtafuta Chen Zi.

Kwanini watu hao walimdanganya kama vile alivyoaminishwa na wenyeji wake?? Kwanini wafanye hivyo ilhali hakuwa ameeleza taarifa zake binafsi, badala yake akitumia picha ya kike??

Hapa akabishana na akili yake. Ina maana amebumburukiwa?? Hapana! ... kivipi?? Hakuwa ameacha nyayo zozote za kuhisiwa kombo.

Ila ...

Akawaza.

Kuwaomba wanaume hao 'address' zao kutakuwa kuliwapa mashaka?? Yani mwanamke aliyejirahisisha kupita kiasi?? Hapana. Akatikisa kichwa. Sidhani.

Aliagiza juisi hapo mgahawani. Akatoa simu yake na kuitazama. Haikuwa na ujumbe wowote ule. Akaiweka mezani na kunywa juisi yake taratibu akifikiria namna ya kufanya.

Punde hapo mgahawani wakaingia wanaume watatu waliovalia nguo nyeusi juu mpaka chini. Walikuwa ni wanaume wenye miili mikubwa, wawili miongoni mwao walikuwa ni wachina, mmoja alikuwa ni mtu mweusi ti.

Jamaa huyu mweusi hakuwa na nywele hata moja kichwani. Wenzake walikuwa nazo ila chache, kwa mbali.

Wakakaketi eneo moja. Upande wa kushoto wa Lee kwa umbali wa hatua kama nne hivi za mtu mzima. Nao wakaagiza juisi.

Ikapita kama dakika tatu wakiwa hapo. Ila walikuwa wanamtazama Lee si mara moja wala mbili, wala tatu.

Na kuna kitu walikuwa wanateta midomoni mwao kisisikike hata kwa majirani.


**

Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
 
Steve Mungu azidi kuibariki kazi ya mikono yako.
Ahsante miranda wewe ndio tegemeo letu kwa sasa....mponyeshe kwa Jona then mengine yatafuata
Hahaha mdada unamuonea huruma jona eh sheng Huyo anaenda kumpiga risasi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…