Wanaomhujumu mgombea ubunge wa CCM Same waonywa
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya same, Bw. August Kessy amesema kuanzia sasa viongozi wa ngazi zote wanaomhujumu mgombea Ubunge wa Jimbo la same Mashariki kupitia Chama hicho, Bi. Anne Kilango, wataondolewa.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Kambene Kata ya Miamba Bw. Kessy alisema kuna viongozi ambao wamekuwa mwiba mkali kwa kampeni hizo, kutokana na kuchochea uasi.
Bw. Kessy alisema kutokana na hali ya kampeni kudorora katika Kata nyingi, ameamua kupeleka taarifa mkoani, kuelezea tatizo hilo.
Nimeshapeleka taarifa mkoani wameniruhusu kumuondoa kiongozi yoyote, ambaye ataleta vurugu na mgawanyiko wa kichama wakati wa kampeni, hata kama kiogozi huyo anaondolewa na vikao kwa mujibu wa katiba, lakini mimi nitamuondoa kwa muda hadi kampeni zimalizike, ndipo vikao vikae, sasa hivi hatuna muda,alisema Mwenyekiti huyo.
Alisisitiza kwamba viongozi hao, ni wale ambao hawakufarahishwa na mgombea ubunge aliyeteuliwa na CCM.
Alisema viongozi hao pamoja na wananchi, wamekuwa wakisusia mikutano ya kampeni ya mgombea huyo wa CCM.
Jamani kura za maoni sasa hivi ni historia, lakini kwa Jimbo la Same Mashariki, bado kura za maoni ni tatizo. Matokeo yake yamesababisha kudorora kampeni zetu bila sababu za msingi,alisema Bw. Kessy.
Mwenyekiti huyo, alitoa karipio hilo, baada ya kupita kwa maandamano na kukuta bendera za CCM zinapeperushwa nusu mlingoni, kama ishara ya maombolezo.
Alisema kwa vyovyote hatua hiyo, ina mkono wa viongozi, jambo ambalo lilipingwa vikali kwa kiapo na Mweneykiti wa Kata hiyo Bw. Pagu Mkulu.
Tangu kuanza kwa kampeni za mgombea huyo, wananchi wamekuwa wakisusia mikutano yake, kuzomea na kurusha mawe kwa sababu zinazoelezwa kwamba chanzo chake ni kura za maoni, ambapo mgombea anayekubalika na wananchi wengi Bi. Naggy Kaboyoka alitemwa.
Hata hivyo, Bw. Kessy alisema hata kama wananchi hawampendi Bi. Kilango ni vema wakaja kumsikiliza, badala ya kususia mikutano yake.
Pale Mjema na Bombo Kata nzima walikuja watu saba kwenye mkutano, hapa kuna tatizo, pia kuna kukosa uungwana kwa viongozi na wanachama wa CCM,alisema.