Mzee wa Kujitoa
KYOOOKI EKI! Wacha tu nizungumze kikwetu mwanakwetu. Mwashangaa napaniki hadi nazoza hicho mnachoita kilugha?
Nitakaaje kimya huku tukiambiwa eti kuna wala nchi wamejichotea bilioni 133? My God! Leo nitachanganya lugha zote. Iwezekane tulikuwa tunapigania uhuru ili kushibisha matumbo ya wachache? Tulikuwa tunadhani yule mtoto wa Slaa, yaani Willbrod alikuwa anapiga porojo za kisiasa kumbe ni kweli?
Mbona hata Mheshimiwa Spika alishasikika akielezea kwamba madokyumenti aliyokuwa anabeba huyo Dokta Slaa yanatia shaka? Si mlisikia ile azima ya Mheshimiwa sana Spika, ndugu yetu, kaka yetu msomi Samuel Sitta? Si alisikika hata kwenye luninga akionyesha nia yake ya kumpeleka Slaa kunako Polisi Post ili wakachunguze yale makabrasha?
Tunaomba mheshimiwa huyu atueleze kama kweli bado ana dhamira hiyo tena. Wakaguzi si wameshatuambia kwamba wamegundua kuna ulaji haramu huko kwenye jumba la kuhifadhia fedha? Nasema tumeingiliwa mwanakwetu.
Eti huyu Ballali aliyetimuliwa kwenye kiti cha ugavana si ndiye aliyesikika akijiapiza kwamba yeye yu safi na tena hajiuzulu?
Tulimsikia kwa masikio yetu na kumuona kwa macho yetu wakati akijiapiza hivyo. Tazama sasa amepigwa teke na kuachia ngazi bila ustaarabu wowote. Wenzake si wanamalizia utumishi kwa kugonganisha bilauri huku wakiropoka chiaaaaaaz?
Yeye kasukumwa nje bila staha mwanangu huku wapambe wakitaka akamatwe na kuwekwa lokapu. Huko najitoa mimi wala simo tena.
Hebu turudi kwa wabunge wetu watukufu hasa wale wa chama tawala. Chonde chonde enyi wabunge, msiwe na itikadi linapokuja suala la masilahi ya taifa. Si mmeona hata REDET wanadai eti heshima ya taasisi ya Bunge imepungua? Sina hakika lakini nadhani kile kibuti mlichompiga mdogo wangu Mheshimiwa Zitto kimechangia.
Si alikuwa akidadisi mambo kwa masilahi ya taifa? Mwanakwetu nasikia mwisho kibao kikageuka baada ya mtuhumu kugeuka mtuhumiwa na kuhukumiwa kwamba kawadanganya waheshimiwa. Yarabi toba, huko simo miye.
Hata hivyo kiaina fulani si kama hoja yake nayo imepita? Kwani si tume imeundwa na rais kushughulikia hayo mambo ya madini? Haidhuru, yeye alitaka tume ya Bunge lakini sasa ipo tume ya rais.
Na Dk. Slaa si alisema hadharani kwamba amelazimika kuichomoa hoja yake na akaamua kwenda kuisema kwa wananchi? Mambo si ndiyo haya mwayaona? Rais kaibuka na kumwondoa bila shangwe gavana.
Bado mwashangaa REDET wakisema JK yuko juu kuliko wengine mbele ya macho ya umma?
Ni matokeo ya madodoso hayo, si maneno ya Mzee wa Kujitoa. Huko nasema simo tena simo kabisa mtoto wa mama miye.
Halafu wabongo mnanishangaza kweli kweli. Kibaka akiiba kamkufu mnakodhania ni kadhaabu, hamkawii kumgeuza mshikaki.
Mwabisha hatujashuhudia watu wanaodaiwa kuwa na hasira kali wakiwavisha vibaka matairi na kuwachoma? Mbona tumeshuhudia watu wakinyofolewa nafsi kwa madai ya kuiba nokia za promosheni?
Na huko kwenye mahabusu zetu si wamejaa vibaka wanaokaba kwa ajili ya njaa zao?
Mbona hawa wezi wa mali ya umma hawajakamatwa Yarabi? Eti si tunashuhudia watu kibao wakikamatwa halafu upelelezi unaendelea wakati tayari wameshapandishwa kizimbani?
Mbona katika hili sakata la bilioni 133 hatujasikia aliyenaswa na kuwekwa mbaroni? Tukishangaa katika hili eti mtatushangaa kwanini tunashangaa? Nasema kama kawaida najitoa katika haya. Simo!
Mama Meghji naye kanifurahisha kwa kauli yake kwamba alipigwa fiksi na Gavana bwana Ballali! Ebo!
Kumbe hata huko kwenye maofisi matukufu kuna fiksi? Mama wa watu kaambiwa hela ni kwa ajili ya shughuli maalumu za kiserikali, kumbe zikaingia kwenye matumbo ya wale mnaodhani ni wafanyabiashara maarufu.
Kiama kweli kinakaribia. Iweje huyu mama ambaye mashabiki wake wanamwita 'Iron Lady' adanganywe kirahisi namna hiyo? Kuna matumizi ya serikali yasiyokuwa na dokumenti?
Nini kilimfanya ajiridhishe kwamba wakubwa hawasemi uongo hata akamwaga wino kwenye barua akisema malipo ya karibia bilioni 40 ni sawa, tena yamefuata sheria?
Alikuwa amejiridhisha kwa dokumenti na sheria zipi? Eti hapo huyo mama si akubali tu, aliteleza hata kama hakuanguka? Huko simo mtoto wa watu. Nikimbie mbio mimi.
Vyombo vya habari vinadai huyu Mheshimiwa Meghji alikuja kugundua kwamba amepigwa fiksi siku nne baadaye. Hiyo mwazungumzia Septemba, 2006 mwanangu! Eti tangu 2006 alijua kuna vibaka kwenye ofisi nyeti? Kilichokuwa kinazuia huyo Ballali kufukuzwa kazi ni kipi hasa hadi ifike 2008? Mwanangu bado kuna vitu sivielewi vizuri hapa.
Na Dokta Slaa aliposimama na kuanza kurapu kuhusu Benki Kuu huyu Mheshimiwa Meghji hakumsikia wala hakukumbuka hizo fiksi alizokuwa amepigwa na Ballali?
Si angesimama kuungana mkono na Slaa kwamba jikoni kuna vibaka wanabaka uchumi wetu? Au kanuni ya kusimama kwa pamoja ilimfunga? Maswali ni mengi kuliko majibu mwanakwetu.
Hawakawii kusema eti waliagiza maodita kuanza kazi.
Mtu adanganye 2006 halafu maodita waanze kazi mwaka mmoja baadaye bado hakuna cha kushangaza hapo? Mbona walianza kazi baada ya vuta nikuvute ya bungeni hadi Dk. Slaa akaamua kuchomoa hoja na kuipeleka kwa wananchi?Kwani yawezekana tamko la wakubwa wa Ulaya halikuhusika kwa namna yoyote na kuanza kwa ukaguzi huo?
Nasema maswali yanazidi majibu mwanakwetu. Huko simo tena simo kabisa wala siingilii sana maana tindikali bado zinauzwa madukani. Simo!
Piga ua mwanangu. Waliopora hizo hela tunataka tuwaone kwenye karandinga wakipelekwa iwe ni Segerea au Ukonga au Karanga.
Hata ikibidi kwenda Isanga wacha tu wapelekwe. Ninyi mwahangaika kuandamana kupinga kinachodaiwa wizi wa kura Kenya lakini hamjafanya kitu kuhusu wizi wa fedha kwetu?
Kwani si tunataka tuwaone mkiweka shinikizo walioiba wakamatwe? Nikimbie mbio kukingali mapema. Nasema katika haya yote wala miye simo. Mkiulizwa msinitaje.
source: Tanzania daima leo
kevinmakyao@hotmail.com
0784 265072