Arusha, Kilimanjaro, Mbeya zaongoza kwa viriba-tumbo

Arusha, Kilimanjaro, Mbeya zaongoza kwa viriba-tumbo

Mbega Daniel

New Member
Joined
Jul 16, 2015
Posts
4
Reaction score
0
IMG_20211018_121332_2.jpg

MIKOA ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Unguja Kaskazini inaongoza kwa wanawake wenye unene wa kukithiri, maarufu kama ‘viriba-tumbo’ (obesity).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Germana Leyna, ameeleza hayo katika mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu, Oktoba 18, 2021 wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yatakayofanyika mjini Tabora Oktoba 23.

Dkt. Leyna alisema, mikoa hiyo ina kiwango cha hadi 49% cha wanawake wenye viriba-tumbo na kuonya kwamba, ikiwa jamii haitabadilika na kuzingatia mlo kamili, hali hiyo inaweza kusababisha watu kupata magonjwa yasiyoambukiza.

“Ni muhimu jamii ikapata mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula vyote vya aina tano (wanga, vitamin, protini, mafuta, mbogamboga na matunda) kwa sababu badala ya kupambana na utapiamlo wa ukosefu wa chakula, sasa kuna tatizo la viriba-tumbo ambao ni unene wa kuzidi,” alisema.

Tatizo la uzito uliokithiri (viriba-tumbo) kwa wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15 hadi 49) limeongezeka kutoka 29.7% mwaka 2014 hadi 31.7% mwaka 2018.

“Uzito uliozidi (kiribatumbo) ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayosababishwa na ulaji duni pamoja na mitindo mibaya ya maisha kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, figo na baadhi ya saratani,” anasisitiza.

Alisema, maadhimisho ya mwaka huu yanatanguliwa na wiki ya maonyesho ya chakula na lishe kuanzia Oktoba 18 hadi 22 na kwamba siku ya kilele, Oktoba 23, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, ndiye atakuwa mgeni rasmi.

Dkt. Leyna amesema, lishe bora ni msingi wa uhai, ukuaji wa maendeleo ya binadamu kimwili na kiakili na kwamba huongeza uwezo wa mtu kufanya kazi na hivyo kuchangia kuongeza tija katika uzalishaji mali kwa kaya na taifa kwa ujumla.

“Umuhimu huo wa lishe katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi umepewa kipaumbele na kuwekewa mikakati ya utekelezaji katika malengo ya maandiko mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwemo Malendo Endelevu ya Maendeleo 2030, Malengo ya Baraza la Afya Duniani 2025, Agenda ya Afrika ya mwaka 2063 pamoja na Ilani ya Chama tawala (CCM) ya mwaka 2020-2025,” alisema.

Takwimu zinaonyesha kuwa, hali ya lishe nchini inazidi kuimarika kutokana na kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria, mathalan kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndicho kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka 34.7% mwaka 2014 hadi 31.8% mwaka 2018, kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa wa hali ye lishe wa mwaka 2018.

Hata hivyo, licha ya kupungua huko, lakini kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO kwa mwaka 1995) kiwango hicho bado kinaashiria hali mbaya ya lishe na inakadiriwa kuwa nchini Tanzania kuna watoto zaidi ya milioni tatu ambao wamedumaa.

Idadi kubwa ya watoto hao waliodumaa ipo katika mikoa 11 ambayo ni Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Mara, Dodoma, Geita, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Morogoro na Tabora.

Dkt. Leyna anasema, kiwango cha ukondefu kimepungua kutoka 3.8% mwaka 2014 hadi 3.5% mwaka 2018.

“Pamoja na kupungua kwa kiwango hicho lakini bado kuna takriban watoto 600,000 wenye utapiamlo mkali (acute malnutrition) na wa kadiri, tatizo la uzito pungufu nalo limeongezeka kutoka 13.4% mwaka 2014 hadi 14.6% mwaka 2018,” alisema.

Anasema, kwa watu wazima, tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15 hadi 49) limepungua kutoka 44.8% hadi 28.8% kati ya mwaka 2014 na 2018.

Ili kukabiliana na matatizo hayo, Dkt. Leyna alisema, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuboresha hali ya lishe nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya, uongezaji wa madini joto kwenye chumvi, kutoa virutubishi vya nyongeza kwa makundi maalum huhususan wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Pia, wanahimiza kanuni za ulishaji sahihi kwa watoto wadogo na wachanga, kutoa chakula dawa kwa ajili ya kutibu watoto wenye utapiamlo mkali na wa kadiri pamoja na kuanzisha siku ya lishe kitaifa ili kuuelimisha umma umuhimu wa lishe bora.

“Lengo la kuanzisha siku ya Lishe Kitaifa ni kuwaleta kwa pamoja wadau wa lishe ambao ni viongozi, wanasiasa, watendaji, wataalam, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi ili kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa lishe kama ni msingi wa afya bora na maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” anasema Dkt. Leyna.

Anabainisha kwamba, shughuli zinazofanyika katika wiki ya maonyesho hayo mwaka huu ni kutoa elimu kwa jamii juu ya utayarishaji wa mlo kamili kwa makundi mbalimbali wakiwemo watoto, vijana, wajawazito na wanawake wanyonyeshao, wazee, wagonjwa na watu wengine na kusisitiza umuhimu wa lishe bora katika kujikinga na magonjwa.

“Tunafanya maonyesho ya utayarishaji na maandalizi yam lo kamili kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo husika, kufanya uchunguzi wa afya na hali ya lishe kwa watu wote pamoja kutoa ushauri stahiki.

“Kufanya maonyesho ya bidhaa na vyakula vilivyoongezewa virutubishi kutoka shambani au viwandani,” alisema na kuongeza kwamba lishe bora huimarisha kinga ya mwili na husaidia kupunguza ukali wa maradhi pamoja na vifo vitokanavyo na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo Uviko-19.
 
Back
Top Bottom