Baada ya kutua jana kwa akitokea uhamishoni Canada alipokimbilia kwa takribani miaka 2, mwanasiasa machachari na maarufu aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema alipokelewa kwa shangwe kubwa na wafuasi wake na tayari ameibua mijadala ambayo ilikosekana kwa muda mrefu sana.
Mijadala hiyo ni pamoja na uhai wa upinzani kutokana na ukubwa wa umati wa wafuasi wake , mahusiano ya serikali na upinzani ikizingatiwa kufika kwake uwanja wa ndege kuliingiliana na msafara wa Rais bila matatizo yoyote, aina ya hotuba aliyotoa ambayo sasa ameibua mjadala mwingine mkubwa kuhusu aina ya ajira ya bodaboda ambayo kwa masikitiko makubwa imekuwa kimbilio kwa vijana wengi taifa hilo hata wale ambao ni wasomi.
Haya yote ni mambo mazuri sana yaliyokosekana kwa kipindi fulani, yanapaswa kuendelea na kushamiri zaidi kutoka kwa wanasiasa kama tunataka nchi nzuri yenye fursa sawa kwa wote na yenye demokrasia imara. Kufika kwa Lema ni mwamko zaidi na afya kwa taifa letu.