Askofu Bagonza: Taifa lililoungana linaweza kupambana na Mabeberu

Askofu Bagonza: Taifa lililoungana linaweza kupambana na Mabeberu

Richer

JF-Expert Member
Joined
Jun 9, 2025
Posts
2,318
Reaction score
4,079
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Askofu Dkt. Benson Bagonza, amesema Taifa lililoungana lina uwezo wa kupambana na Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Pia akisisitiza kuwa hatari kubwa kwa Tanzania si “mabeberu” wa nje pekee bali migawanyiko na viongozi wasiosikiliza wananchi. Ameikumbusha serikali umuhimu wa uwazi, uwajibikaji, sheria sawa kwa wote na uongozi unaosikiliza wananchi kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Nyerere. Ametahadharisha kuwa taifa limevurugika, watu wamekufa, masanduku ya kura hayajahesabiwa, na kelele za wananchi zikiendelea, hivyo haja ya umoja na maridhiano ni ya lazima ili kuepusha migogoro zaidi.

Maelezo hayo ameyaandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa "Facebook"

TAIFA LILILOUNGANA LAWEZA KUPAMBANA NA “MABEBERU”.
Dhana ya Ubeberu uwa sipendi. Inatufanya sisi tuonekane ni “mbuzi jike” na wale ndio “mabeberu” wanaotubananga bila sisi kutaka. Lakini ukweli ni kwamba, mabeberu tunao humu humu ndani na wananchi tumegeuzwa kuwa kama mbuzi jike ili kuwa kiburudisho cha mabeberu yetu.

Pande mbili zinazovutana, zinatuhumiana kutumiwa na mabeberu. Gen Z wanaituhumu serikali kutumiwa na mabeberu kuuza utu, raslimali na uhuru wetu. Serikali inawatuhumu Gen Z kwa kutumiwa na mabeberu kuvuruga amani yetu. Mimi niwakumbushe:

1. Taifa lililoungana lina uwezo wa kupambana na EU, World Bank na IMF. Linaweza kupambana na AU, SADC na majirani wenye chokochoko. Tumegawanyika. Kilichotugawa, hakiwezi kutuunganisha. Inahitajika kafara. SIPENDI. Ya Yesu ilitosha msalabani. Huku kitaani hakuna “vya Yesu”.

2. Enzi za Mwalimu, alipowatindinganya IMF na World Bank au alipowahondomola majirani wabaya kama Kamuzu Banda na Idd Amini, tuliandamana bila kupewa posho na bila kufundishwa tuandike nini kwenye mabango. Toka Kazura Mimba hadi Lukuledi tuliandamana kwa kutaka wenyewe tena kiroho safi.

3. Lilipotokea tatizo la kiuongozi, Mwalimu alikuwa msikivu. Hakuwasikiliza washauri. Aliwasikiliza waswahili. Niliwaona Wasukuma wanamshinikiza Mwalimu hadharani amfukuze RC. Alimfukuza siku hiyo usiku. Niliwaona wazee wanatishia kuvua nguo mbele ya Mwalimu huko Butiama kulalamikia mateso ya Polisi na Usalama. Alichukua hatua hapo hapo.

4. “Vibaka” wetu na “wahuni” wetu wameuawa. Viongozi wetu wamekomaa kuwa hawakuwa waandamanaji bali vibaka. Sawa. Hakuna mzazi anayetunga mimba ya kibaka. U-kibaka hutengenezwa hapa duniani. Tuambieni wamekufa vibaka wangapi ili tulale usingizi na milango ibaki wazi.

5. Kama ni vibaka tuonyesheni waliowaua ili tuwape maua yao. Tunasikia kuna polisi wetu wema waliuawa na vibaka; tutajie tuwaenzi mashujaa wetu waliokufa wakitutetea wananchi.

6. Mh. Rais Samia, DSM hakuna wazee. Uzee mwisho Chalinze. Jijini kuna washikaji wa kitaa na machawa wa kujitakia. Jihadhari nao. Mungu wao ni bahasha. Wakitaka kukushauri wanakuangalia machoni. Ukikunja uso wanabadili kauli. Hawajiamini, usiwaamini.

7. Nimewaona wananchi wanatema nyongo mbele ya mawaziri. Nimewaona mawaziri wasikivu. Nimewa-zoom Mapolisi wakiigiza kuwa mapadre. Wamekuwa kama Paka aliyeokoka na kuacha kula panya! Siyo kweli. Unaweza kumtoa Simba porini lakini huwezi kulitoa pori ndani ya simba. Wananchi wanataka serikali ya wananchi siyo serikali ya serikali. Serikali yenye nguvu kuliko wananchi HAIFAI.

8. Tunaoshauri kwa nia njema tumeitwa ni MAKAFIRI. Najua hawajatumwa na mtu. Wametumwa na njaa yao. Ningekuwa na chakula ningewatuma wanitukanie Wajaluo! LAKINI nataka wajue; Ukafiri si wangu peke yangu. Wote wanaoamini kama mimi wameitwa MAKAFIRI. Na asiye kafiri lakini amechaguliwa na makafiri, amefanywa kuwa kafiri. Hawajui wasemalo. Ni ngedere anayeucheka msitu unaoungua asijue jioni atalala wapi? Mabadiliko ya “Tabia nchi” yakikimeza kisiwa chao kwa mafuriko watakimbilia wapi kama si huku kwa makafiri? Jamani, Kitimoto iliyo karibu ni bora kuliko kondoo wa mbali!

9. Tunahitaji Taifa lililoungana. Sheria moja kwa wote; bunge moja kwa wote; serikali moja, mbili au tatu LAKINI kwa wote. Atakayeachwa nje, aachwe kihalali, siyo kwa mizengwe ya kuvaa dela lililojaa kura. Sichochei, lakini kelele za wapita njia siku hizi zinakosesha usingizi. Tatizo kubwa ni pale wenye macho wanapokula na kipofu halafu wakamgusa mkono. Utawasikia, “kura pigeni popote lakini dola ni yetu”, au “ hatutoki mpaka Yesu arudi”. Kweli?! Jamani, wakati wa njaa huwa tunangojana wakati wa kula.

10. Wapo wanaosema hili nalo litapita.
Wapo wanaosema risasi tunazo za kutosha. Wapo wanaosema tuwateke wataogopa. Na wapo wanaosema kila mtu ana bei, tutamnunua. Lakini, Kuna watu wamekufa. Kuna watu wana mabox ya kura mpaka leo. Hayajahesabiwa lakini washindi wameishaanza kazi. Huko jikoni biashara ya kuvujisha siri imepamba moto! Tumelivuruga taifa letu. Mama yangu mzazi bado yu hai! Alinichapa sana kwa makosa ya wadogo zangu. Tumchape nani kwa makosa ya waliofanya makosa? Basi wajichape itapunguza hasira.

Mke mwema wa Kijaluo huwa hakwepi ngumi ya mmewe. Mjaluo mzuri ni aliyekwisha kufa tu. Walio hai wote matapeli. Mkichukia mtanilipa. Bora mtabasamu, siku ipite.
Imeandikwa na KAFIRI MWANDAMIZI.
(Wale mnaopenda niwe Kafiri, nimekubali. Furahini sasa shida zetu ziishe).


1764655194445.png
 
Sawa! Yaani hapa ni kama unampigia gitaa mbuzi.
Serikali ya CCM ina Kiburi cha Shetani.
Nadhani muda wa kuishauri serikali umekwisha!
 
Mabadiliko ya “Tabia nchi” yakikimeza kisiwa chao kwa mafuriko watakimbilia wapi kama si huku kwa makafiri? Jamani, Kitimoto iliyo karibu ni bora kuliko kondoo wa mbali!
Ila Bagonza bana dah! 😂😂😂
 
Back
Top Bottom