Josephat Gwajima ni Askofu na mwanzilishi wa kanisa la 'Glory of Christ Tanzania Church' GCTC (Ufufuo na Uzima Ministries), kadhalika ni mwanasiasa ambaye mwaka 2020 alichaguliwa kuwa
mbunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
Tarehe 24 Mei, 2025 Gwajima alifanya
mkutano na waandishi wa habari ambapo alisema kumekuwa na mlolongo wa matukio ya watu kutekwa pamoja na kupotea hivyo kutokana na hayo ameamua kuitisha mkutano na waandishi wa habari kuongelea kuhusu suala hilo na kisha kutoa ushauri wake.
Kutokana na mkutano huo mtumiaji mmoja wa mtandao wa X, kwa jina la 'SEMA NAE' alichapisha
taarifa iliyotumia utambulisho wa Millard Ayo kuwa, Askofu Gwajima aliitaja CHADEMA kuhusika na utekaji na mauaji ya Ali Kibao.
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Kupitia ufuatiliaji wa kimtandao kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key Word Search) pamoja na marejeo ya video ya mkutano huo, JamiiCheck imejiridhisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli.
Chapisho lililotumika kusambaza taarifa hiyo si la kweli, bali ni la kughushi kwani halijachapishwa na
Millard Ayo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii. Hata hivyo taarifa iliyochapishwa na
Millard Ayo kuhusu mkutano huo ilikuwa na kichwa cha habari 'Matukio ya utekaji yanachafua nchi' ikieleza kuwa Gwajima alikemea vitendo vya utekaji vinavyoendelea nchini na kwamba vinaharibu taswira ya Tanzania.
Aidha kupitia
mkutano wake na waandishi wa Habari Gwajima hakukituhumu chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kuhusika na tukio la kutekwa na kuuawa kwa Ali Kibao bali
alitoa ushauri wa namna ya kukomesha matukio ya utekaji nchini kwa si utamaduni kwa kitanzania huku
akigusia tukio Ali Kibao kama sehemu ya mfano wa matukio yanayostahili kukomeshwa.
Unaweza kufuatilia mkutano huo kupitia kiunganishi hiki
View: https://youtu.be/U89Gm7CuGgA?si=7H6ouzVGn7GUPvqq