SoC03 Athari ya uchama nchini kikwazo cha vita dhidi ya umasikini

SoC03 Athari ya uchama nchini kikwazo cha vita dhidi ya umasikini

Stories of Change - 2023 Competition

Librarian 105

JF-Expert Member
Joined
May 6, 2023
Posts
261
Reaction score
356
Kwanini umasikini unaendelea kuwa adui wa taifa? Ni vigumu kuupatia majibu ila kwa kuugawa maeneo mawili. Nayo;
a) chini ya mfumo wa chama kimoja 1961-1992: hapa umasikini ulipigiwa vita kwa kutumia falsafa ya ujamaa wa kujitegemea uliosimamia sera ya uchumi wa kisiasa kuchochea sekta ya kilimo na viwanda ya mapinduzi ya kijani nchini. Huku Azimio la Arusha likiwa dira ya mpango wa maendeleo wa taifa ilhali serikali ikiwa bega kwa bega na wananchi katika shughuli za uzalishaji mali.

b) mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 na kuendelea : hiki ndicho kipindi ambacho,kwa shinikizo la nchi za magharibi, tulifuata uchumi wa kibepari bila utayari wa kitaifa kujiandaa na mageuzi kamili ili kutoathiriwa na utandawazi duniani. Na ndipo kadhia ya uchama ilipoanza kuwa kikwazo cha vita dhidi ya umasikini nchini kama ifuatavyo:

KISIASA:
Kwa mujibu wa ibara ya katiba 3(1) na 9: ni vigumu kuutokomeza umasikini nchini kutokana na nchi kufuata siasa za ujamaa na kujitegemea wakati huo huo pia kufuata mfumo wa kidemokrasia na vyama vingi. Ambayo kwayo ni mifumo miwili isiyoiva ndani ya chungu kimoja. Hapa akili yangu inakataa kuamini hii ilikuwa ajali ya kisiasa iliyosababishwa na uchanga wa taifa letu. Bali naweza kusema utashi wa kisiasa ulitumika ili kulinda nafasi ya chama tawala wakati huo dhidi ya matokeo ya siasa za ushindani. Hatua ambayo kwayo uchama ukajiimarisha hadi hivi leo kama ifuatavyo hapa chini:
  • kuhodhi mihimili ya dola hata kuathiri mabadiliko ya kweli ya kidemokrasia nchini.
  • Ukada umezuia uwazi wa ajira za umma na uzalendo katika utumishi wa umma.
  • Nyuma ya uchumi wa kisiasa uchama umejitengenezea ubepari wa kichama nchini. Mbinu hii imekisaidia chama na pia kujenga mazingira kwa chama kingine kitakapoingia madarakani kudhibiti utawala wa kidemokrasia na kujipa nguvu ya ushawishi kwa wananchi. Kuwa ndicho pekee chenye uwezo wa kuongoza na kuleta maendeleo.
KIUCHUMI:
Ubepari wa chama nchini umewapa uwezo viongozi wa umma kukipendelea chama kutawala sera za nchi kiuchumi kwa taswira zifuatazo:
  • uchumi wa kisiasa umedhiti nguvu ya soko huria na njia kuu za kiuchumi nchini.
  • Ilani ya chama kuwa ndio tafsiri na dira ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa taifa.
  • Maslahi ya chama kukaa sehemu ya maslahi ya nchi katika ajenda za kitaifa zenye kuhoji uwajibikaji wa serikali.
Kwa njia hii, utendaji wa serikali umesabisha ukiritimba katika ofisi za umma, njia kuu za kiuchumi na maliasili na rasilimali za taifa kuangukia mikononi mwa watu wachache. Kiasi cha kuathiri miradi ya maendeleo huku kashfa za rushwa na ufisadi zimekuwa miongoni mwa sababu za umasikini kushamiri nchini. Pia kuweka mazingira magumu ya kuikosoa na kuihoji serikali na taasisi zake, mashirika ya umma, na bajeti za nchi pamoja na miradi ya maendeleo pindi inapohujumiwa. Hili tunaliona mara kwa mara kupitia ripoti za CAG pamoja na nguvu ya uchama inavyotumiwa kulinyima bunge mamlaka ya kuhoji baadhi ya mikataba ya uwekezaji yenye kuweka maslahi ya umma mashakani. Haitoshi mwananchi amegeuzwa kuwa mtaji wa kisiasa katika vita dhidi ya umasikini. Na mbaya zaidi uchumi wa nchi kunyimwa fursa ya kuzalisha mamilionea wapya wazawa nje ya ulingo wa ushirika wa kisiasa au ushirika wa siri wa kibiashara na viongozi wa dola wasio waadilifu.

KIJAMII:
Ukirejea kifungu cha katiba ya nchi 145(1-2); serikali za mitaa zilianzishwa ili kupeleka madaraka ya umma kwa wananchi kwa shabaha ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia nchini sanjari na kuharakisha maendeleo ya wananchi. Walakini uchama umekuwa kikwazo kwa mambo yote mawili kupatikana kwa muktadha wa ibara ya 3(1) na 9 kuathiri misingi ya demokrasia nchini kisiasa na kiuchumi.

Leo hii inahuzunisha kusikia vilio vya mmomonyoko wa maadili na demokrasia nchini kugandamizwa. Huku dola ikipuuza kilio cha watetezi wa misingi ya kidemokrasia nchini na vuguvugu la mabadiliko ya katiba mpya. Matokeo yake vita vya umasikini vimekuwa vigumu kutokana na utendaji wa tawala za mikoa na serikali za mitaa kuwa matanuri ya miradi ya maendeleo ya nchi. Na kwa namna moja au nyingine huduma za kijamii nazo zimegeuzwa kuwa mtaji wa kisiasa ili kulinda maslahi ya chama kwa kigezo cha utekelezaji wa ilani ya chama. Hata kufanya mamlaka za serikali za mitaa kugeuka kuwa maabara za kupeana ajira kwa kuchunguzana kwanza ukada.

HITIMISHO
Hitajio la umma sasa hivi ni kupatikana kwa katiba mpya. Ila ukweli unabakia kuwa kikwazo ni uchama ambapo chama tawala kwa sasa kuna wahafidhina ambao wanazuia maridhiano ya kitaifa kwa vyama vyote nchini kuwa katika mzani sawa kwa mujibu wa katiba. Sivyo tunaweza kuipata katiba mpya ila isitufae kitu. Tukitazama huo uhalisia ulio mbele yetu. Chanzo chake ni kupuuzwa kwa uwepo wa dira ya taifa wakati wa kukubali mfumo wa vyama vingi ulio muongozo wa wadau wote wa maendeleo kisiasa na kiuchumi.

Nikitathmini hivyo. Naona kabisa uendelezwaji wa utamaduni wa uchama kwa yoyote aliye madarakani kutumia mamlaka za nchi kulinda chama chake kwanza. Ambao ni udikteta wa chama uliojificha nyuma ya utumishi wa umma kulinda maslahi ya wachache. Hivyo kuwa kikwazo cha mchakato wa mabadiliko endelevu ya kitaifa na mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Ilhali taswira yetu nje ya mipaka ya nje, tunaheshimiwa kuwa kisiwa cha amani na kuwa wapatanishi wa nchi zingine zinazokumbwa na migogoro ya kisiasa, inafikirisha kuona hatuutumii ukomavu huo wa kisiasa kwa manufaa ya taifa letu wenyewe.

Mwisho, chama tawala cha sasa hakina budi kusikia kilio cha mabadiliko ya katiba mpya, kwani kinasiwiri athari ya uchama kujivika ufalme juu ya sheria ya nchi. Wala isichukuliwe kuwa tofauti zetu za kisiasa ndizo zinazochelewesha maendeleo nchini. Kila mtanzania anatamani kuitumikia nchi yake kiufanisi katika kustawisha amani na vita dhidi ya umasikini nchini. Je, tutafikiaje lengo hili bila umoja wa kitaifa unaoathiriwa na uchama kudhitibiti siasa za nchi kisiasa na kiuchumi?

Tujitafakari.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom