Mbunge wa Tabora Kaskazini, Mh. Athuman Maige ameitaka serikali kufanya utafiti wa kina kuhusu lugha ya kufundishia nchini Tanzania. Mbunge huyo amesema "Ziko tafiti zaidi ya 40 zimefanyika na zote zinasema lugha inayofaa kufundishia Tanzania ni Kiswahili, naomba serikali ifanye tena utafiti mahususi kwa ajili ya lugha ya kufundishia kwa Tanzania,"
Aidha Mh. Maige ameongeza kwa kusema "Duniani kote hakuna nchi iliyoendelea kwa kutumia lugha ya watu wengine, Uingereza wanatumia kiingereza, Wachina kichina, lakini Tanzania tunatumia lugha ya kufundishia ni Kiingereza, watoto wanasoma Kiswahili darasa la kwanza hadi la 7,"
Kauli hii inakuja baada ya mjadala mkali unaoendelea kuhusu ipi ni lugha sahihi ya kufundishia nchini Tanzania ambapo baadhi ya wadau wakitaka jitihada zaidi iwekwe kwenye kuwafundisha watoto kiingereza huku wengine wakitaka lugha ya kufundishia ibadilishwe na kuwa kiswahili kwa ngazi zote kuanzia Shule za awali mpaka chuo kikuu huku lugha ya kiingereza ikifundishwa kama somo.
Tatizo hawa watu hawaelewi mambo ya msingi yanayotakiwa kuangaliwa kabla hujasema utumie lugha ipi kufundishia.
Watasema tu kuwa Waingereza wanatumia Kiingereza, Wajapan wanatumia Kijapan, Wachina wanatumia Kichina, hawaendi zaidi ya hapo.
Hawajiulizi kwa nini Wamarekani wanatumia Kiingereza wakato siyo Waingereza, Waswizi wanatumia Kifaransa wakati siyo Wafaransa, Wakanada wanatumia Kiingereza wakati siyo Waingereza, Brazil wanatumia Kireno wakati siyo Wareno, etc.
Huwezi kuamka tu, na kusema naanza kutumia lugha fulani.
Nguvu ya lugha hutegemea nguvu ya uchumi, teknolojia na sayansi.
Tanzania, hata leo hii, tuamue kuwa kuanzia Primary mpaka University, kitumike Kiswahili, wengi wenye uelewa watahangaika kuwapeleka hata mataifa jirani ili watoto wakasome kwa Kiingereza.
Mchina, kwa sasa, anazidi kuongeza vyuo vinavyotoa degree kwa Kiingereza, na pia kuna shule nyingi na vyuo, wanazidi kufungua vya kufundisha lugha ya Kiingereza, unadhani ni kwa sababu gani?
Nchi ikiwa na uchumi imara, teknolojia ya juu na Sayansi, watu wa lugha nyingine, watahangaika kuifahamu lugha yako ili kuzipata fursa zinazopatikana kwako, fursa za uchumi, teknolojia, biashara na sayansi. Nchi ikiwa hohe hahe, ni wachache sana watakaojishughulisha kuifahamu lugha yako. Ukiwatengenezea mazingira wananchi wako wang'ang'anie kutumia hiyo lugha yako katika kupata maarifa, unazidi kuwaua.
Unaweza kuhangaika kutafsiri vitabu vya Kiingereza kwenda Kiswahili ili uwafundishe watu wako kwa Kiswahili lakini ujue kuwa vitabu vya kufundishia ni sehemu ndogo sana ya rejea ya maarifa. Kama hujui Kiingereza, Kifaransa na Spanish, utayakosa maarifa mengi maana makala mbalimbali, rejea, histotia, ugunduzi, vyote vipo katika lugha hizo.
US na Canada, zilikuwa nchi za Wahindu wekundu ambao lugha yao haikuwa Kiingereza. Lugha yao ilipotea kutokana na wahamiaji matajiri toka nchi za Ulaya, ambao wengi wao walikuwa wanaongea Kiingereza. Mpaka leo Kiingereza ndiyo lugha ya Taifa la Marekani na Canada.
Tukitaka lugha itusaidie kupiga hatua kwenye maandeleo katika nyanja nyingi, masomo yote yafundishwe kwa Kiingereza, na Kiswahili kifundishwe tu kama lugha ya mawasiliano yetu ya kila siku. Siyo kitu cha ajabu. Hata hapo kale, wakati wa Masiha Yesu Kristo, huko Uyahudi, Kiebrania (hebrew) kilitumika kama lugha ya mawasiliano ya kawaida kwa Wayahudi, na Kigiriki kilitumika kama Lugha ya wasomi (wengine waliita lugha ya kitaalam). Mpaka leo, Kigiriki kina maneno na alama nyingi, hasa kwenye Sayansi na dini. Mfano herufi ya alfa, omega, etcetera (etc), exampli gratia (e.g.)