Nimeona hili tamko japokuwa liko nyuma sana lakini nikaona labda niliweke hapa mpate kusema lolote .
RAIS AINGILIE KATI TATIZO LA MIKOPO WA ELIMU YA JUU
ARUSHA
Vijana wa CHADEMA waitika mwito wa Rais Kikwete,
kuwakusanya wanasiasa na wasomi kujadili sheria ya
madini na ufisadi nchini
Taarifa ya Kongamano lao la Wanavyuo zaidi ya 2000
kutolewa wiki ijayo
Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA inamuomba Rais Kikwete
kuingilia kati matatizo ya mikopo kwa takribani
wanafunzi mia tatu(300) wa Chuo cha Uhasibu
Arusha(IAA). Wanafunzi hao wako kwenye uwezekano
mkubwa wa kushindwa kuendelea na masomo na baadhi yao
wamesharejea nyumbani baada ya kujulishwa kwamba Bodi
ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) haitawapatia mikopo
ya kuwadhamini masomo yao.
Wanafunzi wa fani mbalimbali zikiwemo biashara, benki,
uhasibu, ugavi, kodi na fedha wengi wao wakiwa ni
wasichana waliopata daraja la tatu wamefika chuoni
hapo baada ya kuomba na kutimiza vigezo vya kudahiliwa
kujiunga na chuo hicho(admission criteria), na baada
ya kupata udahili(admission) waliwasilisha maombi yao
Bodi ya Mikopo na wakakubaliwa kupata
udhamini(sponsorship) kwa viwango mbalimbali kwa
kadiri ya mahitaji yao.
Tangazo la kustahili kwao kupewa mikopo lilitolewa na
bodi katika tovuti yake ya
www.heslb.go.tz tarehe 11
mwezi Septemba mwaka 2007 wiki chache baada ya
kumalizika kwa kikao cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma.
Inasikitisha kwamba hawa waliwasilisha maombi bodi ya
mikopo baada ya kupata udahili(admission) kwa maana
nyingine bodi ilikuwa inajua kabisa ni fani zipi
wanakwenda kusomea. Bodi ikawakubalia na kutangaza
majina yao na viwango vya mikopo wanavyostahili
kupata. Mpaka hivi leo tarehe 7 Novemba 2007 majina
yao bado yapo kwenye tovuti ya bodi ya mikopo katika
kundi la wanaostahili kupewa mikopo. Inasikitisha
kwamba mpaka sasa hawajapewa mikopo yao. Na tayari
viongozi wao wa wanafunzi wamewaeleza kwamba bodi
imewajulisha kuwa hawastahili kupewa hata shilingi
moja. Kinachoshangaza zaidi ni kwanini bodi inaacha
kutoa tangazo la kubatilisha tangazo lake la awali
badala yake maofisa wabodi wanawadokeza tu viongozi wa
wanafunzi wawaambie wenzao. Ni vyema taarifa rasmi
ikatolewa na bodi yenyewe moja kwa mojan kufafanua
suala hili.
Tangazo hilo la bodi ambalo liko sehemu ya habari
mpya(current news) limetaja daraja za viwango vya
mkopo mbele ya kila jina la mwanafunzi katika orodha
hiyo ya wanaostahili kupata mikopo- alama zilizowekwa
ni pamoja na A(100%), B(80%), C(60%), D(40%), E(20%)
na F(0%). Kutokana na tangazo hili la bodi vijana hawa
wengi wakiwa wanatoka familia masikini walifunga
safari toka majumbani mwao na kuja kuanza masomo kwa
matarajio ya kupata mikopo kama ambavyo bodi
imetangaza.
Nimekutana na baadhi ya wanafunzi hao hapa Arusha,
hali yao ya kifedha wengine ni mbaya sana. Wengi wako
darasani lakini wanashindwa kusoma kutokana na kuhofia
hatma yao, huku ni kuwapa msongo na matatizo ya
kisaikolojia wanafunzi na hatimaye kuathiri maendeleo
yao chuoni. Baadhi wanataka kurudi majumbani kwao
lakini hata nauli hawana. Hali inakuwa ya hatari zaidi
kwa wanafunzi wa kike. Hii ni kama vile wametelekezwa.
Tangazo toka kwa taasisi ya serikali kama bodi ya
mikopo ni sawa na mkataba wa maneno kati ya serikali
na mwananchi. Utamaduni kama huu ukiendelea utawafanya
wananchi wasiwe wanaamini matangazo ya serikali yao.
Na tukifikia hapo kasi ya maendeleo itakuwa mashakani.
Ndio maana katika hatua hii tunamuomba Rais aiingilie
kati kunusuru maisha ya vijana hawa wakitanzania.
Itakumbukwa kwamba Rais Kikwete aliwahi kufanya
mkutano na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dar es salaam
kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya CCM tarehe 3
Februari 2007 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo
(baada ya kusikiliza risala ya wanafunzi) aliahidi
(kama mwenyekiti wa chama tawala) kwamba atawasiliana
na chama chake kutafuta ufumbuzi wa suala hili na
kwamba taarifa zingetolewa baada ya mwezi mmoja kuhusu
hatua ambayo ingefikiwa. Pia akasisitiza kwa namna ya
pekee kwamba hakuna mwanafunzi atayeshindwa kuendelea
na masomo kwa kushindwa kuchangia gharama za elimu ya
juu.
Ahadi hii ya Rais ilikuwa ni mwanzo wa mwaka. Leo
tunaelekea ukingoni mwa mwaka matatizo ya mikopo ya
elimu ya juu bado yapo katika vyuo karibu vyote
nchini. Ni vyema Rais akaagiza watendaji wake
kumweleza hali halisi, mpaka leo kuna wanafunzi wa
vyuo mbalimbali ambao hawajapata mikopo hata wale
waliopata daraja la kwanza na la pili. Inafurahisha
kwamba wiki hii Rais Kikwete amerudia tena ahadi yake
ya mwezi Februari, amenukuliwa na vyombo mbalimbali
vya habari (7 Novemba 2007) wakati akiwapokea baadhi
ya wanavyuo ambao wamejiunga na CCM akiwa Dodoma
kwamba atakaa na Waziri wa Elimu ya Juu- Prof. Msolla
kuwasaidia wanafunzi ambao hawajapata mikopo. Ndio
maana tunaomba katika kufanya hivyo awape kipaumbele
wanafunzi hawa wa Arusha ambao wako wengi na wengine
hali yao ya kimaisha ni mbaya
Matatizo haya ya mikopo ya wanafunzi yamekuwa
yajirudia rudia kila wakati. Wakati wa utawala wa
awamu ya kwanza wa Hayati Nyerere hakukuwa na mfumo wa
mikopo ya elimu ya juu, serikali ilidhamini wanafunzi
wote kwa asilimia mia moja. Hata wakati wa utawala wa
awamu ya tatu wa Rais Mkapa pamoja na kuwa serikali
ilikuwa inatekeleza sera ya uchangiaji wa elimu ya juu
wanafunzi walikuwa wanapewa mikopo katika mahitaji
makuu kwa asilimia mia moja. Leo katika utawala wa
kipindi cha nne cha Rais Kikwete mikopo inatolewa kwa
asilimia ndogo na kiasi kinachobaki mwanafunzi
anapaswa ajigharamie mwenyewe na hata hicho kiwango
cha mkopo ambacho mwanafunzi amepangiwa kupata bado
kuna wengi hawajakipata kama hao wanafunzi takribani
300 wa Chuo Cha Uhasibu Arusha(IAA).
Hivyo, kama taifa bila kujali itikadi tunapaswa
kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu mfumo wetu wa
gharama za elimu hususani elimu ya juu. Na katika
kufanya hivyo hakuna njia ya mkato zaidi ya kuwekeza
katika elimu na kufanya elimu ya ngazi zote ikiwemo ya
vyuo vikuu kuwa kipaumbele mama cha serikali kwa
vitendo. Na ili tuweze kufikia huko ni lazima tuepuke
ufisadi, matumizi makubwa ya serikali na kuhakikisha
taifa linanufaika na rasilimali ambazo mwenyezi Mungu
amejalia Taifa letu.
Kama sehemu ya kutekeleza azma hii Kurugenzi ya Vijana
CHADEMA inaandaa Kongamano kubwa litakalofanyika
Mkoani Dar es salaam litakalojumuisha vijana hususani
wasomi zaidi ya elfu (2000) kujadili kuhusu Ufisadi na
Hatma ya Rasilimali za Taifa. Kongamano hili
limepangwa kufanyika Novemba 17 mwaka 2007 kama sehemu
ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanafunzi.
Wasomi mbalimbali wamealikwa kutoa mada katika
kongamano hili, pia wanasiasa mbalimbali wamealikwa
wakiwemo wabunge Zitto Kabwe na Dr Wilbroad Slaa.
Leo naondoka Arusha kurudi Dar es salaam kujua
maandalizi yalipofikia. Lakini nimeshatoa maelekezo
kwa Afisa Habari wetu David Kafulila na Afisa
Mwandamizi wa Vijana Taifa- Regia Mtema kuitisha
mkutano na waandishi wa habari mapema wiki ijayo ili
tutoe taarifa ya kina kuhusu watoa mada ni wakina
nani, mada ni zipi na Kongamano lenyewe litafanyika
katika ukumbi gani.
Hili ni tukio ambalo lilikuwa ndani ya Mpango wa Mwaka
wa Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA lakini imebidi mambo
kadhaa yaongezwe kutokana na matukio mbalimbali ya
kisiasa yaliyotokea hapa nchini hivi karibuni.
Baada ya Rais Kikwete kuahidi kuwashirikisha wasomi
na wapinzani katika Kamati ya Kupitia madini imebidi
tubadili kidogo ratiba ya Kongamano letu. Tumeona
tuweke mjadala pia kuhusu sheria ya madini. Lengo ni
kupata hoja mbadala ambazo tutaziwasilisha katika
kamati hiyo inayotarajiwa kuongezewa wajumbe. Sisi
tunaamini wasomi na wanasiasa hususani katika upinzani
wenye maono kuhusu rasilimali za nchi hii wapo,
kinachokosekana ni dhamira ya kisiasa ya
kuwashirikisha na kuzingatia maoni yao. Kwa kuwa Rais
Kikwete ameahidi, sisi vijana wa CHADEMA tumeona
tutimize wajibu wetu kwa kuwaleta pamoja wanasiasa na
wasomi hususani vijana kujadili suala hili. Tunapenda
vitendo zaidi ya maneno, tunaamini serikali itachukua
hatua .
Kongamano hili litadhaminiwa na vijana wenyewe(wale
wenye uwezo) kupitia michango yao midogo midogo
itayowezesha kutolewa kwa nyaraka mbalimbali za
mkutano, viburudisho na usafiri kwa washiriki. Katika
mkutano huo washiriki watapewa nyaraka mbalimbali
ikiwemo uchambuzi wa Mkataba wa Richmond, Buzwagi,
Orodha ya Mafisadi(list of shame), Sheria ya Madini na
nyaraka zinginezo.
CHADEMA ni chama kinachopokea ruzuku ndogo toka
serikalini, na wala hatuna vyanzo visivyoeleweka wa
mapato yetu. Tukio la halaiki kubwa kama hii
linahitaji nguvu ya kila mmoja wetu mpenda demokrasia
na maendeleo. Linahitaji nguvu ya kila anayekerwa na
ufisadi na anayetaka kutetea rasilimali za taifa hili.
Tumeambiwa wenzetu waliwaita wawakilishi ishirini(20)
wa wanafunzi wenzao elfu moja(1000) na kuwapa takrima
ya shilingi elfu hamsini(50,000) kila mmoja ili kwenda
Dodoma kupokea kadi za chama kwa niaba ya wenzao. Sisi
tunataka vijana wasomi wenye uwezo watambue wajibu wao
katika jamii na kukutana kujadili mustakabali wa Taifa
letu hata kama ikiwa ni kwa kuingia gharama wenyewe
kwa niaba ya watanzania wengine masikini. Kama Mwalimu
Nyerere alivyowahi kuasa, vijana wasomi ni kama mtu
aliyetumwa na kijiji kwenda kutafuta chakula kwa niaba
ya wengine walioko kwenye njaa, kijana msomi
akishindwa kukumbuka alipotoka ni usaliti.
Kurugenzi ya Vijana inaamini kwamba matatizo ya mikopo
na ukosefu wa ajira ni matokeo tu ya udhaifu katika
mifumo yetu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hivyo
mkazo unapaswa kuwekwa katika kukabiliana na vyanzo
badala ya kushughulikia matokeo katika mtindo wa
zimamoto. Tukiweza kupunguza ufisadi ni wazi tutaweza
kupata fedha za kusomesha wanafunzi wote bila kuweka
madaraja, na tukiweza kutumia vizuri rasilimali za
taifa ikiwemo madini ni wazi mazingira ya vijana wengi
kupata ajira yatakuwepo katika Taifa letu.
Leo vijana wasomi wanaahidiwa ukuu wa wilaya,
wakumbuke kuwa kuna mamia tu ya nafasi hizo na sehemu
kubwa zikishikiliwa na wazee. Lakini maelfu ya
wanavyuo wanahitimu katika vyuo vikuu kila mwaka. Na
kwa ujumla zaidi ya watanzania laki saba(700,000)
wanaingia katika soko la ajira kila mwaka huku ahadi
ya serikali ikiwa ni ajira milioni moja tu mpaka 2010
ambayo ni sawa na ajira laki mbili(200,000) kwa mwaka.
Vijana wasomi wanapaswa kujiuliza, hawa laki tano na
zaidi wanakwenda wapi kufanya nini? Ndio maana katika
kuadhimisha Siku ya Wanafunzi Duniani kurugenzi ya
Vijana wa CHADEMA tumeamua kuwakutanisha Vijana wote
bila kujali itikadi katika Kongamano kuhusu Ufisadi na
Hatma ya Rasilimali zetu.
Imetolewa 7 Novemba 2007 na:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
Mnyika@yahoo.com
0754694553