Attention Bodi Ya Mikopo Ya Elimu Ya Juu Kwa Wanafuzi(HESLB)

Attention Bodi Ya Mikopo Ya Elimu Ya Juu Kwa Wanafuzi(HESLB)

Huyu mwandishi si Mwanakijiji...
Ina maana umeanza kutumia jina jingine (Mjenga hoja)?
 
Hivi hawa watu wa bodi wanatufikiriaje sisi Watanzania? yaani kuandika vitu kama hivi kana kwamba kwenye ofisi hiyo hakuna mtu aliyewahi kwenda shule. I'm really disappointed.
 
Hivi hawa watu wa bodi wanatufikiriaje sisi Watanzania? yaani kuandika vitu kama hivi kana kwamba kwenye ofisi hiyo hakuna mtu aliyewahi kwenda shule. I'm really disappointed.

Maybe it's about time to go and shake things up....
 
Hivi kuna mtu anaweza kuhojiwa endao kuna matatizo kwenye bodi, au katika nchi yetu hakuna mtu mwenye kuhojiwa?
 
Ee bwana eeh JF kweli kiboko,hizo data ni mwisho wa maneno.Ila naona wataanza kutafuta nani kaandika.
 
Mzee Mwanakijiji,

Vipi tena? Si ungeandika tu kama siku zote, mzee Mwanakijiji?

Ungeendelea kutumia jina la Mzee Mwanakijiji, sio tu unanijengea wewe kama mtoaji hoza za nguvu lakini pia unaijengea JF.

Kwa wale ambao wanaweza kukutafuta, wanajua mwandishi wa hiyo habari ni nani hata usipotumia jina la Mwanakijiji. Kwa faida ya wale tunaotaka kuwaelemisha ingefaa kuendelee kutumia jina la Mwanakijiji, hayo ni mawazo yangu.

Jambo lingine ambalo tunaweza kufuatilia kuhusu ufisadi wa hiyo board ya mikopo ni jinsi pesa zinavyokatwa hasa kwa wanafunzi wa nje. Yaani mwanafunzi anasema amepewa mkopo milioni 3 lakini anaishia kupata dola 2000. Hata ukiweka charges na vitu vingine vyote, utakuta kunakuwa na upungufu wa dola zaidi ya 300 kwa kila mwanafunzi. Kama tuna wanafunzi hata 100 tu wanaosoma nje, bado hizo ni pesa nyingi sana kuzipoteza kila mwaka.
 
hivi inakuwaje unapomkamata mwizi wako live,bodi ya mikopo ujanja wa mbuni kuficha kichwa mchangani hautawasaidia kitu.
tunaomba pia mtoe na majina kwa wanafunzi wote waliokopeshwa na kiasi walichopata.
msolwa kwa nini usipumzike tu maana sasa unkoelekea ni kubaya, angalia usije vuliwa nguo.
 
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/7/15/makala7.php



Uozo Bodi ya Mikopo, kilele cha ufisadi Serikali ya Kikwete

M. M. Mwanakijiji


WIKI iliyopita nilielezea kwa kirefu kwanini Watanzania hatuwezi kumuamini Prof. Peter Msolla ambaye ni Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu. Nikafafanua kwa mifano mbalimbali ni jinsi gani waziri huyu wa awamu ya nne ameshindwa kabisa kuongoza wizara hiyo na hivyo kuendelea kutoa matamko mbalimbali ambayo hayatekelezeki na pia yeye mwenyewe kushindwa kabisa kuonyesha mfano wa jinsi yanavyopaswa kutekelezeka. Hatuna sababu ya kumuamini Profesa Msolla hata chembe licha ya mbwembwe zote za maneno matamu ya asali bungeni.
Kama hujashawishika, ni lengo langu leo kuonyesha mfano dhahiri wa jinsi gani Profesa Msolla si tu hastahili kuendelea na wadhifa huo, bali pia ni jinsi gani amewaacha vijana wetu kuteseka huko Ukraine kutokana na uzembe wa Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu iliyo chini yake. Kwa kuendelea kusema kuwa vijana hawa "waliondoka wenyewe" na ya kuwa walikurupuka kupanda ndege "kwa udhamini binafsi" wakati yeye na watu wote walio chini yake wanajua ukweli kuwa vijana hawa waliondoka baada ya kukubaliwa mikopo (si kuomba) na pia kupewa msaada wote na bodi wa kuweza kupata pasi za kusafiria na zaidi ya yote kupata visa za kwenda Ukraine.

Kinachoonyesha ni jinsi gani Prof. Msolla si msema kweli ni kauli ya wizara yake mapema kwenye kikao cha Bunge linaloendelea wiki chache zilizopita kwamba serikali "haikutoa udhamini wa mwaka wa kwanza kwa mwanafunzi yeyote nje ya nchi" wakati ushahidi upo na unaonyesha kwamba serikali hata kama haikutoa, ilitenga kiasi cha fedha kwa wanafunzi wanaosoma huko nje ya nchi. Mfano dhahiri ni kitendo cha serikali kuanza kuwalipia wanafunzi watatu kati ya wale 29 huko Ukraine. Wanafunzi ambao wanalipiwa na serikali na walikuwa kwenye kundi la wale 29 ni Yesse Cornelio Msechu (sh 3,000,000), Rajabu Kihalla na Adiel Daniel Mushi.

Katika hawa watatu, tutamtumia Adiel Daniel Mushi kudhihirisha ni jinsi gani Bodi ya Mikopo iliyo chini ya Prof. Msolla ina ubovu ambao tiba yake ni kuivunja na kuiunda upya baada ya maandalizi ya kitaalam kufanyika na si kukurupuka kama ilivyo sasa. Matatizo yaliyowakuta vijana wetu huko Ukraine ni matokeo ya moja kwa moja ya ubovu wa bodi na uzembe wa maofisa wa wizara na ni kielelezo cha ukosefu wa uongozi toka ngazi za juu za wizara.

Adiel Daniel Mushi alikuwa ni miongoni mwa wale wanafunzi 29 na yeye kama wao, alichelewa kwenda kuanza masomo Ukraine mwaka 2005/2006, na pamoja nao alienda Ukraine kwa malipo yake baada ya kuambiwa mkopo wake utamfuata Ukraine. Pamoja na wenzake wawili tuliowataja hapo juu, Adiel alisubiri kama wale wengine mkopo wake na mwanzoni alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi waliolalamika kucheleweshewa mikopo yao.

Kwa namna ambayo Prof. Msolla na Nyatega pekee wanajua (bila ya shaka kuna maofisa wengine wanajua), Adiel alianza kupokea fedha kutoka bodi na hivyo kuendelea na masomo yake kama kawaida na hivyo kujiengua kutoka katika kundi la wale 29. Wenzake wawili nao wakaanza kupatiwa mikopo.

Wizara inaweza kutafuta kisingizio chochote cha kuelezea ilikuwaje Adiel na wenzake waanze kupokea mikopo wakati wengine 26 waliokuwa katika mazingira yale yale na vyuo vile vile wasipatiwe mikopo yao? Kama hiyo haitoshi, huyo huyo Adiel alitengewa na bodi hiyo hiyo inayomlipia huko Ukraine fedha nyingine kwenye vyuo vya nyumbani kwa mwaka ule ule! Kwenye batch 8 alitengewa sh 1,320,000 kwenda kusomea BSc hapo CoET (mwaka wa kwanza), kama vile hiyo haitoshi, bodi yetu yenye makengeza ikamkubalia sh 1,320,000 nyingine kwenye chuo hicho hicho, lakini hiyo ikitangazwa kwenye Batch 13! Nilisahau kuwaambia huko Ukraine ametengewa sh 3,000,000! Ina maana mtu mmoja alikubaliwa sh 5,640,000!

Sasa bila ya shaka bodi wanaweza kutoa maelezo kuwa hayo ni makosa ya kompyuta, wanaweza kusema haina maana fedha zote zilitolewa kwa mtu mmoja na wanaweza kusema kuwa jina hilo la "Adiel Daniel Mushi" ni la watu watatu tofauti, wawili wakiwa chuo kimoja na wakisomea kitu kile kile! Kama hii ni nasibu, basi inafaa kuingizwa kwenye Guinness Book of World Records!

Ndugu zangu hili si nasibu, bali ni mtindo unaoendelea kwenye bodi hii iliyo chini ya Msolla, kwa watu wachache kujitajirisha kwa kuomba na kutoa mikopo hewa. Uchunguzi wangu wa kina umegundua zaidi ya majina ya wanafunzi 500 ambao wamekubaliwa mikopo ya karibu wastani wa shilingi milioni sita kila mmoja kwenye vyuo zaidi ya kimoja. Jumla ya mikopo ile ya ziada (tukichukulia kuwa mwanafunzi huyo alichagua chuo cha gharama zaidi) inakaribia shilingi bilioni moja! Swali kwa Prof. Msolla na maafisa wake, kama wanafunzi hawa hawakutumia hizo bilioni moja kwenye vyuo vilivyowakubali na wakaamua kwenda chuo kimoja tu, zile fedha zilizotengwa kwa ajili ya vyuo vile vingine zimekwenda wapi? Kama hazikuliwa wanaonaje wakazitumia kuwasomesha vijana wetu huko Ukraine badala ya kukimbilia kuwatumia tiketi ili warudi haraka haraka ili yaishe kinyemela?

Kwa vile watataka ushahidi kuwa tukio la Adiel si la pekee na kuwa kweli wapo watu wengine ambao wamekubaliwa mikopo kwenye vyuo zaidi ya kimoja na fedha, ninawapatia hapa tone la majina hayo mia tano, vinginevyo itabidi ninunue kurasa za magazeti na kuzijaza.

Wa kwanza kati ya wanafunzi hawa ambaye nusura anipe ugonjwa wa moyo ni mwanafunzi aitwaye Charles J. Temba. Huyu si miongoni mwa wale waliokubaliwa kule Ukraine. Ila kesi yake ni kali zaidi kuliko ya Adiel.

Charles J. Temba, mwanafunzi huyu (kama kweli yupo) amekatiwa mikopo mara tatu katika vyuo vitatu tofauti, na vyote ni kwa mwaka wa kwanza! Haiwezekani kuwa bodi haikujua kuwa inamkatia mikopo mtu huyo huyo na kama haikujua basi ni sababu tosha ya kuonyesha kuwa kuna ubovu, na kama walijua, basi ni ushahidi kuwa kuna ubovu zaidi ya tunavyofikiria. Temba kwa mwaka huo wa 2006/2007:

Yuko Batch 11, Tumaini University – sh 1,860,000.00

Yuko Batch 8, Sokoine University – sh 1,794,800.00

Yuko Batch 16, Mzumbe University - sh 1,560,000.00

Yuko Batch 16, MIST – sh 1,500,000 Kwenye Batch hiyo hiyo 16 kuna mwanafunzi mwingine anayetumia jina la "Charles B. Temba", inawezekana kuwa ni mtu yule yule? Huyu yupo University of Arusha mwaka wa kwanza na katengewa sh 1,560,000 – Jumla ya fedha alizotengewa ni sh 8,274,800!
Wanafunzi wengine waliokubaliwa mikopo mwaka huo huo zaidi ya mara moja na kwenye vyuo tofauti (au vile vile) ni:

Denis David Kanyika: Yeye alitengewa fedha za mwaka wa kwanza kwenda kusoma Ukraine 2006/2007 (Batch 12). Hiyo ni kinyume na madai ya waziri kuwa hakukuwa na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyedhaminiwa nje ya nchi. Zaidi ya yote, huyo alikuwepo kwenye batch 8 ya mwaka 2005/2006. Batch hiyo ilikuwa na mwanafunzi aliyekwama, Ramadhani Nyello. Kanyika alitengewa sh 3,000,000


Alistidia J. Rupia ambaye yuko Batch 10, alikubaliwa mkopo mwaka wa kwanza wa shilingi 1,320,000 (UDSM) kwenda kusomea B.A Education na wakati huo huo akakubaliwa mkopo wa sh 4,390,400 (batch 14, batch 16) wa kwenda kusoma Kifaransa Algeria. Yote ni mwaka wa kwanza. Jumla sh 5,710,000


Salim J. Chadoe aliyeko batch 5 (UDSM) ambaye amekubaliwa mkopo wa kusomea Bcom kiasi cha shilingi 1,760,000 na pia alikubaliwa (batch 14) mkopo wa shilingi 3,000,000 kwenda Poland jina la chuo na alichokubaliwa kusomea hakikuwekwa dhahiri. Jumla fedha alizokubaliwa ni sh 4,760,000


Patrick Kazinja ambaye yuko batch 11 (UDSM) ambako alikubaliwa mkopo wa shilingi 1,440,000 kusomea Bcom na wakati huo huo alikubaliwa shilingi 4,390,000 kwenda kusomea Kifaransa mwaka wa kwanza huko Algeria Batch 14, na 16. Jumla alizokubaliwa ni sh 5,830,000


Mary Ligunda ambaye alikubaliwa kwenye batch 4 shilingi 1,320,000 (UDSM) kwenda kusomea Food & Biochemical Engineering. Wakati huo huo na mwaka huo huo na mtu yule yule alikubaliwa shilingi 4,390,000 kwenda kusoma Kifaransa Algeria. Jumla alizokubaliwa ni sh 5,710,000.

Sophia Sokoni ambaye yuko Batch 13 amekubaliwa mkopo wa shilingi 1,440,000 (UCLAS) kusomea BSc in Building Economics na wakati huo huo amekubaliwa sh 4,390,400 kwenda kusoma Algeria Kifaransa. Jumla alizokubaliwa ni sh 5,830,000


Mohammed Matwera ambaye amekubaliwa mkopo (batch 4) wa shilingi 1,700,000 kusomea Udaktari (UDSM) na wakati huo huo akiwa amekubaliwa mkopo wa sh 4,390,000 kwenda kusomea Kifaransa Algeria (Batch 14, na 16). Jumla alikubaliwa sh 6,090,000.

Nyamhanga Msabi Mwita: Huyu ni mwanafunzi katika vyuo viwili ambako sehemu zote ametengewa fedha za chakula, ada, vitabu. Ametengewa sh 1,910,000 huko SAUT (Batch 11) na pia kuna mtu mwingine naye anaitwa Msabi Mwita ambaye alitengewa sh 9,247,045 kwenda kusoma China (Batch 2). Je, huyu ni mtu yule yule au ni watu wawili tofauti? Amekubaliwa zaidi ya sh milioni 11!

Exaud Chengula: Huyu ametengewa fedha kwenye vyuo viwili tofauti mwaka ule ule na vyote kwa mwaka wa kwanza. Ametengewa sh 1,320,000 kusomea Elimu (DUCE – Dar es Salaam University College of Education) na pia ametengewa sh 1,860,000 huko Tumaini University kusomea BA-CAT (Cultural Anthropology and Tourism).

Emmanuel Richard Kizigha: Huyu alitengewa sh 1,707,000 kusomea pale CBE kwa mwaka 2006/2007 (Batch 7). Wakati huo huo hata hivyo alitengewa sh 3,000,000 kwa mwaka wa pili kusoma huko Ukraine (Batch 8). Huyo naye alikuwa kwenye batch 8 ya mwaka 2005/2006 ambayo kijana Ramadhani Nyello alikuwamo naye. Kama Bodi inajua huyu yuko mwaka wa pili huko Ukraine, kwanini wamtengee tena fedha hapo CBE?
Hayo ni majina machache tu ya wanafunzi ambao Prof. Msolla na watu wa bodi wameona ni vyema wawatengee mamilioni ya fedha kwenye vyuo mbalimbali, lakini wakati huo huo kuwanyima kabisa wanafunzi wetu 24 (samahani nilisahau kuwaambia kuwa wanafunzi wawili wengine waliondoka Ukraine baada ya kushindwa kuendelea na masomo na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha. Kisingizio pekee ambacho Prof. Msolla na wenzake wanakitumia ni kuwa "waliondoka wenyewe na kwa udhamini binafsi". Wimbo huu wameendelea kuuimba kiasi cha kwamba wao wenyewe wamekuwa wa kwanza kuuamini!).

Kwenye suala la wanafunzi hawa waliotengewa mikopo zaidi ya mara moja, kuna maelezo kadhaa yanayoweza kutolewa, kwanza ni kuwa kukubaliwa mkopo haina maana kupata mkopo; kwa hili tunasema kama umekubaliwa mkopo na fedha zako zikatengwa, ni tofauti gani na mtu kupewa mkopo ambao bado hujauchukua? Kama wanafunzi walikubaliwa, je, serikali inasema hawakuchukua mikopo hiyo baada ya kujua wamekubaliwa? Kama wanafunzi hawa walichagua chuo kimoja kati ya vingi walivyokubaliwa, zile fedha walizokubaliwa vile vyuo ambavyo hawakwenda zimeenda wapi?

Inawezekana wakasema kuwa bodi ya mikopo imefanya makosa kidogo na yatasahihishwa. Makosa ya kutenga karibu bilioni moja kwa wanafunzi hewa, si makosa kidogo! Ni makosa ambayo kwenye nchi zenye kuheshimu sheria yanatosha kabisa kufukuzisha watu kazi. Tunachosema ni kuwa, fedha hizo zilizotengwa aidha zimeishia mikononi mwa watu wachache au bado zipo. Kama zimeishia mikononi mwa watu wachache watu hao ni lazima wajulikane, kama bado zipo kwanini zisitumike kuwalipia wanafunzi wetu wa udaktari, na uhandishi waliokwama Ukraine?

Na mwisho wanaweza kusema kuwa madai ninayoyatoa hapa hayana msingi. Na sitashangaa serikali yetu tukufu ikaanza kutafuta ni nani aliyeandika jambo hili na kuliweka hadharani badala ya kufanyia kazi madai yangu.

Kama suala la BoT ni mfano, sitashangaa serikali kukataa kufanya uchunguzi wowote. Lakini kwa vile suala hili ni kubwa na tulichoonyesha ni kiduchu, basi itakuwa ni kosa kubwa kulifumbia macho kwani itawahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Rais Kikwete haina ubavu wa kupambana na ufisadi na maneno ya ‘Tanzania yenye neema kwa kila Mtanzania' ni maneno matupu kwani hawa wanafunzi wetu 24 hawaoni neema yoyote na hiyo Tanzania kwao ni njozi ya nchi ya kusadikika.

Ni matumaini yangu kwa kuyaweka haya hadharani tumewapa zana wawakilishi wetu bungeni mahali pa kuanzia kumbana Prof. Msolla. Wabunge wetu wamechaguliwa kuwakilisha wananchi. Miongoni mwa wananchi hao ni hawa vijana 24. Itakuwa ni unafiki wa daraja la kwanza kwa wabunge kujifanya wanawatetea Watanzania mamilioni wakati hawa 24 wameshindwa kuwatetea. Itakuwa ni aibu ya taifa letu kuendelea kuwakana vijana wetu "on technicalities". Vijana hawa hawaombi kitu chochote kutoka kwa nchi yao isipokuwa nafasi ya kuendelea na masomo. Hadi hivi sasa vyuo vimewaonea huruma na sasa vyuo hivi vinafungwa na hatima ya watoto wetu haijulikani. Wakati umefika Watanzania tuonyeshe kuguswa na suala lao na kuwatetea. Tusisubiri hadi tusikie wamekufa ndipo tujifanye tunatuma rambirambi na kuonyesha kusikitishwa! Tusisubiri hadi janga litokee ndipo tujifanye tunawatetea!

Mimi nimefanya nafasi yangu, wananchi wengine wamefanya nafasi yao, TANLET wamefanya jukumu lao, viongozi wa upinzani wamefanya nafasi yao, wazazi wamefanya nafasi yao katika kuwasaidia vijana hawa. Watu pekee ambao tunatarajia kuwa watafanya nafasi yao ni viongozi wa CCM na wabunge wake. Wapinzani kwa sasa hawana nguvu ya kulazimisha kufanyika kitu kwani kama CCM haitaki, hakipatikani. Ila viongozi wa CCM wakiongozwa na yule "kiongozi mahiri, shujaa na hodari", basi wana uwezo wa kulimaliza jambo hili. Kwani hawa wakiamua vijana waendelee kusoma wataendelea, ni hawa wakiamua vijana wapatiwe fedha zao za mikopo ya kuendelea na masomo na kulipia deni lao lililoko sasa hivi vyuoni itafanyika.

Tumaini la vijana hawa na wazazi wao ni kuwa serikali ya Kikwete itasita angalau kwa sekunde na kusema itakuwaje kuwa tumewaacha vijana hawa sababu ya uzembe wa watu wachache? Natoa wito kwa wananchi tusimame upande wa watoto hawa ili waendelee kusoma. Tusiwaangushe hadi wakakata matumaini na nchi yao.

Watoto hawa wangetaka kuikana nchi yao wangefanya hivyo, kama wangetaka kuzamia ugenini wangefanya hivyo, lakini hadi hivi sasa kwa machozi na kwa kutetemeka, wanaiomba nchi yao itimize ahadi yake kwao, na isiwalipizie kisasi kwa makosa ya watu wachache.

Wamekinga mikono kama wanaomba wakisema "tusomesheni". Wanalia kila siku wakijiuliza "tumeikosea nini Tanzania?" Wanajiambia kila kukicha, "laiti ningekuwa na uwezo nisingehangaika hivi". Ndugu zangu, tukiendelea kuwafumbia macho vijana hawa, ina maana kweli Tanzania tumeingiwa na kiza kipya cha ufisadi!

Tusikubali kuwaacha, tusikubali warudi bila kuendelea na masomo, na tuhakikishe kuwa ahadi ya ‘Tanzania yenye neema kwa kila Mtanzania' ianze kuwafikia hawa kwani kama ni adhabu wameshapata vya kutosha! Je, Tanzania itasimama upande wao au wakubali yaishe na wachukue tiketi warudi nyumbani na kujipanga mstari kuanza moja na hivyo kuwapa furaha kina Msolla kuwa wamewashinda vijana hawa? Ikitokea hivyo, basi walioshindwa ni sisi wananchi wote kwa kuwaacha watawala wetu kuwatenda vibaya vijana hawa huku tukijifanya kuwa hilo ni jimbo dogo. Siku moja itakuwa kwa mtoto wa mwingine. Mmeonywa.
 
kuna mtu Ukraine mwenye jina hilo na alitengewa fedha kusoma huko mwaka jana Angalia Hapa Search kwa Ctr+F na andika jina lake. Je inawezekana kuna watu wawili waliokubaliwa mikopo hiyo? Waweke hadharani majina ya waliogawiwa mikopo mwaka jana Ukraine na jina la Adiel limo.
 
Naona serikali wameshamjibu tena mkjj kuhusu ile article yake kuhusu ndege inayopaa. Wamelipia kurasa kadhaa katika magazeti. Naona wameamua ku-invest kwenye kujisafisha kwa kila criticism wanayopewa. Problem ni kuwa hawana kabisa vichwa vilivyotulia; kila statement wakitoa inapwaya mno inakuwa kama imeandikwa na mwanafunzi mwerevu wa drs la saba!
 
kuna mtu Ukraine mwenye jina hilo na alitengewa fedha kusoma huko mwaka jana Angalia Hapa Search kwa Ctr+F na andika jina lake. Je inawezekana kuna watu wawili waliokubaliwa mikopo hiyo? Waweke hadharani majina ya waliogawiwa mikopo mwaka jana Ukraine na jina la Adiel limo.


Nashukuru kwa link. Sasa ngoja nasubiri majibu yako kwa bodi, halafu nitaendelea maana hii issue ni tata kwa kila upande.
 
Naona serikali wameshamjibu tena mkjj kuhusu ile article yake kuhusu ndege inayopaa. Wamelipia kurasa kadhaa katika magazeti. Naona wameamua ku-invest kwenye kujisafisha kwa kila criticism wanayopewa. Problem ni kuwa hawana kabisa vichwa vilivyotulia; kila statement wakitoa inapwaya mno inakuwa kama imeandikwa na mwanafunzi mwerevu wa drs la saba!


Ni vizuri kama watakuwa wanafanya hivyo kwa kila uozo unaoanikwa. Hii ina faida mbili: moja ni kutoa usahihi wa jambo kama allegations ni uzushi, na pili ni kuwafungua zaidi wale ambao hawakupata kuona hizo allegations na hivyo kupata nafasi ya pili ya kutafuta ni nini kilichomo. Na hapo ndipo unaweza kuanza kuona nani yuko sahihi kwa asilimia kadhaa!!
 
Back
Top Bottom