Katika medani ya siasa sio kila kitu kiko wazi kwa mwananchi wa kawaida, hivyo ni kazi ya wakulu na wachambuzi kutufungua macho. Hili suala la Azimio la Msasani ni suala tete na nyeti sana ambalo inabidi tuliangalie kwa undani kama tunataka kuelewa hali halisi ya chama tawala. Ndio suala pekee lililomliza Mwalimu mbele ya kadamnasi. Ngoja nimnukuu Mwalimu mwenyewe kutoka katika ukurasa wa 20 wa kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania:
"Sina kawaida ya kulizwa na mambo ya siasa, lakini katika kikao hicho nilishindwa kujizuia kulia. Sikupata maelezo ya maana ya kuwafanya watu wazima wafanye walivyofanya. Nilipouliza kwa nini hawakupinga hoja ya Serikali Tatu, kama tulivyokuwa tumekubaliana, majibu ya Viongozi wetu Wakuu yalikuwa ni ya ajabu kabisa. Ati Wabunge wenye hoja, baada ya kuonana nami Msasani, walikwenda bungeni wakiwa wakali kama mbogo"
Sasa hapa inabidi tujiulize waliteta nini Msasani kilichowapa ujasiri wa ajabu wabunge hawa wa G55 wageuke nyati bungeni? Iweje Mwalimu ambaye alikuwa anapingana kabisa na hoja yao ya Utanganyika awaite chemba pale Msasani na awape ujasiri huu wa ajabu katika enzi za zidumu fikra sahihi za mwenyeketi wa zamani wa chama na zama za chama kuendelea tu kushika hatamu hata wakati wa mageuzi? Na iweje baada ya tukio hilo Mwalimu asisitize sana katika kitabu chake cha Tanzania!Tanzania! kuwa sera ya Utanganyika sio sera ya chama tawala na kuwa wanaounga mkono sera hiyo watoke waanzishe chama chao? Kama muasisi mwenyewe wa chama tawala alisema upinzani wa kweli utatoka CCM nini kinawazuia G55 wa leo wenye hoja za msingi dhidi ya Richmond, Kiwira na EPA wasijitoe katika mitandao ya chama tawala na kuanzisha chama kitakacholeta upinzani wa kweli?