Shusheni nondo jamani, historia yetu ingekuwaje leo bila tukio hili?
Baliba...
Nimeandika kitabu kuhusu Azimio la Tabora.
Sakata zima la historia hiyo nilielezwa na marehemu
Sheikh Rashid Sembe:
UCHAGUZI WA KWANZA TANGANYIKA ''UCHAGUZI WA KURA TATU'' 1958 KUTOKA KUMBUKUMBU ZAKE SHEIKH RASHID SEMBE (1912 - 1999)
MWAKA 1958 serikali ya kikoloni baada ya kushindwa ilikubali ufanyike uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya rangi. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari, 1958 kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya haya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa au isusie uchaguzi.
Mkutano huu wa Tabora ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama
Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu,
Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama mapande mawili kama isingelikuwa busara ya
Mwalimu Nyerere, Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri na viongozi wa TANU wa Tanga ambao walipanga mkakati wa kuwashinda 'siasa kali' katika chama.
Lakini ili kuzielewa hisia za wanachama wa TANU, uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini Kura Tatu ilizua mgogoro na kutoelewana katika uongozi, inatubidi turudi nyuma. Tunahitaji kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo
Mwalimu Nyerere na uongozi wa TANU Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika mkakati wa
Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Mwalimu Kihere na
Mwalimu Nyerere uliofanya wafuasi wa siasa za wastani wawashinde wale waliokuwa na msimamo mkali. Inasikitisha kuwa kisa hiki cha ujasiri na mbinu za hali ya juu kama zilivyoonyeshwa na watu wa Tanga hadi leo kimebaki siri kuu. Wanaokifahamu kisa hiki wengi wao wameshakufa.
Baraza la Wazee wa TANU
TANU kwa hakika kilikuwa chama cha Waislamu; kwa hiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa kuyakubali masharti yale ya kibaguzi ya upigaji kura ilikuwa sawa sawa na kuwasukuma Waislamu ambao ndiyo walikuwa wafuasi wakubwa wa TANU nje ya wigo wa siasa. Ujumbe wa
Mwalimu Nyerere mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na wajumbe wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao Makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na
Mwalimu Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Azizi, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na
Rajabu Diwani.
Iddi Tosiri
Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislamu kule Dar e Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Baraza la Wazee wa TANU likiwa na wajumbe takriban mia mbili na sabini Waislamu watupu, walikuwa hawawezi kupiga wala kupigiwa kura. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi.
Kushoto Iddi Faiz Mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere, Saadan
Abdu Kandoro na Haruna Taratibu
Serikali ya kikoloni, ikishirikiana na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislamu elimu, sharti lile lile ambalo sasa linawekwa kuwazuia Waislamu kushiriki katika siasa. Hakuna kumbukumbu zozote zinazoeleza mawazo ya
Mwalimu Nyerere katika suala la Kura Tatu wala hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa faragha pale Makao Makuu na washirika wake wa karibu kama
Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwinyimvua, Dossa Azizi au
Bibi Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani Mwalimu Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika Kura Tatu katika masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu kuona kwa nini
Mwalimu Nyerereilibidi afiche msimamo wake katika suala la Kura Tatu kama TANU ilivyotwishwa na serikali.
Mwalimu Nyererealikuwa anafahamu hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na Kura Tatu. Alijua wazi ili kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi haraka na kwa makini kabla ya kwenda kwenye mkutano Tabora.
Siku chache kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU,
Mwalimu Nyerere na
Amos Kisenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga, kuhusu matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa Kura Tatu. Mkutano huu baina ya
Mwalimu Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na
Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng'anzi Mohamed, Mustafa Shauri na
Abdallah Makatta.
Mwalimu Nyerere alizungumza waziwazi na kwa dhati ya moyo alikiambia kikao kile kuwa amekwenda Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa Kura Tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje.
Mwalimu Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wa kuzungumza vizuri.
Mwalimu Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora.
Mwalimu Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima ishiriki katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na seriakli katika siku zijazo.
Kufichuka kwa msimamo wa
Mwalimu Nyerere wa kutaka TANU iingie katika Kura Tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa
Mwalimu Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu
Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wote wawili
Hamisi Heri na
Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa
Mwalimu Nyerere na uchaguzi wa Kura Tatu.
Mwalimu Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya Kura Tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP iliyokuwa na nguvu Tanga kwa sababu ya walowezi waliokuwa wakimiliki mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii akina
Rashid Sembe walikuwa wameelemewa na mashambulizi kutoka kwa wapinzani.
Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lillilokuwa na nguvu sana likiongozwa na
Mmaka Omar kama mwenyekiti na
Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Hawa wote ni marehemu na mchango wao hadi leo haujathaminiwa.
Mwalimu Nyerere na
Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani ili ifanyike
tawaswil. Waliohudhuria kisomo hicho walikuwa
Abdallah Rashid Sembe,
Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu,
Akida Boramimimi bin Dai na
Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Qur'an Tukufu alikuwa mjomba wa
Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora.
Marehemu Abdallah Rashid Sembe na Mjadala wa Kura Tatu
Mara baada ya dua ile
Mwalimu Nyerere aliondoka kwenda Tabora akiongoza ujumbe mkubwa sana kutoka makao makuu. Ile agenda ya uchaguzi wa Kura Tatu ilipoanza kujadiliwa, mkakati wa Tanga uliofanyiwa dua maalum kwa Mwenyezi Mungu katika kijiji cha Mnyanjani ukaanza kutekelezwa.
Mwalimu Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano aliomba amwachie kiti
Mwalimu Kihere ili apate fursa ya kushiriki katika mjadala na kutoa mchango wake. Mara tu baada ya
Mwalimu Kihere kuchukua kiti aliutuliza mkutano na akamchagua
Sheikh Abdallah Rashid Sembe kuwa msemaji wa kwanza kama vile walivyopanga kule Tanga majuma machache yaliyopita.
Sembe alihimiza TANU kushiriki katika uchaguzi. Kama vile
Baba wa Taifa alivyotabiri mapema, zogo kubwa lilizuka. Wajumbe walipiga makelele, wakagonga meza kwa hasira, wengine wakawa wanaburuza meza na viti kwa makelele kudhihirisha hamaki zao.
Jumanne Abdallah, Bhoke Munanka kutoka Jimbo la Ziwa walisimama na kumlaani
Abdallah Rashid Sembe wakimwita msaliti.
Sheikh Sembe alishikilia msimamo wake kuwa TANU ni lazima iingie uchaguzi unaokuja ili ishinde uchaguzi na katika ushindi huo iwe na uwezo wa kufutilia mbali mfumo huo wa dhulma.
Mwalimu Nyerere alisimama na akamuunga mkono
Sheikh Sembe. Mwalimu
Nyerere alitoa hoja katika misingi hiyo hiyo kuwa ili TANU iweze kuondoa Kura Tatu ni lazima kwanza iingie kwenye Kura Tatu. Wajumbe hawakuafiki hoja ya
Mwalimu Nyerere. Wote walishikilia msimamo wa TANU kususia uchaguzi. Hamaki za watu zilikuwa wazi ndani ya ukumbi wa mkutano wa
Mwalimu Kiherealiahirisha kikao hadi siku ya pili ili kuwapa wajumbe muda wa kutuliza hamaki zao.
Siku iliyofuata ustadi wa
Mwalimu Nyerere katika mjadala ulitumika.
Mwalimu Nyerere akizungumza kwa vitendawili na methali, aliwauliza wasikilizaji wake, je, ingewezekana kwa mkulima mwenye busara, aliyelima na kupanda shamba lake kwa taabu, angesita kuvuna mazao yake kwa kuhofia kuchafua nguo zake, kwa sababu tu, ili afike shambani kwake itabidi avuke mto wenye matope. Watu wangelimuonaje mkulima kama huyo?
Mwalimu Nyerere aliwaeleza wale wajumbe kuwa, TANU iko njia panda, ingekuwa kazi bure kwa wakati huu kwa TANU kususia uchaguzi baada ya kufanya kazi yote ile kwa shida kubwa hadi kufika hapo walipofika. Kususia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza katika mtego. Adui angefurahi kuona imenasa katika mtego, TANU ikisimama pembeni na UTP ikiingia katika uchaguzi na kuchukua viti vyote katika Baraza la Kutunga Sheria. Serikali ya kikoloni ingefurahi sana kuona kitu hiki kinatokea.
Mwalimu Nyerere na
Sheikh Abdallah Rashid Sembe ambaye alihatarisha uhai wa yeye kuwapo katika TANU katika suala la uchaguzi wa Kura Tatu walikuwa washindi. Hata hivyo agenda ya Kura Tatu ilibidi ipigiwe kura. Kura ilipopigwa kundi la akina
Sheikh Suleiman Takadiri waliotaka kuususia uchaguzi walishindwa: kura 37 zilipigwa kuunga mkono kushiriki uchaguzi wa Kura Tatu dhidi ya 23 zilizotaka ususiaji.
Mwalimu Nyerere alitia sahihi Azimio la Tabora ambalo baadae lilikuja kujulikana kama 'Uamuzi wa Busara.'
Siku ile
Mwalimu Nyerere alipokuwa akiweka sahihi yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa
Mwalimu Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU,
John Rupia; upande wake wa kushoto alikuwepo
Amos Kissenge, aliyekuwa kakaa nyuma ya
Mwalimu Nyerere akiwa amevaa kofia ya mkono, koti na kanzu alikuwa
Mzee Jumbe Tambaza mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU, upande wake wa kulia alikuwa kijana
Juma Selemani maarufu kwa jina la lake la utani,
'Juma Mlevi', katibu wa Bantu Group. Mwisho wa meza wakitazamana alikuwa
Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia wa
Mwalimu Nyerere na
Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.
Mohamed Jumbe Tambaza
Baada ya kutia saini kwa Azimio la Tabora
Mwalimu Nyerere alimpigia simu
Zuberi Mtemvu makao makuu Dar es Salaam kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU imepiga kura kuingia katika uchaguzi wa Kura Tatu. Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea
Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa rais wa TANU,
Mwalimu Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake cha upinzani - African National Congress (ANC) Chama cha Mtemvu kilikuja kujulikana kama 'Congress' neno ambalo kwa mtazamo wa vyama hivyo pinzani lilikuja kunasibishwa na usaliti.
Mtemvuakimshutumu
Mwalimu Nyerere kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na wananchi kwa kuwatumbukiza katika Kura Tatu; na
Mwalimu Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kujitenga na mapambano na kujiunga na upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai uhuru. Hadi leo
Mzee Mtemvu na wazee wengi wa TANU hawafahamu kuwa mkakati wa Tabora ulipikwa Mnyanjani.
Kulia Zuberi Mtemvu, Julius Nyerere na John Rupia waliosimama nyuma ni vijana wa Bantu Group wahamasishaji na walinzi wa TANU. Nyuma waliosimama wa pili ni Ali Msham ambao picha hii nimeipata kwa hisani ya mwanae Abdulrahman Ali Msham.
Soma historia ya Ali Msham na Zuberi Mtemvu hapo chini:
Mohamed Said: PICHA ADIMU ZA TANU, JULIUS NYERERE NA WAZALENDO WALIOSAHAULIKA KATIKA HISTORIA YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA 1954 - 1961
Mohamed Said: ZUBERI MWINSHEHE MANGA MTEMVU MZALENDO ALIYEKUWA NA MSIMAMO MKALI WA “AFRIKA KWA WAAFRIKA”
Kabla ya kuondoka Tabora
Mwalimu Nyerere lifanya mkutano wa hadhara soko kuu la Tabora na kuelezea maamuzi ya mkutano mkuu. Hotuba ya Mwalimu Nyerere ilijaa hisia kali. Aliwaambia wasikilizaji wake kuwa endapo Waingereza watakaidi kutoa uhuru basi wananchi wataelekeza kilio chao kwa Mwenyezi Mungu. Wakati ule TANU ilikuwa na dini hakukuwa na lugha ya sasa ya 'chama chetu hakina dini'.
Mwalimu Nyererealipotamka maneno haya hakuweza kujizuia, akaangua kilio na vilio vya wananchi waliouelewa uchungu wa dhulma vikatanda uwanja mzima. Baada ya hotuba hii iliyowaliza watu, wananchi wengi ambao walisita kujiunga na TANU sasa waliingia kwa wingi. Ni vigumu kuamini lakini watu huko Tabora walisimama msururu usikukucha kukata kadi za TANU.
Huyu ndiye
Sheikh Abdallah Rashid Sembe, muasisi wa TANU ambae amekufa akiwa mwanachama mtiifu wa CCM na kwa viongozi wake. Mkutano wake wa mwisho aliohudhuria wa CCM ulikuwa Mkutano Mkuu uliofanyika Dodoma Novemba, 1997 ambao alihudhuria kama mwalikwa. Kwa bahati mbaya sana mkutano huu ulimalizika kwa fedheha kwa upande wa
Sheikh Rashid Sembe. Bila ya kujali umri wa
Sheikh Sembe na nafasi yake ya usheikh, msichana mcheza ngoma akiwa nusu uchi alikwenda kucheza ngoma mbele yake na huku akinengua alimkalia
Sheikh Sembe mapajani. Gazeti moja la kila siku bila ya tafakuri ikachapisha picha ile ya
Sheikh Sembe akiwa katika mavazi yake ya Kiislamu ya kanzu, koti, kofia na kilemba katika ukurasa wake wa mbele. Waislamu wengi walikasirishwa na kuhuzunishwa na picha ile. Wapo waliomlaumu
Sheikh Sembe kwa kuhudhuria mikutano ya
kitwaghut na wapo walioilaumu CCM kwa kuachia
Sheikh Abdallah Rashid Sembeavunjiwe heshima na halikadhalika wapo waliolilaumu gazeti.
Wengi wa wanasiasa wa sasa katika ukumbi ule wa mkutano walikuwa wakimpita
Sheikh Sembe bila ya kujua kwa hakika yule mzee aliyevaa Kiislamu katika ukumbi ule alikuwa nani na nini ulikuwa mchango wake katika siasa za Tanganyika. Hata hivyo historia ya uhuru wa Tanganyika na hata maisha ya
Mwalimu Nyerere yatakapoandikwa hayatakamilika bila ya kumtaja
Sheikh Abdallah Rashid Sembe.