Sote tunauona uhuni huu, ila ukimya umekuwa ndiyo chaguo la wengi. Hata wanachama wenyewe wa Chadema wako kimya. Ukimya mzito, kama pazia jeusi lililoshushwa katikati ya jukwaa lenye kelele.
Hayupo anayeongea. Hakuna hata anayethubutu kunong’ona. Ni kama vile walikubaliana kimyakimya kuwa hakuna lolote la kusema. Mtu mmoja,
Pascal Mayalla akiwa nje ya Chadema, anaweza kufanya nini?
Unajua kimya cha huko Chadema kimetokana na nini? Umasikini. Adui wa kwanza wa Tanzania ni umasikini.
Umasikini huu si wa kawaida. Ni mwizi wa matumaini, mkandamizaji wa ndoto, na silaha mikononi mwa wenye nacho.
Wenye nazo hawahitaji silaha nyingine – wanatumia umasikini wa watoto wa masikini kuwajenga wao wenyewe. Wanatoa ahadi nzuri kwa masikini, ahadi ambazo hazitafika popote. Wanajenga ngome zao juu ya jasho na machozi ya wasio nacho.
Wanaomuunga mkono Tundu Lissu wanaongea kwa sauti ya kimya. Ukimya wao unazua maswali zaidi ya majibu. Ni hofu? Ni unyonge? Au ni hesabu za kisiasa za watu waliokwama njia panda?
Lakini, kwenye upande mwingine, wanaomuunga mkono Mbowe hawana muda wa ukimya. Wanakesha wakihubiri sifa zake, wakitengeneza headline za magazeti na mitandao ya habari. Mikocheni imegeuka kiwanda cha propaganda. Na hapa ndipo mchezo wa wenye nguvu unafikia kilele chake.
Unajiuliza, hii ni demokrasia au mapambano ya kiitikadi yaliyojaa hila? Labda suluhisho ni moja tu, kuongeza matajiri kwenye siasa.
Wenye nazo wakishindana wao kwa wao, labda masikini wataachwa wapumue. Lakini kwa sasa, matumaini ya wanyonge yamekwama kwenye mifumo inayowalalia.
Swali linabaki, Tanzania itaamka lini? Tutapambana lini na adui huyu ambaye kila siku anazidi kutufanya watumwa wa wenye nguvu? Labda ni ndoto tu – ndoto inayongoja shujaa wa kuifanikisha.
Swali ni; shujaa huyo ni nani? Na atafika lini?
Ova