Tarehe 14 ya Mwezi Julai mwaka huu wa 2026, Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) inatimiza miaka 50 tangu kuanza rasmi kufanya shughuli zake za kibiashara mwaka 1976. Wahenga wanasema kila kwenye mafanikio yoyote yale basi nyuma yake kuna mtu anayeyaunga mkono. Mwaka 1947, liliibuka wazo la kuiunganisha Afrika Mashariki na Kati kupitia reli. Wazo ambalo lilikataliwa na walowezi katika kipindi cha ukoloni wakidai kwamba eti “mradi huu haukuwa na tija kiuchumi”.
Hata hivyo wazo la kuiunganisha Dar es Salaam na Kapiri Mposhi kupitia reli yenye urefu wa zaidi ya kilomita 1860 halikufa kamwe, kwani China kupitia Mwenyekiti Mao Zedong ilisema watafadhili, watasanifu na kuijenga TAZARA, na kuweka bayana kwamba itakapomalizika wataikabidhi kwa nchi husika.
Ikumbukwe kwamba wakati huo China pia haikuwa na hali nzuri ya kiuchumi. Na ndio maana wakati Mwalimu Nyerere alipotembelea China mwaka 1965, alipata wakati mgumu kuomba msaada wa ujenzi wa TAZARA. Mwenyekiti Mao alipokutana na Nyerere, alisema China ina hali ngumu, lakini Tanzania na Zambia zina hali ngumu zaidi ya uchumi. Ni heri China isijenge reli yake lakini itoe msaada kwa Tanzania, kwasababu wao ni marafiki, na China inataka kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ni kweli China ilisaidia wakati msaada ulipokuwa unahitajika zaidi. Kufikia Oktoba 22, 1975 reli ilikamilika kujengwa na kuzinduliwa kwa majaribio, na Julai 14, 1976 reli ya TAZARA ilianza kufanya kazi rasmi.
Baada ya miaka mingi ya uendeshaji reli hii ilikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya uchakavu. Licha ya changamoto hizo TAZARA imeendelea kufanya kazi ikileta ukumbusho wa kimyakimya wa enzi ambazo siasa za kijiografia zilipanda mbegu ya reli ya Afrika, na kuonesha kwamba hadithi hii bado haijafika mwisho.
Ilipofika Septemba 29, 2025 China, Tanzania na Zambia zilifikia tena makubaliano ya kufufua urithi wa Mwenyekiti Mao, Mwalimu Nyerere na Rais Kaunda na kufanya sauti za mataluma ziweze kusikika tena chini ya anga ya Afrika Mashariki. Baada ya kuhuishwa reli hii inaaminika kwamba itasaidia kuongeza mzunguko mkubwa wa biashara na bidhaa utakao kua kwa kasi.
Tanzania kwa upande wake ina matarajio makubwa juu ya mpango huu wa kuhuisha TAZARA na umuhimu wake kwa eneo lote la SADC. Na hii ni kutokana na kwamba njia hii ni moja kati ya njia ambazo zinapita kwenye maeneo makubwa ya kiuchumi ambayo kwa nchi nyingi ikiwemo Tanzania, italeta matokeo makubwa, hasa katika maeneo yenye rasilimali kubwa za madini, rasilimali kubwa za mazao ya kilimo, na pia itaunganisha bandari ya Dar es salaam ambayo imekuwa lango kubwa la nchi nyingi za SADC, ambalo ni muhimu na la kimkakati kwa uchumi kwa nchi hizo.
Kwa upande wa Zambia uhuishaji wa reli ya TAZARA utaongeza biashara yake pia na kuleta uwekezaji zaidi kwenye shughuli nyingine zikiwemo bandari kavu na vituo vya usambazaji. Itakapomalizika, TAZARA inatarajiwa kuleta urahisi wa usafiri kwa watu, bidhaa za kilimo na bidhaa za kawaida, na kutokana na hilo wakulima watakuwa na uwezo pia wa kuongeza mavuno yao. Na hatimaye serikali itaweza kupunguza umasikini kwa kiasi fulani.
Katika kipindi cha miaka 50 ya huduma yake, Reli ya TAZARA imesafirisha abiria zaidi ya milioni 40. Hivyo mradi huu wa uhuishaji wa reli hii iliyotengewa bajeti ya takriban dola bilioni 1.4 za Marekani, utakapamalizika lengo lake kuu litakuwa ni kurejesha ufanisi wake wa usafiri na kuboresha muunganiko wa kikanda. Na pia baada ya kukamilika, uwezo wa usafirishaji mizigo utaongezeka kutoka takriban tani 200,000 za sasa kwa mwaka hadi tani milioni 2.4, na muda wa usafiri pia utapungua kwa theluthi mbili.
Wakati huo huo, Tanzania na Zambia pia zimepanga "ukanda wa reli wa ustawi wa kiuchumi," ili kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda ambao reli hiyo inapita. Hapa tunazungumzia kuhusu bandari kavu, vituo vya usambazaji, jamii za wakulima kuweza kupata pembejeo na kuweka bidhaa zao, wafanyabiashara ya kuvuka mpaka nao watanufaika na reli hii, pia itaweka mzunguko wa kaskazini wa utalii na shughuli nyingine za kiuchumi kama vile maendeleo ya kilimo.
Kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China CRCC, Dai Hegen kwamba kampuni yao itatekeleza kithabiti makubaliano yaliyofikiwa na wakuu wa China, Tanzania na Zambia. Wataenzi moyo wa Reli ya TAZARA, kuendeleza urafiki wa jadi kati ya China na Afrika, na kuufanya mradi huo wa uhuishaji wa Reli ya TAZARA uwe njia ya maendeleo na ustawi kwa wananchi wa Tanzania na Zambia katika zama mpya.