A
Anonymous
Guest
Mimi ni mdau wa JamiiForums, Mkazi wa Mbezi Msakuzi, Mtaa wa Makamba, jirani na Shule ya Msingi Makamba.
Mtaani kwetu tumepitiwa na mradi mpya wa maji kutoka DAWASA, pamoja na kwamba baadhi ya Wakazi wamepata huduma hiyo, bado eneo letu halijafikiwa, licha ya kuwa na nyumba nyingi zinazostahili huduma hiyo.
Hali Ilivyoanza
Kuna jirani yetu mmoja alitufuata majirani wote na kutuambia kuwa mhandisi wa mradi anataka kupewa kiasi cha Tsh 2,000,000 ili aweze kutuletea huduma ya maji haraka. Bila hivyo, alisema tusitegemee kupata huduma hiyo kwa wakati wa karibu. Alitutaka kila mmoja achangie Tsh 300,000 ili tumpe huyo mhandisi.Baadhi ya watu walikubali, lakini wengine wetu tulikataa. Mhandisi alipita na kuonyesha wapi bomba lingepita. Bomba likaletwa na mtaro ukaanza kuchimbwa.
Huyu bwana aliyekuwa mratibu alituuliza tena kama tuko tayari kutoa hela au bado tumesimama kwenye msimamo wetu wa awali. Tulipokataa kwa mara ya pili, wachimbaji waliambiwa waache kazi na wakahamishiwa upande wa pili wa mtaa – hasa nyuma ya nyumba ya yule aliyetuambia tutoe hela za "kushughulikia."
Tulipojaribu kumtafuta mhandisi na kumuuliza sababu ya kusimamisha uchimbaji na kuhamisha ramani ya bomba, alikasirika na kudai kwamba upande huu una watu wachache. Hii ni kinyume na ukweli, kwani bomba hilo lingefikia familia nyingi zaidi kuliko liliko sasa.
Hali ya Sasa
Mpaka sasa, kaya zaidi ya tano kwa upande wetu hazijapata huduma ya maji. Inasikitisha kuona kuwa hata mtaro wa maji ulikuwa umeanza kuchimbwa, lakini ukaachwa kwa sababu tulikataa kutoa rushwa.Kwa ujumla, mazingira ya ugawaji wa huduma ya maji Msakuzi yamejaa rushwa na upendeleo. Kuna maeneo yenye kaya mbili tu ambazo ziko mbali zenyewe kwa zenyewe lakini zimepata maji, ilhali sisi tulio wengi na tunaoishi karibu hatujapata huduma hiyo.
Hitimisho
Tunaomba mamlaka husika ziingilie kati suala hili kwa haraka ili Watanzania wote wanufaike kwa kupata huduma ya maji kwa haki na bila kulazimika kutoa rushwa.Asante.
Majibu ya DAWESA ~ DAWASA yawajibu Wakazi wa Mbezi Msakuzi kuwa "Hakuna Mtumishi anayeruhusiwa kupokea fedha cash kutoka kwa Mteja"