Baadhi ya wanawake hula kondo mara baada ya kujifungua

Baadhi ya wanawake hula kondo mara baada ya kujifungua

vipodozi.jpg

Vipodozi vilivyotengenezwa kwa kutumia kondo la nyuma

Ni kama sahani ya kwanza ya mlo kwa mtu yeyote kabla hajazaliwa. Ni eneo la kwanza lenye manufaa kwa viumbe wengi wakiwa bado hawajauona ulimwengu.
Kwa binadamu, sahani hii ni ya muda usiozidi miezi tisa na baada ya hapo kazi yake huwa imekwisha, hivyo kuondolewa.


Hili ni kondo la nyuma, kwa lugha ya Kiingereza huitwa placenta. Huwa ni sehemu ya mwili wa mama anapokuwa mjamzito. Sehemu hiyo humsaidia mtoto kupata chakula na hewa kutoka kwa mama akiwa tumboni.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili, Meshack Shimwela anasema kondo la nyuma ni ogani iliyojishikilia katika ukuta wa nyumba ya uzazi ambayo huunganika na kitovu cha mama na hivyo kuwa kama daraja linalomuunganisha mama na mtoto kabla hajazaliwa.

Ogani hii husafirisha hewa safi, damu, huchuja chakula na kukitoa kwa mama kwenda kwa mtoto, hutoa hewa chafu pia na uchafu kutoka kwa mtoto kwenda nje. "Kondo la nyuma si nyumba ya uzazi bali ni kiungo kinachoumbwa mara baada ya mimba kutungwa kwa sababu ya kumuunganisha mama na mtoto," anasema Dk Shimwela.

Baada ya mtoto kuzaliwa kiungo hicho hutoka mwilini mwa mama anaposukuma mtoto au hutolewa na madaktari anapofanya upasuaji. Pamoja na kumsaidia mtoto kupumua, ogani hiyo humlinda mtoto na maambukizi ya magonjwa iwapo yapo kwenye mwili wa mama na huzalisha vichocheo vinavyoulinda ujauzito.

Baada ya mama kujifungua tu, kondo la nyuma huishia hapo hapo na kutupwa. Lakini si wote wanaolitupa; hulitumia kama dawa. Baadhi hulikaanga na kula kama nyama, wengine kukausha na kutengeneza tembe au vidonge na pia wapo wanaolila likiwa bichi hivyo hivyo mara tu baada ya kutoka tumboni mwa mama.

  • Nchini China na Vietnam, hii hufanywa kama mila kwa kondo la nyuma kuandaliwa na kuwa chakula cha mama.
  • Makabila ya mataifa haya yanaamini kuwa kondo la nyuma lina utajiri wa viinilishe mbalimbali ambavyo mama huhitaji mwilini ili apone kwa haraka baada ya kujifungua.
  • Nchini Italia, wanawake wanaamini kula sehemu ya kondo la nyuma kunasaidia kuongeza maziwa ya mama baada ya kujifungua.
  • Nchini Hungary wanawake hutafuna sehemu ndogo ya kondo hilo na huhifadhiwa ili siku zijazo watakapopata ujauzito wazuie matatizo yanayoambatana na mimba hasa katika kipindi cha kujifungua.
  • Baadhi ya makabila pia yanaamini kuwa wanawake wakila kondo la nyuma baada ya kujifungua hawawezi kutokwa na damu kwa wingi kwani lina wingi wa viondoa sumu.
  • ​Baadhi ya wataalamu wa afya wanadai kuwa kondo la nyuma lina vitamin na madini ambayo huweza kuondoa msongo wa mawazo.

Kondo hilo linatajwa kuwa na wingi wa madini ya chuma na protini ambayo huwasaidia wanawake kurejesha nguvu na afya baada ya kujifungua. Nchini China, utafiti uliofanyika mwaka 1954 na kujumuisha wanawake 210, ulibaini kuwa kondo la nyuma linazalisha maziwa ya mama kwa wingi. Asilimia 86 ya wanawake waliokula ogani hiyo baada ya kujifungua waliongeza maziwa kwa wingi kwa kipindi cha siku chache.

Kampuni moja nchini Uingereza inayotengeneza bidhaa mbalimbali kwa kutumia kondo la nyuma, hulipisha watu kati ya Pauni 150 za Kiingereza au Dola 170 za Kimarekani kwa kila tembe. Pia hutoza chini ya Dola 50 za Kimarekani kwa maji ya kondo hilo likiwa limesagwa.

Dk Shimwela anasema ni vigumu kulila kondo la nyuma kwani lina taswira ya nyama mbichi na lenye maji mengi kiasi kwamba halichukui muda mrefu kuoza. "Ndiyo maana baada tu ya wanawake kujifungua, hukusanywa na kuchomwa moto hadi kuwa majivu kwani yanaweza kusababisha maambukizi ya maradhi kwa urahisi zaidi," anasema. Lakini anakiri kuwa kondo la nyuma hubeba viinilishe vingi zaidi na ndiyo maana baadhi ya watu hutengenezea bidhaa mbalimbali.

Bidhaa zilizotengenezwa na kondo la nyuma
Zipo bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia kondo la nyuma. Hapa nchini kipo kipodozi cha kuimarisha nywele (steaming) kiitwachoplacenta. Si hivyo tu yapo mafuta ya ngozi, dawa za kusafisha nywele na mafuta ya kuzuia uzee.

Kondo la nyuma kama tiba
Kondo la nyuma ni chanzo cha viinilishe ambavyo hutumika katika kutibu baadhi ya magonjwa kama vile pumu, mishipa ya fahamu, moyo kushindwa kufanya kazi, unywaji wa pombe, saratani hasa ile ya ngozi ijulikanayo kama kaposi sarcoma.


Mkurugenzi mtendaji wa kliniki ya kimataifa ya mama, baba, kijana na mtoto, Dk Ali Mzige anasema kondo la nyuma si kitu safi na wala hawezi kuruhusu mtu yeyote alitumie kama bidhaa au chakula. "Ni kitu kichafu mno. Utajuaje kama lina HIV, kaswende, homa ya ini au maradhi mengine. Sitaki hata kufikiri kuhusu binadamu kutumia kitu hicho. Ndiyo maana tunayachoma kabisa," anasema.

Dk Mzige anasema kondo la nyuma kutumika kama tiba au bidhaa bado hakujathibitishwa kisayansi na nafasi ya kusababisha maambukizi ni kubwa. Pamoja na kuwa kondo la nyuma linamkinga mtoto na maambukizi, bado halizuii pombe, kemikali ya nikotini na baadhi ya dawa kali kupenya na kumdhuru mtoto.

Wakunga huhakikisha kuwa kondo la nyuma limetolewa mara tu baada ya mama kujifungua. Endapo ogani hiyo itasahaulika huweza kusababisha kifo au madhara makubwa kwa mama.

Wanyama kama ng'ombe, mbwa na simba hulila kondo la nyuma mara baada ya kuzaa kwa sababu huwa na njaa kali. Kwa sababu hiyo, anashauri watu wasiwe na mawazo ya kushawishika kulitumia kama dawa wala kama kichocheo cha kuongeza maziwa kwa mtoto.

Anaelezea huo kuwa ni kama uvumi tu ambao hajathibitishwa kisayansi na unaweza kuwa chanzo cha kueneza maradhi mengine.

Source: Mwananchi
 
Kuna watu wanakula ubongo wa binadamu hali hii huitwa cannibalism.
Chonde chonde tusipoangalia kina mama wajawazito watawindwa kama swala ili kujipatia nyama ya placenta
 
Kuna watu wanakula ubongo wa binadamu hali hii huitwa cannibalism.
Chonde chonde tusipoangalia kina mama wajawazito watawindwa kama swala ili kujipatia nyama ya placenta

IMG_1932.jpg

Binafsi sioni sababu za msingi kwa kinachojadiliwa katika mada hizi, inaonekana tu ni imani tu za watu na hakuna hoja za msingi kisayansi. Hii ni sawa na Cannibalism (wala-watu si kiuchawi ila kwa uwazi) kama ulivyosema. Kazi yake ya msingi ni moja tu kubeba na kumtunza mtoto na akishafikisha umri wa kuwa nje ya mama kwa kutokuwa parasite kwa mamake ndio mwisho wake.

Hata katika makabila kadhaa nchini Tanznia ambayo huzalishwa kwa njia za wakunga wa kienyeji wanataratibu zao tofauti na inavyofanyika mahospitalini, wengi huzitunza na wengine huzizika, lakini si kwa uwazi, ni kwa siri, nini kinaendelea huko sirini wao wanajua.

Mbona hata utumbo unaobakia kwenye kitovu cha mtoto baada ya kuzaliwa ambacho huanguka baada ya siku kadhaa kikisha kauka huwa wengine wana mila na desturi za kukitunza, ingawa vijana wengi wa siku hizi hana mazoea hayo.
 
Tamaduni na mazoea tu, halafu kuna mchangiaji amesema 'kanibalizimu' ni kula ubongo wa binadamu ingawa navyofahamu mie ni kula nyama ya binadamu.
 
dunia haijaisha hivyo vitamin supplements kabisa ?? au zimeisha kabisaaaa tuanze kufikiria kula placenta mnh mie ngumu kumesa hii...oteee
 
Nusra nitapike loh

Sent from my BlackBerry 9320 using JamiiForums
 
Hii ni dawa ya kusaidia kuzifanya nywele zisikatike na ziwe na mng'ao mzuri. Imetengenezwa Italy. Mara ya kwanza kuiona nami nipishtuka sikuamini lakini ndo ukweli inatoka ktk placenta.

Na ina matokeo mazuri sana. Kwani nywele zinapendeza kweli.
 

Attachments

  • 1401159724974.jpg
    1401159724974.jpg
    73 KB · Views: 95
  • 1401159772220.jpg
    1401159772220.jpg
    78.4 KB · Views: 96
Bahati mbaya lugha iliyotumika ni kitaliano so sikuona haja ya kuchukua sehemu ya nyuma yenye maelezo yake.
 
Back
Top Bottom