KERO Baadhi ya Watumishi tuliokuwa hospitali ya Ubungo tunadai 'overtime' kwa muda mrefu

KERO Baadhi ya Watumishi tuliokuwa hospitali ya Ubungo tunadai 'overtime' kwa muda mrefu

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Mimi ni miongoni mwa watumishi wa mkataba waliowahi kufanya kazi katika Hospitali ya Wilaya ya Ubungo iliyopo Kimara Baruti. Nilisitisha mkataba wangu kwa kufuata utaratibu wa kutoa barua rasmi ya kusitisha mkataba.

Ninaandika kuwasilisha malalamiko kuhusu kutolipwa malipo ya overtime tuliyofanyia kazi kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Juni 2026, kabla ya kusitisha mkataba.

Kwa mshangao, baadhi ya watumishi wengine wamelipwa malipo yao ya overtime, wakiwemo watumishi walioajiriwa rasmi na Serikali pamoja na baadhi ya watumishi wa mkataba waliokuwa bado wanaendelea na kazi hospitalini au hata wale waliokuwa tayari wameondoka. Hata hivyo, sisi baadhi yetu ambao tulikuwa na madai hayo hatujalipwa hadi sasa.

Tulipofuatilia suala hili katika mamlaka husika, tulipewa majibu ambayo hayakuwa ya kuridhisha. Tuliambiwa kuwa hatujalipwa kwa sababu hatupo tena katika mazingira ya kazi ya hospitali, kwamba malipo hayo yalikuwa kama msaada kwa watumishi wa kujitolea na si haki yetu, au kwamba tusubiri hadi mapato yatakapokusanywa tena.

Maelezo hayo yanatupa maswali mengi, kwa sababu sisi hatukuwa watumishi wa kujitolea. Tulikuwa watumishi wa mkataba uliokuwa ukihuishwa kila baada ya miezi mitatu, na nyaraka za ajira hazikuonyesha kuwa tulikuwa tunafanya kazi kwa kujitolea. Tulifanya kazi hizo za ziada kwa wajibu na kwa matarajio kuwa tutalipwa stahiki zetu kama ilivyo kwa watumishi wengine.

Tunaomba viongozi husika, hususan Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, kusaidia kulifuatilia suala hili ili tupate haki yetu.

Tulitoa huduma kwa moyo wote na kutekeleza majukumu yetu kwa uaminifu, hivyo tunaamini tunastahili kulipwa malipo hayo ya overtime kwa kazi tuliyofanya.

Tunawasilisha kwa heshima.
 
Back
Top Bottom