Baba Mtakatifu Francisko, ameteua Makardinali wapya Ishirini na Moja (21), mmoja anamiaka 99 na ametangaza kuwasimika rasmi Disemba 08, 2024 katika Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.
Baba Mtakatifu ametangaza uteuzi huo Dominika ya Oktoba 6, 2024 majira ya mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana na kusema kuwa watasimikwa siku ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ambayo hufanyika kila mwaka Disemba 08.
Amesema lengo la kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwenye Baraza la Makardinali ni kushuhudia Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, ambapo mpaka sasa kuna Makardinali 256.
Aidha, amesema kazi ya Makardinali kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Hata hivyo, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu ni kwa sababu kila sehemu kuna wawakilishi wa Baba Mtakatifu, ambao mara zote hupeleka vipaji vyake na kwa Kanisa lote na daima hufanya juhudi kila mmoja ili kupata ukamilifu katika umoja.
Baba Mtakatifu Fransisko amewaomba waamini kuendelea kuwaombea Makardinali hao ili kwa kuteuliwa kwao wakashikamane kabisa na Kristo Kuhani Mkuu, mwenye Huruma na mwaminifu na ili wamsaidie kiuaminifu katika majukumu yake kwa watu wa Mungu.
#Redio Maria Tanzania