Kongamano kupinga ufisadi lahusishwa na chama kipya
KONGAMANO kubwa la kupinga ufisadi linatarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo hivyo, huku likihusishwa na Chama Cha Jamii (CCJ).
Waandaaji wa kongamano hilo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyo ya Serikali ya Aford, Julius Miselya Seneta, alisema jana kuwa kongamano hilo la siku mbili litafanyika kuanzia Februari 13 mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee.
Tangazo la kufanyika kwa kongamano hilo, limekuja zikiwa ni siku chache tu baada ya maombi ya kusajiliwa chama kipya cha siasa cha CCJ kuwasilishwa ofisini kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Miselya alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye atakuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo ambalo litahudhuriwa na wasomi, wanafunzi, wanasiasa na watu wa rika zote.
Sisi kongamano hili tumeliandaa ili kuipa fursa serikali iseme namna inavyowashughulikia mafisadi, tunaamini wananchi wataelewa kwa kina mambo yanayofanywa na serikali yao, alisema Miselya.
Wakati Miselya anasema hivyo, habari zimedai kuwa nia ya kongamano hilo ni kufikisha kilichoitwa ujumbe kwa wananchi wa namna Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyochukia na kupambana kikamilifu na ufisadi.
Hatimaye ni wananchi hao kuwa waangalifu na makini katika uchaguzi mkuu ujao wasiwachague viongozi mafisadi, kilisema chanzo chetu cha habari kilicho karibu na kamati ya maandalizi ya kongamano hilo.
Miselya alisema watoa mada kwenye kongamano hilo watakuwa ni wanataaluma kutoka vyuo vikuu nchini ambao alidai wana weledi wa hali ya juu katika kueleza mambo yanayohusu utawala bora.
Hatutaki wawe wanasiasa, wanaweza kuligeuza kongamano hilo kama jukwaa la wanasiasa, alisema Miselya ingawa kuna taarifa kuwa miongoni mwa watoa mada ni mtu mwenye wadhifa bungeni na mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam.
Hawa wamekuwa mstari wa mbele na watu makini waliojitolea kikamilifu kupambana na ufisadi wengine watakuwa wachangiaji tu, kilisema chanzo chetu cha habari. Miselya, ambaye ni mmoja wa waasisi wa NDC hakutaka kabisa kuwataja watoa mada hao akisema bado tunawasiliana nao siwezi kuwataja.
Alipoulizwa kwa nini wamemwalika Waziri Mkuu kuwa mgeni rasmi, Miselya alisema awali walizungumza na Mzee Rashidi Kawawa kabla hajafikwa na mauti.
Sasa tumemwomba Waziri Mkuu kuwa mgeni rasmi, lakini awali pia tulimtaka Rais Jakaya Kikwete, lakini tumeshauriwa kuwa ni mtu mwenye shughuli nyingi, itakuwa ni vigumu.
Huyu kwa sasa tunaona anafaa awe mgeni rasmi hasa kwa hatua yake ya kutangaza mali na kuwatimua maofisa wa halmashauri ya Bagamoyo, anaonesha anachukizwa na vitendo vya ufisadi, alisema.
Alipotakiwa kusema kama kongamano hilo lina uhusiano wowote na kuanzishwa CCJ, alisema halina kabisa.
Habari zilisema kongamano hili halitakuwa na tofauti na lililofanyika hivi karibuni Karimjee chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, kwani washiriki wengi watakuwa ni wale wale.
Ilielezwa pia kuwa washiriki hao miongoni mwao ndio wako nyuma ya uanzishwaji wa CCJ, chama ambacho kiliwasilisha maombi yake ya usajili kupitia kwa Mwenyekiti wa muda, Richard Kiyabo na Katibu wa muda, Renatus Mubhi.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Mubhi aliwahi kuwa mwanajeshi mwenye cheo cha ukoplo, ambaye inadaiwa anahamasisha wanajeshi wastaafu kudai mafao yao kama ushawishi wa kuwataka wajiunge CCJ.
Inadaiwa Mubhi, ana undugu na Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wabunge wanaotarajiwa kujiunga na chama hicho na kwamba ndiye mratibu mkuu wa shughuli za chama.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano huo, Mubhi alisema hana uhusiano na Mbunge huyo na wala hamfahamu na kuhusu madai kuwa anahamasisha wanajeshi wastaafu kudai haki zao ili wajiunge CCJ, alisema hizo ni chuki za wasiompenda wanaotaka kumchafulia jina.
Hao wanataka kunichafulia jina, hata hivyo chama chetu hakina lengo baya, na CCM ina hofu dhidi yetu sasa hivi hatutasema mengi tusubiri usajili wa muda kwanza ndipo tutazungumza, alisema.
Kuhusu madai kuwa alitoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) makao makuu akiwa Koplo baada ya kuhamishiwa Arusha, alisema si kweli na aliacha kazi kwa hiari yake na kujiunga na siasa.
Naye Mpendazoe alipoulizwa kuhusu uratibu huo na uhusiano na Mubhi, alisema yeye bado ni mwana CCM na ni mwakilishi wa watu na wanaomhusisha na CCJ wanaweza kuwa na nia yao.
Siwezi kuzungumzia mambo ya CCJ kwa sababu mimi ni CCM na huyo Mubhi si ndugu yangu na nasikia anatoka mkoa wa Mara hata angekuwa ndugu yangu kuna tatizo? Mbona Slaa (Wilbrod) yuko Chadema na mkewe CCM na wanaishi pamoja? Kila mtu ni mtu mzima, alisema.
Maandalizi ya kongamano hilo ambalo awali lilikuwa lifanyike Diamond Jubilee, yanaendelea na waalikwa watatakiwa kununua fulana na kofia maalumu zenye picha ya Mwalimu Nyerere na maandishi ya kuhamasisha mapambano dhidi ya ufisadi.
Fulana na kofia hizo zitauzwa kati ya Sh 20,000 na Sh 7,000 kila moja ili kuchangia gharama za kongamano hilo ambazo ni karibu Sh milioni 10 kwa ajili ya vinywaji, chakula na ukumbi, kilisema chanzo chetu.
Kilisema hadi sasa fulana 5,000 zimetengenezwa kwa gharama ya Sh 12,000 kwa kila moja katika kampuni moja Dar es Salaam na zinaandaliwa zingine milioni moja.
Habari zaidi zilisema waandaaji wanawasiliana na kituo kimoja cha televisheni ambacho kitarusha kongamano hilo moja kwa moja kwa kati ya saa mbili na tatu kwa malipo ya Sh milioni nane.
Alipoulizwa kama wana kibali cha kufanya kongamano hilo, Miselya alisema kwa kuwa ni mkutano wa ndani, hawahitaji kuomba kibali na kuhusu usajili wa Aford, alisema ilisajiliwa mwaka 1997 na iliyokuwa Ofisi ya Kabidhi Wasii wa Serikali, ambayo sasa ni RITA (Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini).
CCJ ni chama ambacho kinadaiwa kuanzishwa na baadhi ya wanaCCM ambao wanapambana na ufisadi, pamoja na baadhi ya walioshindwa katika kinyanganyiro cha urais mwaka 2005 kwa tiketi ya CCM na inadaiwa kaulimbiu yao inatokana na jina la chama Sisi Je (CCJ)?
Source,,,http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=5365