Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakati wa kikao cha Tathmini cha maandalizi ya maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichofanyika tarehe 21 February 2024 Jijini Arusha, ugomvi mkubwa uliibuka kati ya aliyewahi kuwa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema na wajumbe wa kamati ya maandalizi.
Mashuhuda wa tukio hilo wamedai chanzo cha ugomvi huo ni kitendo cha CHADEMA makao makuu kugoma kutoa fedha za bajeti ya maandamano kiasi cha TZS Milioni 160 na badala yake kuutaka uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Arusha kuendesha harambee, jambo lililopingwa na wajumbe wengi wakihoji uhalali wa makao makuu kuzuia fedha za chama zilizotolewa na Serikali kama Ruzuku katika tukio la kitaifa.
Hoja za wajumbe zilipingwa na Ndg Godbless Lema ambaye alionyesha kuchukizwa na madai ya wajumbe na kuamua kuanza kutoa lugha ya kejeli kwa kudai wajumbe hao hawana uchungu na chama hivyo yeye ataendesha harambee kwani hawezi kusubiri huruma za makao makuu kutoa fedha kwaajili ya uratibu, jambo lililoibua hisia kuwa Ndg Lema anayo mambo ya siri anayopanga kutekeleza kupitia maandamano.
Mpaka kufikia siku ya Ijumaa, tarehe 23 Februari 2024, watu wa karibu wa Godbless Lema wamethibitisha kuwa kiongozi huyo anaendesha harambee kwa wafanyabiashara yeye mwenyewe na tayari amekusanya zaidi ya Milioni 80. Baadhi ya wajumbe wameeleza kuchukizwa na dharau iliyoonyeshwa na Lema kwa kutosikiliza hoja yao iliyojikita katika kutaka Chama kutoa fedha badala ya kuchangisha wananchi kutokana chama hicho kupokea ruzuku takribani TZS Bilioni 2.7.
Kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja ya viongozi wa Kanda ya Kaskazini ameeleza kusikitishwa na kitendo cha viongozi wa makao makuu kutojali mambo yanayofanyika mikoani hususani linapokuja suala la kibajeti, aidha kiongozi huyo amedai kuwa wapo viongozi waliotoka mikoa mbalimbali kwaajili ya kuhamasisha maandamano ambao mpaka sasa hawajapewa stahiki zao jambo ambalo wanaona siyo la kiuungwana.