EPA yatikisa Bunge
2008-06-21 10:05:07
Na Boniface Luhanga, Dodoma
Wabunge wa CCM wameaswa kutogawanyika kuhusu suala la mafisadi waliochota fedha za Benki Kuu Tanzania (BoT) kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, bungeni jana, Bi. Anna Abdallah (Viti Maalum-CCM) alisema hakuna mbunge anayeogopa kuzungumzia suala la ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (EPA) na kwamba halipaswi kuwagawa wabunge.
Bi. Abdallah alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu Bi. Anna Kilango Malecela (CCM-Same Mashariki) atoe wito kwa wabunge wenzake kutoogopa vitisho katika kuzungumzia suala hilo ili mradi wanasimamia ukweli na haki.
Bi. Abdallah alisema kimsingi hakuna mbunge anayeogopa kulizungumzia hilo isipokuwa wanatofautiana katika kulisema.
``Baadhi wanalisema kwa madoido huku wengine tukilisema kwa upole lakini wote hatuogopi wala kutishwa ndani ya Bunge,`` alisema.
Hata hivyo, alisema vyombo vya habari, hususan magazeti, kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakichangia kuwa ndani ya Bunge kuna mtafaruku kuhusiana na sakata la EPA.
Alisema wabunge wote wana lengo moja la kuhakikisha kwamba, wanakemea vitendo viovu vinavyofanyika ndani ya jamii.
Aidha, mbunge huyo pia aliishauri serikali kuvitumia vikosi vya ujenzi vya majeshi ya JKT, JWTZ, Polisi na Magereza katika kujenga nyumba za taasisi hizo badala ya kuwatumia wazabuni kwa lengo la kubana matumizi.
Bi. Abdallah alisema haoni mantiki kwa serikali kutumia wazabuni kujenga nyumba za taasisi hizo huku kukiwepo na vikosi vya shughuli hiyo ndani yake.
Kuhusu suala la Tanzania kukemea vitendo vinavyoendelea nchini Zimbabwe, Mbunge huyo alisema Tanzania imechelewa kutoa tamko hilo.
Bi. Abdalla alisema si busara kuendekeza mambo yanayoendelea kutokea nchini Zimbabwe kwa sasa hasa kwa kuzingatia kwamba, Rais Jakaya Kikwete ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
``Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe) anapaswa kuambiwa (ukweli) pale anapofanya tofauti,`` alisema.
Juioni jana wakati akifanya majumuisho, Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, alisema kwamba Serikali inasubiri ripoti ya Timu iliyoundwa na Rais ndipo inaweza kuwa katika nafasi ya kulizingumzia suala hilo pamoja na hatua za kuchukua.
Aidha alisema pesa hizo za EPA si za BoT wala serikali bali wafanyabiashara ambao wengi wako nje ya nchi ama walikufa.
Bajeti ilipitishwa jana na wabunge wengi wa CCM na kwa upinzani aliyeipitisha ni John Momose Cheyo. Bajeti ambayo hupitishwa kwa wabunge kusema `Ndiyo`ama `Hapana` wabunge wengi wa upinzani walisema `abstantion` wakimaanisha hawakubali wala hawakatai.
Wakati huo huo, Simon Mhina anaripoti kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba, amekanusha uvumi kwamba kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana mjini Dodoma hivi karibuni ilizima kujadiliwa kwa hoja za EPA pamoja na sakata la Richmond.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Bw. Makamba, alisema ni kweli hoja za kuwashughulikia mafisadi zilizuka ndani ya kikao hicho, lakini yalitolewa maelezo ya kina yaliyohusu umuhimu wa kutolijadili, lakini kamwe halikuzimwa.
Akifafanua, alisema si kweli kwamba CCM inawaogopa watu wanaoitwa mafisadi, lakini ni vema vyombo husika vyenye madaraka kwa mujibu wa nchi vikaachiwa kushughulikia tatizo la mafisadi.
Alisema kitu ambacho CCM inaweza kukifanya ni kuwashauri wale wanaotuhumiwa waachie madaraka ili kukisafisha chama na serikali yake, jambo ambalo limekuwa likifanyika.
Bw. Makamba, alisema CCM ni chama cha siasa na sio dola, japokuwa ndicho kimeunda serikali.
``Hatutaki kuingilia kazi ya serikali, tuhuma za ufisadi iwe EPA, Richmond au sijui vijisenti, zote hizo zinashughulikiwa na vyombo vya dola. Hii siyo kazi ya Halmashauri Kuu, hii sio siasa,`` alisema.
Alisema kama watuhumiwa wangekuwa wameshtakiwa kwenye vikao vya chama, hapo CCM ingewajibika kuchunguza, lakini kwa vile tuhuma hizo zimeanzia nje na zingine bungeni ni busara sheria ikachukua mkondo wake.
``Wengine walisema mafisadi wafukuzwe ndani ya chama. Jamani hawa ni watuhumiwa, tuwafukuze halafu tukifika kwa wananchi waliowachagua tukawaambie tumewafukuza viongozi wao kwa sababu zipi?`` Alihoji.
Bw. Makamba, alikiri kwamba katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana hivi karibuni, baadhi ya wajumbe walitaka chama kikemee wakubwa wa serikali ambao baada ya kujiuzulu kufuatia tuhuma za ufisadi, wafikapo kwenye majimbo yao wanalakiwa kwa nderemo na wapiga kura wao.
Katibu huyo alisema wajumbe hao walikuwa hawajaelewa dhana nzima ya kujiuzulu, kwamba ni \'kuwajibika` lakini kamwe sio kukiri kosa.
``
Kujiuzulu ni moja ya sifa za ustaarabu na uadilifu, sasa hawa waliojiuzulu, kisha wapiga kura wao wakawapokea, bila shaka wamewapokea kwa sababu ya ustaarabu waliouonyesha,`` alisema na kuongeza ``Hawa bado ni wabunge, na wengine ni wajumbe wa Halmashauri Kuu, hatuwezi kuwanyima haki zao za kisiasa na kikatiba eti tu kwa sababu wametuhumiwa.``
Kuhusu madai yaliyotolewa kwamba katika kikao hicho, wajumbe walisema kwamba wanataka CCM kama ile aliyokuwa anaongoza Mwalimu Nyerere irejee, Bw. Makamba, alisema Mwenyekiti Jakaya Kikwete ameshairejesha.
Alisema sifa moja ya CCM ya Nyerere ilikuwa kukaa pamoja na kujadili matatizo ya kila mtu, kukosoa na kisha watu wote wanatoka kwa umoja.
``Ndicho kilichotokea juzi, kila mjumbe alitoa dukuduku lake, mwenye kulaani ufisadi alifanya hivyo, mwenye kumlaumu Makamba alifanya hivyo na baadaye tukafikia majumuisho kisha tukakubaliana. Hii ndo CCM ya Nyerere ambayo tuliapa kuwa tutasema kweli daima, fitina kwetu ni mwiko,`` alisema.
Bw. Makamba, alisema kama kuna mjumbe aliyeacha kutoa hoja yake kwenye kikao hicho na kulalamika kwenye vyombo vya habari, amekiuka kiapo cha CCM.