Shura ya Maimamu Tanzania, imezindua ‘Muongozo' kwa ajili ya waumini wa Kiislamu ambao itawaongoza wakati Watanzania wakielekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Uzinduzi wa Muongozo huo unafanyika miezi michache baada ya Kanisa Katoliki nchini kutoa waraka unaowaelekeza waumini wake namna ya kuwachagua viongozi waadilifu wakati wa uchaguzi huo.
Muongozo huo uliopewa jina la "Muongozo kwa Waislamu", ulizinduliwa jijini Dar es Salaam jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja na Katibu wa Kamati Kuu ya Siasa ya Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya waumini wa jumuiya na taasisi za Kiislamu za Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.
Muongozo huo ulio kwenye mfumo wa kijitabu chenye kurasa 45, umejikita zaidi katika kueleza maeneo 15, ikiwamo dhana ya maisha bora, hadaa za uchaguzi na dira ya Waislamu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Maeneo mengine ni taswira ya uchaguzi uliopita, dhana ya uchaguzi, uhuru wa kutoa maoni, tumefikaje hapa tulipo, maadili, elimu, afya, kilimo, fedha na uwezeshaji, umoja na amani, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na uwakilishi.
Akizindua Muongozo huo, Sheikh Ponda alisema wamefikia hatua hiyo kwa vile Waislamu ni jamii iliyodhulumiwa, ambayo inahitaji ukombozi na uhuru.
"Lakusikitisha Waislamu leo wanadai uhuru kutoka kwa ndugu zao weusi," alisema Sheikh Ponda.
Alisema anamshangaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, kuwataka Waislamu wasitoe Muongozo wao kwa vile waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki umechafua mazingira na kuhoji: "Marmo alikuwa wapi hadi waraka ule ukachafua mazingira?"
Awali, akifungua mkutano huo, Amiri wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha, alisema kilichozinduliwa na Waislamu kisichukuliwe kuwa ni waraka kwa kuwa waraka ni kitu kinachotoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, bali walichozindua jana, ni Muongozo kwa Watanzania wote.
Kutokana na hali hiyo, alisema iwapo serikali itaufuata Muongozo huo, itafanikiwa katika kutawala na ikiupuuza itawatawala Watanzania katika mazingira magumu, ambayo hayajapata kutokea.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Baraza Kuu), Sheikh Ramadhan Sanze, alisema Muongozo huo utaisaidia serikali kutawala vizuri, Watanzania kuishi kwa amani na waumini wa dini mbalimbali kutobaguana.
"Ni mwongozo kwa watu wote na si njama," alisema Sheikh Sanze.
Alisema tofauti na Muongozo huo, ipo hati ya makubaliano (MoU) iliyotiwa saini kati ya serikali na makanisa kwa lengo la kuwapendelea Wakristo nchini mwaka 1992.
Hata hivyo, Sheikh Sanze alisema anashangazwa namna MoU ilivyotiwa saini na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kwa niaba ya serikali.
Naye Sheikh Mohamed Issa akiwasilisha mada ya hali ya Waislamu kabla na baada ya uhuru Tanzania, alisema Muongozo huo hauna lengo la kuwabagua baadhi ya wanadini na kuwapendelea wengine, bali umejikita zaidi katika kuwataka Waislamu wasikubali kudhulumu na kudhulumiwa.
Alisema kwa kuzingatia hilo, katika uchaguzi ujao, Waislamu wako tayari kumchagua mgombea yeyote, asiyekuwa na chuki na Waislamu bila kujali anatoka chama gani cha siasa.
"Ila akiwa ana dalili za ufisadi hata akiwa Muislamu wa aina gani hatutamchagua," alisema Sheikh Issa.
Naye Imamu Mkuu wa Msikiti wa Idrisa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Maalim Ally Bassaleh, alisema Waislamu wamekuwa wakidanganywa muda mrefu na kuwataka waumini hao katika uchaguzi mkuu mwakani kuhakikisha wanatamka: "Hatudanganyiki."
CHANZO: NIPASHE