DuaZaMama
JF-Expert Member
- Jun 2, 2025
- 1,882
- 4,153
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza orodha ya Taasisi na Asasi 164 zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kuelekea Oktoba mwaka huu.
Taasisi na Asasi hizo zitakuwa na jukumu la kutoa elimu ya mpigakura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani.
Orodha hiyo imewekwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya INEC.
Aidha, katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima imeeleza kuwa Taasisi na Asasi zilizopewa vibali zinapaswa kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwamo kuweka orodha ya watakaotoa elimu hiyo.
Orodha hii imetolewa ikiwa ni siku chache kufika Julai 25 ambapo INEC imesema itataja tarehe ya uchaguzi wa viongozi hao.
Hadi sasa ni vyama 18 pekee vimesaini Kanuni za Maadili ya uchaguzi ambavyo vimeridhia kushiriki Uchaguzi Mkuu,huku CHADEMA ikiendelea na msimamo wake wa 'No Reforms No Election'.
Jumla ya Taasisi na Asasi 76 za ndani zimepewa kibali cha kuwa waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani Oktoba mwaka huu.
Aidha,Balozi 10,Umoja wa Ulaya (EU),Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),na asasi moja ya kimataifa zimepewa kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi huo.
Taarifa iliyotolewa jana Julai 19,2025 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima kwenye tovuti na mitandao yake ya kijamii, imetaja orodha ya Taasisi na Asasi zilizopewa vibali hivyo.
Aidha,amezitaka Taasisi na Asasi hizo kuwasilisha majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi kwa ajili ya kupata vitambulisho.
