CCM HAWALIONI JANGA HILI?
Rais Dkt. John Magufuli
Na Balinagwe Mwambungu,
Mtanzania
NCHI yetu inaonekana katika uso wa kimataifa kuwa na waoga na wanafiki, tunatumia vibaya rasilimali fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo ya nchi yetu.
Tamko la Rais John Magufuli la kutowasomesha watoto wanaopata ujauzito wakiwa bado wanasoma, limewaacha midomo wazi wadau wa elimu wa ndani na nje ya nchi.
Tangu tupate uhuru, nchi kadhaa duniani—hasa za Scandinavia—Sweden, Norway na Denmark, zimemwaga fedha nyingi za walipakodi wao kwa ajili ya kuinua sekta ya elimu. Mfano wa kudumu ni uwepo wa Shirika la Elimu Kibaha. Aidha, kuna shule mbalimbali za sekondari zilizojengwa kwa msaada wa nchi hizo—mfano ni Shule ya Sekondari Bagamoyo. Nchi hizo zimegharimia upanuzi na ukarabati wa shule mbalimbali, hasa wakati wa utawala wa Rais Mwalimu Julius Nyerere.
Si hivyo tu, nchi hizo zimesaidia kuendesha miradi ya elimu kwa watoto waliokosa kwenda shule kwa sababu mbalimbali, zikiwamo mimba za utotoni na zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike walio sekondari.
Rais Magufuli amesema wakati wa utawala wake, watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, hawataweza kuendelea na masomo tena.
Hakuna kiongozi yeyote—kuanzia mawaziri wa elimu, afya na ustawi wa jamii—wanaoogopa kumweleza Rais Magufuli ukweli kwamba elimu ndio msingi wa maendeleo na hatutaweza kuendelea na kufikia nchi ya uchumi wa kati, kama sehemu ya jamii yetu imeachwa nje ya mfumo wa elimu na kwamba wizara zao tayari zilikuwa zinatekeleza programu iliyowalenga watoto wa kike—walioshindwa kuendelea na masomo sababu ya kupata ujauzito.
Tanzania ni kati ya nchi zinazoendelea ambazo zimesifiwa katika anga za kimataifa kuhusiana na hatua yake ya kumwelimisha mtoto wa kike na utekelezaji wa haki ya mtoto kupata elimu. Sijui wadau ambao wamekuwa bega kwa bega na nchi yetu katika kuendelea na kuboresha elimu kwa ujumla!
Inashangaza jinsi jamii ya Kitanzania ilivyobadilika ghafla na kuwa kama kondoo (ambaye hata anapopelekwa kuchinjwa, hunyaa tu). Hivi viongozi wenye dhamana ya elimu, afya na ustawi wa jamii hawana uthubutu wa kumwambia Rais kwamba tamko lake ni pigo kubwa kwao—kwa kuwa wamekuwa wakitekeleza mipango mbalimbali kuhusiana na mimba za utotoni na namna ya kumnasua mtoto wa kike aliyepata ujauzito akiwa shuleni.
Afya na Uzazi wa Mpango na ajenda ya kupunguza mimba za utotoni. Katika programu hii wabunge walipewa majukumu, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa wanawahamasisha watoto wa kike kuendelea na masomo pindi wanapopata ujauzito.
Serikali za mitaa, mashirika ya kiraia na makundi mengine, yalikubali kutekeleza mpango huu. Wizara ya Elimu ilikuwa na programu ya MEMKWA na MMEM, zote zikiwalenga zaidi watoto wa kike waliokuwa nje ya utaratibu wa shule. ‘Mabinti Tushike Hatamu’ ni mradi uliokuwa unaendeshwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa kushirikiana na UNICEF.
Chukua hili kwa mfano, kwamba mtoto wa kike akipata ujauzito, asirudi shuleni baada ya kujifungua—kwa maelezo kwamba watoto wa kike wataona kuwa ni jambo la kawaida na wataendelea kufanya ngono zembe bila kujali kuwa kuna uwezekano wa kupata mimba.
Rais Magufuli alishangiliwa aliposema wakati wa uongozi wake, hakuna mwanafunzi atakayeruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua. Bila shaka, hili ni kama bomu kwa Mama Salma Kikwete (Mbunge), ambaye kwa mwongo mmoja, kupitia taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), amekuwa anampigania sana mtoto wa kike.
Chakushangaza zaidi ni pale viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Amina Makilagi, anaunga mkono kauli hiyo. (Majira Julai 5, 2017). Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alinukuliwa Aprili mwaka huu, akisema watoto wa kike warudi shuleni baada ya kujifungua.
“Tunapowakataza watoto wa kike wasiendelee na masomo pindi wanapopata ujauzito wakiwa shuleni, tunawaadhibu watoto wa masikini washindwe kutimiza malengo yao ya wakati waliotarajiwa,” alisema.
Aidha, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, Februari, 2016, alitoa mwongozo wa namna ya kumruhusu mwanafunzi wa kike kurejea shuleni baada ya kujifugua. Lakini yote haya inaelekea yamefutwa kwa kauli ya Rais Magufuli.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Unicef, Unesco, Shirika la Afya (WHO), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP), yamekuwa yakifanya kazi na Serikali ya Tanzania kutokana na azma yake thabiti ya kutoa huduma, elimu na mafunzo mbalimbali kwa watoto na vijana.
Hii inatokana na ukweli kwamba, hata kabla ya Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu elimu, ilikwishaingiza kwenye Katiba yake na kutamka kwamba binadamu wote ni sawa, ikapiga marufuku ubaguzi wa aina yoyote, na ikaridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto. Mwaka 2009, Bunge likatunga Sheria ya Mtoto ambayo inasema kuwa ni haki ya mtoto kupata elimu bila ubaguzi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wenye ujauzito.
Leo hii kwa tamko tu, mtoto wa kike atakayepata mimba akiwa shuleni, atakuwa amekatishwa ndoto ya ‘kuwa anachotaka’. Wabunge, hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwa madarakani kwa miongo minne, chama ambacho kiliasisi Elimu kwa Wote (UPE), kimekaa kimya! Vijana wa chama hicho—ambao suala hili linawagusa wao moja kwa moja, wamekaa kimya, badala yake wanaandama viongozi wa vyama vingine ambao wanaikosoa Serikali kwamba inatakiwa kutenda haki kwa wananchi wake wote—wadogo kwa wakubwa. Kama vijana wa CCM hawalioni hili kama ni janga la kijamii, basi wanaugua uzezeta.
Katika mwaka 2015, ambao ndio mwaka wa Uchaguzi Mkuu uliomwingiza Dk. John Magufuli madarakani, watoto wa kike 1,271 kutoka mikoa ya Mbeya (322), Morogoro (260), Mwanza (258), Kilimanjaro (235) na Dodoma (196), walikatishwa masomo kutokana na kupata ujauzito. Je, kwa nchi nzima itakuwaje—maana kama Taifa, hatujapata mwarobaini wake.
Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaonyesha kuwa wasichana kati ya umri wa miaka 15 hadi 20 (umri ambao wanatakiwa wawe shuleni), wanaachishwa masomo kwa sababu ya ujauzito.
Taarifa hiyo inasema idadi ya wasichana wanaopata mimba imepanda kutoka asilima 10, mwaka 2010 na kufikia asilimia 27, mwaka 2015/16.
Hata kwa mtazamo wa juu juu tu, hali hii inatishia si tu kuongezeka kwa umasikini, bali pia kuvuruga mipango ya Serikali kwa sababu ya kuwapo duniani watoto ambao hawakuwa katika mipango ya nchi.
Serikali inapigana na umasikini kupitia Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini (TASAF), na mipango mingine ya kupambana na umasikini—huku kukiwa na ongezeko la watoto wasiotarajiwa. Hii ni sawa na kuchota maji na kujaza kwenye ndoo iliyotoboka chini.
Matokeo yake ni wazi—ndoo hiyo kamwe haitajaa. Mipango ya uchumi na kijamii, haitaweza kufaulu. Kutakuwa na midomo mingi ya kulisha, ongezeko la ombaomba, ‘dada poa’ mijini, na watoto wa mitaani, makundi ambayo Jeshi la Polisi linasumbuka nayo kila uchao! Matatizo haya yanatakiwa kutibiwa kwenye vyanzo vyake—si kwenye matokeo.
Vijana wa CCM wanatakiwa kujiongeza. Waache kugombana na wanasiasa ambao hawatakuwapo miaka 50 ijayo, watafute ufumbuzi wa masuala yanayowahusu vijana, hili likiwa mojawapo.
Elimu ni ufunguo wa maisha. Mnyime mtoto elimu, utakuwa umemfungia mlango wa maendeleo. Tunataka Tanzania ya viwanda, ni lazima wawepo watu—hasa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa—vijana waliojizatiti katika fani mbalimbali na watakaoweza kulisukuma gurudumu la maendeleo. Asiwepo atakayeachwa nyuma na boti ya elimu. Usiwepo ubaguzi—kuwabagua waliokoseshwa elimu (sio kwa mapenzi yao).
Kama mtoto wa kike hatapewa nafasi maalumu, basi malengo ya Elimu Bure, hayatafanikiwa.