Hapana.
Nadhani kuna mengi tusiyoyaelewa bado katika makubaliano hayo, na yanahitaji kuelezwa kwa njia rahisi kwa wenye ufahamu wa mambo kama haya.
Bila shaka ufafanuzi mzuri wa makubaliano haya yatakuja kuelezwa, ama na wahusika wenyewe ndani ya serikali, kuwajulisha wananchi tulichopata, au na wabobezi wa lugha hizi za kimikataba.
Kwa mtu kama mimi asiye na uelewa mkubwa wa 'jargon' hizi zinazotumika, kama "a free carried shareholding," au kitu kama "An annual 'true-up' mechanism," kidogo ninafarijika kwa kujua kuwa hali kidogo si haba; sio kama ilivyokuwa wakati wa Acaccia, ambapo hata hiyo namba tu ya 16% ilikuwa haionekani popote.
Utofauti unazidi kujitokeza ninaposoma vitu kama, "The GoT will 'participate in all cash distribution made by the mines and Twiga."
Au, 'statements' kama: "Twiga...will give the government 'full visibility of and participation in operating decisions made for and by the mines..."
Haya yote sio ya kubeza hata kidogo, na hayakuwepo kabisa enzi za Acaccia, na sijui kama yamo katika mikataba ya makampuni mengine nchini.
TAHADHARI ni moja tu. Sisi wenyewe kuyatimiza hayo ipasavyo. Tukimpa Karamagi ayasimamie hayo atayafanya kwa uaminifu, uzalendo wa nchi yake. Huo ni mfano tu, maanake huko ndiko tulikoanzia hadi hapa tulipofika leo.
Kwa hiyo, kwa maoni yangu, tusibeze tulichopata, hata kama sio chote tulichonuia. Ni makosa tuliyafanya huko nyuma kuwapa hawa watu mali zetu kama hatuna akili kichwani.
Napongeza yaliyofanyika, hata kama yalifanyika kwa vurugu. Sikupenda kamwe kuitana majina kama "Wasaliti" kwa vile tu hao wanaoitwa 'wasaliti' wanayo mawazo tofauti.
Palikuwa pia na upotoshaji ambao haukuwa wa lazima. Yale makinikia hata siku moja yasingeweza kuwa na thamani yaliyodaiwa kuwa yanayo. Ndio maana waliohusika katika upotoshaji huo wakapewa jina stahiki kabisa la "Profesorial Garbage,' hata kama ninaelewa sababu iliyowafanya kujidhalilisha vile kama wataalam wetu.
Nimalizie kwa kusema kwamba siijui misimamo ya vyama vya upinzani, hasa CHADEMA kuhusu mali zetu za taifa kama madini. Je, wao wangekuwa madarakani wangefanya nini ili taifa linufaike na hizi mali?
Msimamo wa Zitto Kabwe, ambao pengine ndio msimamo wa ACT-Wazalendo unafahamika, kuwa unaegemea katika mapendekezo ya Tume ya Bomani.
Yote tukiyaweka kwa pamoja, walichofanya CCM (Magufuli) ni sehemu ndogo tu ya kuanzia. Inabidi , kama bado tunayo madini mengine ambayo bado yamo ardhini na hatujayauza kwa wawekezaji, inatubidi turudi kule kule kwenye dira ya waasisi wetu kuhusu madini haya.
Kiasi cha uwezo sasa tunacho cha kujitegemea na kunufaika zaidi na mali hizi alizotujaalia Mwenyezi Mungu. Tuache kuzitapanya ovyo kama akili kichwani hatuna.
Ile Helium kule Rukwa, ije itengeneze ma - mashine ya kupimia wagonjwa hapa hapa kwetu, tuwauzie waafrika wenzetu. Nchi zaidi ya 50, na mahospitali yote yale hatuwezi kukosa wanunuzi. Tuwaite Siemens, Philips, GE, waje wawekeze hapa, hata kama ni kuyaunganisha tu hayo ma-mashine na kuyajaza Helium yetu hapa hapa Tanzania.
Kama hawataki, tuwaite marafiki zetu waChina. Wao wanakopi kila kitu, watashindwa kuyafurumua na kuyaunganisha tena upya , wakitumia mali ghafi zetu wenyewe hapahapa!
Halikadhalika, sijui ni kwa nini tunatupa "Graphite" yetu nzuri kwa bei chee, huku mChina akihodhi ya kwake.