Jinamizi la Nidhamu ya Chama, litamkaba Malima!
Na. M. M. Mwanakijiji
Aliyedhania kuwa sakata la Mhe. Malima na mfanyabiashara Bw. Mengi limekwisha alidhania vibaya. Tulioadhani kuwa baada ya uamuzi wa spika wa tarehe 8 Februari, 2007 ambapo aliamua kuitisha mkutano wa usuluhishi kati ya watu hao wawili mashuhuri tumejikuta tumedanganywa kuachwa solemba. Suala hili kwa sababu fulani bado liko hai na halioneshi ni jinsi gani litamalizika hii karibuni. Siku chache zilizopita Mhe. Samuel Sitta (Spika) amesema kuwa suala hili kwa vile linamhusisha na yeye na inaonekana kuna watu hawakuridhika na maamuzi yake basi litazungumzwa tena Bungeni. Kabla hata kikao hicho hakijasikiliza, mmoja wa wahusika wakubwa wa suala hili Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mkuranga - CCM) ameandika barua ya kutoridhishwa na uamuzi wa spika na hususan kutoridhishiwa kwake na utaratibu mzima aliotumia spika kufikia uamuzi huo wa kuitisha usuluhishi. Bw. Malima ameandika barua hiyo kwa Katibu Mkuu wa CCM ili kuweza kupata nafasi ya kusikilizwa malalamiko yake na hivyo kutafuta suluhisho la kichama zaidi kuliko lile lililopatikana au kupendekezwa na Spika. Bw. Malima amehisi kuonewa na kutotendewa haki.
Msingi mkubwa wa uamuzi wa Mhe. Malima kuandika barua hiyo ni kujaribu kutafuta njia muafaka ambayo itawaweka sawa viongozi hawa wa CCM na hivyo kwa kutumia vikao vya chama hicho basi kujaribu kulimaliza jambo hili kwa heshima na taadhima bila kuendeleza malumbano yasiyo ya lazima. Kwa maoni yake ni kuwa kwa vile yeye ni Mbunge wa CCM na Spika ni Spika anayetoka CCM basi uongozi wa juu wa chama chao unaweza kabisa kutafuta muafaka na kusikiliza hoja za Bw. Malima na hivyo kupata usuluhishi utakaokubalika na pande zote. Kwa maneno mengine, Bw. Malima ana imani na taratibu za chama katika kushughulikia migogoro ya wanachama wake. Bw. Malima anaamini kabisa kuwa kwenye vikao vya huko Dodoma basi kutapatikana suluhisho hilo ambalo litazingatia ukweli wa mambo halisi na hasa kutengua uamuzi wa spika.
Tatizo ni kuwa kabla ya kuandika barua hiyo, Bw. Malima hakuambiwa kuhusu lile jinamizi kubwa lililoko CCM, jinamizi ambalo linaweza kula na kumaliza, ingawa mara nyingi linakula na kubakisha. Ni jinamizi hilo lililowakaba kina Maalim Seif na Shaaban Mloo wakatimuliwa, ndilo jinamizi lililomkaba Mrema akatimka, na ndilo jinamizi hilo hilo lililowapa watu mishtuko ya moyo kila likitokea. Hili jinamizi ni chombo kikubwa kabisa ndani ya CCM ambacho kinawafanya watu wanyamaze na kunywea kama wamemwagiwa maji toka Makambako!! Bw. Malima hajajiandaa kusimama mbele ya jinamizi hilo.
Kabla sijaendelea ni bora niwatajie jina la jinamizi hilo, kwa wengi jinamizi hilo huitwa "nidhamu ya chama". Nidhamu hii ya chama ndio imehakikisha kuwa kuna kuonekana umoja na mshikamano ndani ya chama na ndilo lililohakikisha uwepo wa makubaliano ya pamoja na uwajibikaji wa pamoja ndani ya chama. Jinamizi hilo ndilo limesimamia kwa kiasi kikubwa nidhamu ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduz na hivyo kukifanya chama hicho kuonekana kuwa na umoja unaokosekana katika vyama vingi vya upinzani. Hili ndilo jinamizi ambalo Bw. Malima anatarajia kuweza kulishawishi hadi kukubali hoja zake. Juhudi za Bw. Malima ni kama juhudi za kushawishi jini lililofunguliwa kwenye chupa lisikumeze wakati lina njaa ya miaka 100 ya kifungo! Kwa yeyote anayechunguza masuala ya kisiasa ya Tanzania na ni mchambuzi aliyebobea kama wenu mtiifu, Bw. Malima hana nafasi ya kushinda au kujenga hoja ikakubalika mbele ya jinamizi hilo.
Njia pekee ambapo Bw. Malima anaweza akaondoka akiwa na sura ya ushindi ni pale ambapo vikao vya juu vya CCM vitakapoamua kukataa kusikiliza hoja zake na kumlazimisha kulirudisha suala hili Bungeni. Kwa vile suala hili limeanzia Bungeni na kuhusisha wabunge kwa viongozi wa CCM kuamua kulizungumzia pembeni na kulitolea maamuzi itakuwa ni kosa kubwa kwao na kufanya jambo ambalo CCM halina mamlaka nayo, nalo ni kuichukua kesi toka Bungeni na kuizungumza kwenye vikao vya Chama. Kama CCM inatambua uzito wa Katiba, haiwezi hata chembe kukubali kulisikiliza shauri hili hadi pale taratibu zote za Bunge zitakapofikia kikomo. Kwa vile Spika ameshasema wazi kuwa jambo hili litazungumzwa na Wabunge katika kikao kijacho, kitu chochote ambacho viongozi wa CCM watafanya na vikatafsiriwa kama kujadili suala hili nje ya Bunge, basi itaonekana ni kiburi cha hali ya juu cha CCM kuweza kuingilia shughuli za Bunge. Ni kwa sababu hii peke yake CCM itakaa kulizungumza jambo hili.
Endapo itatokea kuwa CCM itaamua kusikiliza shauri hili na kujaribu kuwaita Mhe. Malima na Mhe. Sitta ili kutafuta suluhisho, basi atakayeshindwa atakuwa ni Bw. Malima. Hili halina ubishi. Jinamizi hilo litamkaba, litamkunja, na kumpa ndoto mbaya mheshimiwa huyo kijana mpaka ajute kwa nini alilipeleka shauri hilo kwenye vikao vya CCM. Akitoka kwenye vikao hivyo ni bora akimbilie kupimwa msukumo wa damu! maana wengi hujihisi wamekimbizwa mchakamchaka na jinamizi hilo. Mhe. Malima atashindwa mbele ya nidhamu ya chama. Nitakuambia kwa nini.
Kwanza kabisa, kwa Mbunge kijana kama yeye kumshtaki mbunge mwenye sifa kama za Sitta ni kujtakia mabaya. Bw. Sitta ana nafasi ya pekee na ya kuonewa wivu. Bw. Sitta kwa kutumia watu mbalimbali ndani ya CCM aliweza kupanga na hatimaye kufanikisha mapinduzi ya kumng'oa Spika mkongwe nchini Bw. Pius Msekwa kitu ambacho watu wengi hawakutarajia ukizingatia umaarufu wa Bw. Msekwa. Kuangushwa kwa Msekwa na baadaye uthatibiti wa Spika kutetea maslahi ya Wabunge kumemfanya Bw. Sitta kuwa gwiji wa mambo ya Bunge. Mtandao uliomsaidia kumweka Sitta madarakani bado una nguvu na kama Bw. Malima alikuwa hajajiandaa kupambana nao (wengi wako kwenye vyombo vinavyosimamia nidhamu ya chama) basi atashangazwa ni jinsi gani watakuja kumtetea Bw. Sitta.
Jambo la pili ni kuwa historia ya Bw. Malima na CCM siyo historia ya mtoto aliyelelewa na kukulia ndani ya Chama. Bw. Malima alitoka chama cha Upinzani ambacho baba yake inadaiwa alishiriki kukiunda na hata kupata kwake nafasi ya kugombea Ubunge CCM kulikuwa ni kwa kubebwa na CCM kwani kwenye kura za maoni alishika nafasi ya tatu. Hivyo, kuna baadhi ya "wakubwa" ndani ya CCM wanaona kitendo cha "ubishi" cha Malima kuwa ni masalio ya roho ile ya upinzani, roho ya kuhoji, na roho ya kukosoa. Kuna baaadhi ya watu wanaweza kumuona Bw. Malima kama siyo "mwenzao" licha ya kuwa na kadi ya chama kimoja nao. Historia hii inaweza kumuumiza kweli Bw. Malima kwani jinamizi hili la CCM halisahau kirahisi hivyo!! Hili jinamizi linakumbukumbu kali kama nini na halichelewi kuiita kumbukumbu hiyo pale inapohitajika.
Jambo la tatu ambalo bila ya shaka litamwangusha Bw. Malima mbele ya jinamizi hilo la CCM ni maneno yake mwenyewe katika barua hiyo. Kwa jinsi ilivyoandikwa barua hiyo "inamshtaki" spika mbele ya viongozi wa juu wa CCM. Kitendo cha Malima kutokukubali maoni na "busara" za Spika na kuacha jambo hili limalizwe kimya kimya na kitendo cha yeye kuendelea kuhoji maamuzi hayo ya spika, kwa viongozi wanaolisimamia jinamizi hilo, Bw. Malima anaonekana mwenye utovu wa nidhamu. Ingawa nia yake ni njema na sababu alizoa zina mvuto wa mantiki, lakini kitendo cha yeye kubishana na spika hadharani na baadaye kuandika barua ya uchongezi dhidi ya spika ni utovu mkubwa wa nidhamu ambao viongozi wa juu wa CCM hawawezi kuvumilia, kufumbia macho, na kutokufuatilia. Hata kama CCM itaamua kurudisha suala hili Bungeni, Bw. Malima ameshatiwa alama na viongozi hao. Kama kulikuwa na nafasi ya Uwaziri au Unaibu nafasi hiyo imepeperuka kwani kumpa nafasi hiyo itaonekana kumzawadiwa kwa kitendo cha kumuumbua spika.
Jambo ambalo Bw. Malima anaweza kufanya ili kujiepusha na jinamizi hilo ni kuondoa mara moja barua hiyo na kukubali usuluhishi wa spika. Akiendelea kung'ang'ania msimamo wake wa kuona kuwa ameonewa na hivyo "kupigania" haki yake mbele ya dubwasha hilo, kwa hakika Bw. Malima atakuwa amejimaliza mwenyewe kisiasa. Sitashangaa wapinzani wakianza kumrushia ndoana!! Pamoja na hayo yote, maajabu duniani hutokea, Daudi alimwua Goliathi! tusishangae kama Bwana Malima akalishinda jinamizi hilo, kwani wanaolisimamia ni binadamu kama yeye!! akijenga hoja vizuri anaweza kulifanya jinamizi litoe machozi na kumsamehe, kwani hata Simba huzaa na kuna mahali niliwahi kuona picha ya simba amepewa kikombe cha chai!! Bw. Malima anaweza kutushangaza. Tusubiri tuone.