Hii extract toka Mwananchi (7/4/2007) ina maelezo ya ziada katika sakata hili.
Wanamtandao wamalizana wenyewe kwa wenyewe
Na Waandishi Wetu
MKAKATI kabambe umesukwa kuhakikisha kuwa Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) ambaye ameonyesha jeuri ya kudharau maamuzi halali ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta anashughulikiwa na hatafurukuta.
Malima, anadaiwa alikaidi uamuzi wa Spika Sitta ambaye alijaribu kumaliza mzozo uliokuwapo kati ya Malima na mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi.
Kutokana na kuibuka kwake katika sakata hilo, kundi mojawapo kati ya yale ya wanamtandao maslahi na wanamtandao matumaini, limekuwa likimtumia kama chambo na hivyo jingine kuapa kumshughulikia ili kusudi kulipiza kisasi kutokana na kile, kundi hilo linachokieleza kuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umegundua kuwa kundi hilo linajumuisha pia baadhi ya mawaziri wa awamu ya nne ambao kwa namna moja ama nyingine wameumizwa na maamuzi ya vigogo wa ngazi za juu na hivyo kujikuta wakiwa na wakati mgumu.
Habari za uhakika ilizonazo Mwananchi Jumapili zimeeleza kuwa upo uwezekano wabunge machachari wanaotoka nje ya mtandao kusimama na kisha kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka Mbunge Adam Malima aadhibiwe na kisha kama kanuni zinavyotaka busara ya Spika itachukua nafasi kwa kuwa katika kanuni za bunge hakuna vifungu vinavyomlinda mbunge huyo.
Malima, ndiye ambaye aliyeanzisha mzozo huo kwa kumshtaki Sitta kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Yusuf Makamba, hatua ambayo tayari wachunguzi wa mambo wanaiona kuwa ni jitihada za kujaribu kumdhibiti spika huyo wa bunge.
Pia, uamuzi wa Malima kuamua kumshtaki Sitta nje ya utaratibu na kanuni za Bunge, nao umesababisha kuibuka kwa maswali mengi miongoni mwa wabunge, ambao baadhi yao wameshaanza kukiona kitendo hicho kuwa ni cha kulidhalilisha kimamlaka bunge hilo.
Hatua hiyo ya wabunge inasemekana kuwa inachukuliwa katika kuhakikisha kwamba wanakomesha kabisa kiburi na dharau iliyoanza kujijenga kwa mbunge huyo na wengine wenye tabia kama yake ingawa kwa upande mwingine mbunge huyo na kundi lake wanaonekana kupambana na wimbi kubwa la wanamtandao.
Kwa mujibu wa Kanuni Namba 51 (1), mbunge yeyote anaweza kuamsha hoja kuwa mbunge aliyekiuka kanuni za bunge asimamishwe ubunge na hatimaye mbunge husika ataitwa kujitetea na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge atawasilisha taarifa za mwenendo wa mbunge na hatimaye hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mbunge husika.
Hata hivyo, kwa namna yoyote ile mzigo wa mzozo huo uliochukua sura nyingi, zikiwamo za udini, uanamtandao na visasi, unaelekea kumwangukia Malima kwa kiasi kikubwa.
Awali, katika maamuzi yake wakati akifunga kikao kilichopita cha Bunge, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, alisema Malima, alishindwa kuthibitisha ukweli wa madai yake dhidi ya Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi kuwa, Rais na Waziri Mkuu, hupewa muda mfupi kwenye televisheni ya ITV wakati wa taarifa ya habari ya saa 2:00 usiku.
Mbunge huyo pia alidai kuwa, wakati viongozi hao wakuu wa kitaifa wakipewa muda mfupi, Mengi ambaye ndiye mmiliki wa kituo hicho cha ITV, hupewa muda mrefu zaidi.
Sitta alisema matamshi hayo ya Mbunge Malima yalikuwa na nia ya kulifanya Bunge liamini maneno yake huku akijua wazi kuwa hakuwa na uhakika wa alichokuwa anakisema.
Maamuzi hayo ya Spika yalikuwa katika kitabu chenye kurasa 32 na alichukua muda wa takriban saa moja kuyasoma.
Alisema ni dhahiri kutokana na ukweli huo, Malima alikiuka kanuni namba 50 (1) inayokataza kusema uongo bungeni na inayomtaka mbunge kuwa na hakika kwamba maelezo anayoyatoa ndani ya chombo hicho, ni sahihi na si mambo ya kubuni au kubahatisha tu.
Tayari, zipo taarifa za uhakika kwamba mbunge mwingine machachari, Chacha Wangwe wa Tarime (Chadema) ameshapanga kuondoa kauli yake dhidi ya spika na hivyo kumuondoa katika orodha ya watakaoadhibiwa katika kikao hiki cha bunge.
Wakati hayo yakiendelea kwa upande mwingine kamati maalumu iliyopanga kula sahani moja na vigogo wa serikali waliohusika na mikataba mibovu ya Richmond, inakutana kesho kulishughulikia suala hilo ipasavyo.
Kabla ya kikao hicho itakumbukwa kwamba kwenye mkutano wa bunge lililopita, suala hilo la Richmond lilitarajiwa kuchomoza, lakini zikafanyika jitihada za nguvu na makusudi na suala hilo likazimwa.
Ni wazi safari hii hoja hii itajadiliwa na Spika Sitta ameshatoa baraka zake zote ili hoja hiyo ifike ndani ya Bunge na kusubiri mjadala mkali.