Barua ya Wazi kwa TMDA: Kushughulikia Dawa Zilizoainishwa Kutofaa kwa Matumizi ya Binadamu

Barua ya Wazi kwa TMDA: Kushughulikia Dawa Zilizoainishwa Kutofaa kwa Matumizi ya Binadamu

Uhakika Bro

JF-Expert Member
Joined
Mar 29, 2022
Posts
3,644
Reaction score
4,315
Mkurugenzi Mkuu

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

S.L.P 1253 Dodoma / 77150 Dar Es Salaam.

Barua pepe: info@tmda.go.tz
Tovuti: www.tmda.go.tz

Yah: PENDEKEZO LA UTARATIBU WA KUSHUGHULIKA NA DAWA ZISIZOFAA KWA MATUMIZI NCHINI

Baadhi ya tafsiri:

Dawa zisizofaa kwa matumizi: Ni zile bidhaa ambazo; zimekwisha muda wake wa matumizi, hazikufungashwa vema, zilozoharibika, au zile ambazo hazijaisha muda wake lakini hazikutunzwa vema, hazikuandikwa vema, zimeainishwa isivyo, zilizo chini ya kiwango, zilizochakachuliwa, zilozopigwa marufuku au zilizozuiwa kutumika.


Uteketezaji: Ni mchakato wa kuzifanya dawa zisizofaa kwa matumizi kwa muda husika wa kibaiolojia na kikemia ili zisiwe zenye kuleta madhara.

Kuchakata-tena (recycling) ni mchakato wowote unaopelekea taka kufanyizwa upya katika bidhaa mpya hivyo kutumika tena na tena kwa dutu ileile. Mfano kuyeyusha chupa mbovu za plastiki kiwandani ili kutokeza viti, meza au hizohizo chupa nyingine mpya.

Kuzungusha-juu-tena (upcycling recycling) ni mchakato unaoelekeana na kuchakata-tena lakini unahusisha zaidi vipengele vya kuchakata tena vya kuitumia taka bila kuibadili (au kwa kuibadili kiasi) kwa matumizi mbadala. Mfano; matumizi ya matairi chakavu kama meza, na ujenzi wa kutumia chupa za maji zilizojazwa mchanga.

Ndugu Mkurugenzi mkuu na watendaji wote walioko kazini TMDA
Habarini za kazi. Hongereni kwa kazi nzuri sana mnazoendelea kutekeleza na kuzidi kuipaisha taswira ya udhibiti wa madawa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mimi ni mtanzania mdau wa madawa, tiba na afya kwa ujumla wake.

Pamoja na kazi kuu ya TMDA kuwa ni kudhibiti dawa zinazozalishwa na kuingia nchini, ikiwamo usajili na uhakiki wa ubora. Kazi ambazo zinafanyika vema. Hilo halitakuwa dhumuni kuu la waraka huu wa leo. Leo nitajikita zaidi katika jambo jingine kabisa japo nalo ni la muhimu sana tu katika kuzilinda afya za walaji (watumiaji, na wasio watumiaji wa dawa). Jambo lenyewe ni uteketezaji wa madawa.

Nilifurahishwa na taarifa iliyoonesha kuwa, sasa TMDA inakwenda kumiliki eneo lenye mitambo ya uteketezaji salama wa madawa yasiyofaa katika eneo la Kibaha. Yaani kichoma-taka 'incinerator'.

Screenshot_20240420-143015_Chrome.jpg


Swali ninalobakiwa nalo ni kwamba je incinerator hiyo imekwishaanza kufanya kazi? Je wadau katika mnyororo wa madawa wanawezaje kuzipata huduma hizo, ni kwa utaratibu upi?

Kumbuka hapa sizungumzii ile hali ya dawa, kuwa imekamatwa kisheria au imezuiliwa kinamna yoyote na TMDA sasa ndio inaharibiwa na taasisi halafu muhusika (aliyekuwa mmiliki wa mzigo wa dawa) ndio anapewa bili. Hapana. Ninahitaji kujua ni kwamba yule mdau mwenye duka la dawa muhimu/famasi au kiwanda mwenye mzigo wa dawa zisizofaa kwa matumizi (taz. Tafsiri) anapohitaji huduma ya kuharibu dawa kupitia nyenzo za TMDA anapaswa kufanyeje? Kufuata utaratibu gani?

Hapa siwazungumzii wenye viwanda au mahospitali makubwa ambao wao kutokana na ukubwa walionao ni rahisi zaidi kutimiza vipengele hasa vya malipo. Uchumi unawaruhusu (Economies of scale). Maana mtu anapoteketeza mzigo wenye uzito mkubwa kama zaidi ya tani moja. Basi gharama zinajifuta hasa katika masuala kama stakabadhi za kupata hasara na kodi za TRA. Na hata bila hivyo mzigo unamruhusu tu. Niishie hapo kwa hao wakubwa. Leo nina hawa wa kati na wadogo ambao kufikisha tani kadhaa za kuteketeza sio rahisi. Tena ni maajabu.

Naomba kuulizia utaratibu mbadala kwa sababu huu uliopo sasa hivi una misukosuko mikubwa sana inayopelekea watu wenye nia za kuteketeza dawa kiusalama kushindwa kutekeleza adhima yao kwa ufanisi.

Ili tuelewane vizuri ninaomba kugusia tu gharama za uteketezaji inayolipwa kama ada kwa NEMC kwa mzigo WOWOTE ulio chini ya tani moja.

Screenshot_20240420-183325_Adobe Acrobat.jpg


Sasa hapo ni NEMC tu bado hujawalipa maofisa wa TMDA, wanausalama(polisi), usafiri na gharama nyingine za kuteketeza. Ukifanya hesabu ya haraka hapo utakuta sio chini ya Milioni mbili na nusu za kitanzania. Sasa je mtu ambaye kwa bahati mbaya aliyeharibikiwa boksi mbili tatu la dawa wanayoita rangi mbili (Amoxicillin 250mg tabs 100 tablets) na vipakiti vya panado/paracetamol katika DLDM yake ataweza kweli kulipia Milioni 2 na zaidi kwa ajili ya uteketezaji? Wamiliki wenye tamaa na waliokosa na uvumilivu ndio wanasababisha hatari kama hizi hapa.
chrome_screenshot_1713627711813.png


Nailaani vikali tabia ya namna hii. Naomba tuzijali afya za viumbe wote nasi tukiwamo tafadhali. Lakini tujiulize, tumefikaje huku?

Sasa huyo ni mtu mwenye biashara yake ya dawa. Lakini lipo pia kundi ambalo ama kwa kutojua au kwa kutozingatia huzitapanya dawa na 'kuziteketeza' katika hali inayohatarisha usalama wa watu wote katika mazingira: Kundi hili ni la watumiaji wote wa dawa za kutibu. Wananchi wote mimi na wewe msomaji.

Tunafahamu kuwa mojawapo ya kanuni bora za ugawaji wa dawa hasa zile zenye viuavijasumu ni kutoa kiwango cha dozi ya mgonjwa husika tu na si zaidi. Yaani kama dozi ni vidonge viwili kumezwa kila baada ya masaa nane kwa muda wa siku saba basi vitatolewa vidonge 21 tu. Utaratibu huu husaidia kupunguza tatizo la usugu wa dawa kwa kutoruhusu madawa kusambaa mtaani bila matumizi mahsusi.

Lakini jambo hili halifanikiwi kila wakati kwa sababu zipo baadhi ya dawa zinazotolewa zikiwa nzima nzima. Mfano mzuri ni dawa za maji za watoto. Mtoto anayehitaji milimita 2.5 kwa masaa nane na yule anayehitaji milimita 5 au 10 za amoxicillin syrup kwa masaa nane kwa siku tano wote hupewa chupa moja (au zaidi) yenye ujazo wa milimita 100;
Huyu wa 2.5ml atatumia 37.5ml na kubakiza 62.5mls za dawa yenye viuavijasumu
Yule wa 5ml atatumia 75mls na kubakiza 25ml za dawa yenye viuavijasumu
Unaweza kuhisi yule wa 10ml ataokoa jahazi? La! Yeye atahitaji 150ml ambapo itabidi apewe chupa mbili kukamilisha dozi, na hivyo ataibakiza nusu chupa kabisa!

Sasa kiutaratibu dawa hazipaswi kutupwa kama taka nyinginezo maana zina athari kibaiolojia, kikemia na kifiziolojia kwa wanadamu na wanyama katika mazingira. Hazipaswi hata kutupwa chooni maana zinaweza kuharibu ikolojia ya mchakato wa kuyeyusha na kumeng'enya takataka. Kwa mfano takataka huhitaji kuvunjwavunjwa na bakteria ambao wanaweza kuathiriwa na viuavijasumu katika madawa wakashindwa kutimiza sehemu yao.

Lakini pia kuachilia madawa katika mazingira kunaweza kuwafundisha vimelea USUGU WA VIMELEA KWA MADAWA na hilo ni janga kubwa. Hupelekea muathirika kushindwa kutibiwa na dawa za kawaida kwa ugonjwa husika. Ni hatari kwa maisha.

Kiufupi tu dawa za majumbani nazo hazipaswi kutupwa hovyo. Lakini, swali linabaki je dawa hizo zilizobaki, au zilizoisha muda wake zikiwa majumbani wazipeleke wapi? Ni mwananchi nani anaweza kulipia milioni mbili, au hata pesa yoyote tu hata ili dawa yake ikateketezwe? Je kuna utaratibu gani wa kuhusu masuala haya?

Kinadharia na inavyofundishwa mashuleni ni kwamba inapaswa dawa hizo azirudishe famasi au hospitali au duka la dawa alikozinunulia ili zikateketezwe kikamilifu. Lakini ni nani mwenye duka anaweza kuweka kampeni ya kuwaambia wateja wake wamletee dawa zote zinazobaki, na makopo ya chupa ili ziteketezwe kiutaratibu. Halafu hizo gharama azilipie nani? Kwa utaratibu uliopo sasa. Kwa kweli ni ngumu sana.

Ndugu Mkurugenzi mkuu, naomba kuwasilisha hayo kama baadhi ya matatizo yaliyopo katika suala zima la uteketezaji salama wa dawa zisizofaa tena kwa matumizi.

Basi wakati tunasubiri majibu ya nini kifanyike kuna mapendekezo / maoni yangu nikiwa kama mdau wa madawa, tiba na usalama wa afya zetu;

1. Kuanzishwa kwa utaratibu vituo vya kukusanyia dawa za majumbani zisizofaa kwa matumizi: Hivi sio lazima viwe vituo maalumu. Vituo vya afya vilivyopo kila wilaya au kata vinaweza kuongeza jukumu hili kama sehemu ya huduma zake.

Kinachohitajika sio vitu vingi bali ni kuwepo kwa kijalala chenye maelekezo ya kukusanyia dawa zisizofaa tena kwa matumizi toka kwa wananchi. Hapo jingine la zaidi litakuwa ni elimu kutolewa sambamba na dawa kwamba dawa zinazobaki utapaswa kukirudisha hospitali/dukani au kwenye kijalala hiki maalumu.

Maduka ya dawa muhimu na famasi zingeweza pia kufanya kazi kama vituo vya kukusanyia dawa zisizofaa tena kwa matumizi. Lakini kwa sasa hapana. Italeta mkanganyiko wa ni dawa ipi imerudishwa na ni ipi imeharibikia dukani(japo hii sio mbaya sana kwa sababu nitakazotoa baadaye). Lakini pia wananchi wanaweza poteza imani kwa kudhani labda dawa hizo wakirudisha watauziwa tena baadaye. Maana uaminifu ni muhimu. Lakini pia elimu ni muhimu.

Basi kuepusha hayo maduka ya madawa yabaki tu kutoa maelekezo ya kwamba dawa inapobaki irudishwe ipeleke kaikusanye hospitali/kituo cha afya kwa ajili ya uteketezaji.

Tukirudi kwenye hayo maduka ya madawa ninapendekeza/maoni ya kwamba;

2. Kuwezeshwa kutokea katikati(centrally orchestrated) ofisi ya TMDA kukusanya dawa zote zisizofaa kwa matumizi kwa ajili ua uteketezaji wa pamoja: uteketezaji wa pamoja ni pale ambapo maduka madogomadogo yenye vimizigo vidogovidogo vya kuteketeza yanapoungana na kukusanya mzigo pamoja kwa kuchangia gharama hivyo kuteketeza kwa pamoja. Hii itasaidia kama kinachoogopwa ni gharama.

Inakuwa kama hisa tu zinakusanywa taarifa za wote na kiasi cha dawa zisizofaaa. Zinapatikana tani kadhaa zinapigwa hesabu za gharama halafu kila mmoja anachangia kulingana na ukubwa wa mzigo wake. Mwishoni kila mmoja anapatiwa cheti chake kutokana na hasara aliyokula ikiwamo gharama alizoingia kutekeleza jukumu hilo kwa ajili ya mahesabu ya mapato.

Lakini kama ukusanyikaji huo unakuwa ni mgumu kutekelezeka basi mbinu inayofuata pia inaweza kutumika;

3. TMDA kufanya utafiti wa gharama za uteketezaji na kisha kuwa yenyewe kwa vyombo vyake inakusanya dawa zisizofaa na kuziteketeza chini ya mifumo yake iliyopo: hapo gharama za uteketezaji wa jumla atalipia mwenye duka kama tu ilivyo katika uteketezaji wa pamoja. Kinachobadilika ni kuwa TMDA inakusanya mojakwa moja dawa hizo na kuzishughulikia baadaye pale mzigo utakaporuhusiwa na uchumi (economies of scale).

TMDA inaweza kuanzisha vituo ambavyo, wamiliki wa maduka wataituma mizigo yao ya dawa zisizofaa hapo. Basi watakadiriwa gharama pamoja na ada zao kwa ajili ya uteketezaji wa pamoja baadaye. Kitu cha msingi tu ni kujitahidi kutumia weledi kiasi ambacho gharama ya mchakato mzima wa kuteketeza kitawiana na tena kitaonesha faida itakayokuja kutokana na msamaha wa kodi ya hasara husika. Hili sio jambo baya kwa wananchi na TRA maana kimsingi hawa wamiliki wa maduka na viwanda vya dawa wanakuwa wamefanya jambo kwa faida ya jamii (public interest) kulinda afya zao. Wanastahili upendeleo huo. Kuweka ugumu hakumsaidii yeyote kuanzia huyo mmiliki hadi huyo mwananchi. Sasa jambo hili lifeli kwa faida ya nani mwingine!?

Ndugu Mkurugenzi Mkuu, ninaamini kuwa ikiwa utaratibu huu utafanikiwa. Basi hata lile tatizo la maduka ya madawa kuchelea kupokea dawa zisizofaa kwa matumizi za majumbani halitakuwepo tena. Kwa nini? Ni kwa sababu dawa hizo zitaingia katika hesabu ya dawa zilizomharibikia dukani na hivyo atapatiwa msamaha wa kodi kwa mzigo wote.

Hapa ndugu mwananchi wote tunakuwa tumefaidika. Dawa zimekusanywa na hivyo kuteketezwa kiufasaha, Mmiliki wa duka amepunguza kiasi mzigo wa hasara binafsi, amefaidika kwa kuifanya kazi ya jamii (public interest), mazingira yamelindwa na afya za walaji zimeimarika kiujumla wake. Yaani ni ushindi hadi mwisho kwa kila muhusika (win win).

Basi ninaomba kutia mkato kwa kuliwasilisha dhumuni hilo kuu la waraka huu mrefu. Sehemu niliyotia mkato ilipaswa kuwa nukta kuu na kuhitimisha barua hii na kutia ile 'Wako katika ujenzi wa Taifa' lakini imekuwa hapana.

Ni kwa sababu tu nina jambo la nyongeza ambalo ninatamani kuliwasilisha pia ndugu Mkurugenzi Mkuu, tafadhali usinichoke.

Jambo lenyewe linalochukua sehemu ya pili ya waraka huu ni suala la kuchakata-tena (recycling and upcycling)(taz. Tafsiri juu).

Nitalielezea kwa ufupi: Katika taaluma ya madawa tunafundishwa kuwa dawa inapoharibika (kuisha muda, kubomoka kinamna fulani) inaweza kuupoteza kabisa uwezo wake wa kufanya kazi husika ki-tiba. Dawa inahitaji kufikia dozi/kiwango fulani mwilini ili tiba ikamilike. Mfano mtu anayehitaji miligramu 10 za dawa hatatibika kikamilifu kwa dawa yenye miligramu 8, 7 au 5 tu za dawa husika. Hivyo kiujumla dawa ikipungua nguvu tunasema ni dawa isiyofaa tena kwa matumizi yake mahsusi.

Tuliache hilo kwanza tuzungumzie viambata-hai(active ingredients) vya dawa. Viambata hivi ndio hufanya dawa iitwe dawa. Mfano acetaminophen 500mg katika panado/paracetamol, au ampicillin 250mg + cloxacillin 250mg katika dawa ya Ampicloxa 500. Dawa inapobadilika na kuwa dawa isiyofaa kwa matumizi inahusisha pia dawa ambazo kwa namna fulani zimepungua nguvu ua viambata-hai vinavyotakiwa. Kuisha muda wa matumizi wa dawa huweza kuikuta dawa ikiwa imepungua nguvu ya viambata hai vyake kwa asilimia kadhaa iwe ni 0.25%, 2%, 5%, 50% au 100% kabisa.

Basi turudi katika nilichoanza kuelezea katika aya mbili zilizopita za nyongeza hii. Nitaanza na swali (kimsingi nyongeza yote ni swali fikirishi yaani 'food for thought'):

Angalizo: Maelezo hapa chini hayajafanyiwa utafiti kamili. Ni 'assumption' na mafikirio ya nje ya boksi lakini bado ni ndani ya boksi la kushughulika na dawa zilizoainishwa kutofaa tena kwa matumizi.

1. Je upo uwezekano wa kuchakata-tena dawa: Yaani dawa yenye viambata hai vya namna fulani, badala ya kuteketezwa basi ikarudishwa kiwandani kisha kutayarishwa upya katika dawa mpya. Utasikia mtu analalamika kwamba "jamani tumefikia kwenye 'dawa za mtumba mweeeh!'". Subiri tafadhali nitoe maelezo.

Lakini ninachojaribu kusema sio kipya kwenye tasnia ya madawa. Kiukweli viambata-hai vyote vya dawa vilivyonunuliwa kwa wingi katika viwanda kwa ajili ya kutengenezea dawa huwa havina muda wa kuisha (expire date). Bali hupatiwa muda hadi kupimwa tena (retesting date) ambapo ukifika zinafanyiwa vipimo (chemical assay) kujua hali yake na ubora wake tu. Kisha huendelea kutumika kulingana na majibu ya kitaalamu. Mf. Unaanza na acetaminophen 5kg ambayo ina ubora wa 100% hii itamiminwa kutengeneza vidonge 10,000 vya paracetamol/panado. Ikifikia kupimwa tena ikawa na 75% basi watamimina kutengeneza vidonge 7,500 tu na inayofuata kama iko na 50% ya acetaminophen basi watatengenezea vidonge 5,000 tu vya paracetamol/panado.

Kama upo uwezekano, Katika makao makuu ya kitengo cha dawa zisizofaa kwa matumizi, kuwepo hatua moja kabla ya uteketezaji wa dawa ambapo uchunguzi unafanyika kuona ni dawa zipi zinaweza kurudishwa kuchakatwa tena. Zitaangaliwa sababu za kiuchumi, kiusalama, na kiafya pia.

Maana kabla hatujawaza kuchakata-tena katika hali ya kawaida (traditional sense) kwa haraka haraka tunaweza kuangazia zaidi kipengele cha kuzungusha-juu-tena. Naomba kutolea mfano (kumbuka hii ni kwa ajili ya mfano tu) kwa dawa mbili za kutiwa mishipani/sindano ampicloxacillin powder for injection na fluconazole injections.

Dawa hizi huwa zimeandaliwa kwa uangalifu wa hali ya juu sana na hazipaswi kuwa na vimelea (sterile) wala kichakachuo cha namna yoyote. Manesi husisitizwa kuwa hairuhusiwi kumchoma mtu ikiwa dawa hiyo itaonesha utofauti mdogo sana kama kutoyeyuka, ukungu, mabonge na rangi isiyo ya kawaida.

Sasa tarehe ya kuisha matumizi mahsusi ya dawa hii mfano (MFANO) huweza kuwa labda ni aidha: 1. (ampicloxacillin powder) mwisho wa kiambata-saidizi kinachowezesha dawa ilowane vema na kuchanganyika na maji ya sindano lakini ampicillin 250mg na cloxacillin 250mg zilizomo bado zinaweza kufikia lengo kwa 99% au yote 100%. 2. (Fluconazole) mwisho wa uimara wa plastiki iliyohifadhiwa kuweza kushikilia uzima wa dawa (integrity) lakini bado iko na fluconazole 200mg.

Dawa hizi zikichukuliwa zikapimwa na kuonekana hivyo au kulingana na asilimia zilizobaki basi zinaweza labda: unga wa ampicloxa ukachanganywa na sukari katika formula ya unga wa dawa ya watoto ya maji ya ampicloxa. Na maji ya fluconazole yakamiminwa na kuvukishwa kupata vidonge au hata kumimina maji hayo hayo katika plastiki mpya na zikapatikana dawa za matone za macho!

Basi ndugu Mkurugenzi mkuu, jukumu la kugawanya kuwa ni dawa ipi iende kwenye A. Uteketezaji, B. Kuchakata tena au C. Kurudisha juu tena.... wafamasia watahusika kwa kiasi kikubwa kwa kutokana na uelewa wao mpana kuhusiana na dawa ikiisha muda wake inageuka kuwa dutu ya namna gani. Haiwezi kutokea kwa dawa ambayo inavunjika kuwa visivyofaa ikahusika na B au C hiyo ni lazima iteketezwe. Lakini pia kujua dawa ipi ikitupwa katika mazingira haitaharibika hivyo ni bora tu irudishwe kwenye matumizi.

Lakini pia itategemea pia maamuzi ya jopo la wanauchumi na wafamasia wa kitengo na viwanda vinavyohitaji malighafi kwa ajili ya kutengeneza dawa. Bongo zote zihusishwe. Na taaluma zote zinazohusika zifanye kazi yake. Ndio maana nikasisitiza ni 'food for thought'.

Mbinu nyingine rahisi katika kuchakata-tena/kurudisha-juu-tena inahusisha kama kawaida: Dawa zisizofaa tena zinakusanywa, zinafanyiwa vipimo kisha zinarudishwa zikiwa na formula inayoelekeza kwamba dawa iko na uwezo upi kwa sasa. Kwa mfano: Mfamasia anapopokea dawa iliyo na maelekezo kuwa dawa ya maji ya watoto Ampicloxa syrup hii ina 50% ya uwezo wake ina maana mtoto aliyehitaji 2.5ml sasa atapatiwa 5mls na yule wa 5ml sasa atapatiwa 10ml. Lakini kama mjuavyo kurahisisha mambo kuna changamoto zake. Busara itumike. Na je tunao wataalamu wenye uwiano wa kutosha kufanya kazi na dawa mojamoja na mgonjwa mmoja mmoja bila kukimbiakimbia kunakoweza kupelekea makosa (medication errors)

Nasisitiza tena kwa maelezo haya marefu ya waraka huu, yote yanaita kwa jambo moja busara ihusike. Je tunaweza kupata utaratibu mbadala kwa uteketezaji wa mzigo mdogo wa dawa?Na pia, Je? ni nani yupo tayari kwa programu ya serikali kuzalisha dawa za mtumba🤨. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. Ninawashukuru sana.

Ndugu Mkurugenzi Mkuu nikutakie kazi njema,

Na pia niwatakieni woote kazi njema.
 
Back
Top Bottom