Travelogue_tz
JF-Expert Member
- Sep 28, 2010
- 855
- 1,224
YAH: MALALAMIKO KUHUSU ZUIO LA USAJILI WA POLYCLINICS (KLINIKI ZA KIBINGWA) MPYA KATIKA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)
Mhe. Waziri wa Afya,
Katibu Mkuu wa Afya,
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,
Sisi, wadau wa sekta ya afya nchini Tanzania, tunakuandikia barua hii kwa nia ya kuwasilisha malalamiko yetu juu ya zuio la kusajili vituo vya kutolea huduma maarufu kama Polyclinic na Specialized Polyclinic au Kliniki za Kibingwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Kuanzia April 2022 NHIF imekua haisajili vituo vipya vya polyclinics bila kutoa taarifa rasmi ya kusitisha usajili wa vituo vipya vya kundi hili''
Hali hii imeleta changamoto nyingi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na pia limeathiri maendeleo ya sekta binafsi ya afya nchini. Tunaelewa nia njema ya serikali katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na vituo hivi ni za kiwango cha juu, lakini tunahisi kuwa zuio hili linaathiri zaidi ya ilivyotarajiwa.
Kumekuwa na kilio cha Wadau katika sekta ya afya juu ya zuio la kusajili Vituo vya kutolea huduma maarufu kama Polyclinic na Specialized Polyclinic au Kliniki za Kibingwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ambapo zuio hilo limelenga Kliniki mpya zilizoanza kutoa huduma mwanzoni mwa mwezi Aprili 2022.
Takwimu za Wizara ya Afya zinabainisha kwamba mpaka kufikia mwezi Machi 2022 kulikuwa na jumla ya Kliniki za Kibingwa 299 ambazo ni sawa na asilimia 3.3 tu ya vituo vyote vya kutolea huduma za Afya Nchini.
Ni zaidi ya miaka miwili imepita bila kuwa na taarifa yeyote rasmi kutoka Wizara ya Afya kuhusu sababu za kutokusajiliwa kwa polyclinics mpya katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kutoa fursa kwa Watanzania kupata huduma bora bila kikwazo chochote, hasa ikizingatiwa Vituo hivyo vinaendeshwa kwa mujibu wa Sera na Miongozo ya Wizara husika, na pia zimekidhi vigezo stahiki.
Kwa mujibu wa chanzo cha Wizara ya Afya, zaidi ya Kliniki za Kibingwa 150 zimekwama kusajiliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya licha ya Vituo hivyo kukidhi vigezo vyote vilivyoainishwa na Mfuko na kwamba baadhi yake vilishafanyiwa tathmini ya vigezo na kuonekana kuwa na sifa za kusajiliwa ili kuhudumia wanufaika wa Mfuko huo, lakini kinyume na matarajio mchakato huo ulisitishwa bila taarifa yeyote kutoka kwa Mamlaka.
Baadhi ya Wawekezaji na Watoa huduma wamedai kwamba baada ya kukamilisha taratibu zote za maombi ya usajili wa Mfuko waliamua kufuatilia maombi yao kupitia Ofisi za Mfuko na kujulishwa kwamba kuna zuio kutoka Wizara ya Afya juu ya usajili wa Polyclinics katika Mfuko wa Bima ya Afya na wanasubiri maelekezo kutoka kwa Mhe Waziri wa Afya.
Wadau waliendelea kupaza sauti zao na kudai kwamba wanadhani Wizara ya Afya imeshindwa kutambua juhudi zinazofanywa na wawekezaji wa ndani kupitia sekta ya afya kwa kuweka zuio bila kutoa taarifa kwa wadau juu ya sababu zake na pengine zuio hilo linalenga kutatua nini, na litadumu kwa muda gani.
Kwa kukizingatia kwamba vituo vinategemea zaidi ya asilimia 70% ya mapato yatokanayo na wanufaika wa Mfumo wa Bima kwa ajili ya uendeshaji, ni wazi kwamba zuio hilo limeathiri kwa kiwango kikubwa uendeshaji wa vituo na kupelekea baadhi yao kusitisha huduma na wengine kuendelea kwa kusuasua.
CHANGAMOTO ZINAZOTOKANA NA ZUIO HILI
Kupungua kwa Upatikanaji wa Huduma:
Zuio la kusajili kliniki mpya linapunguza chaguo kwa wananchi katika kupata huduma za kibingwa. Watu wengi walikuwa wakitegemea kliniki hizi ili kupata huduma za haraka na za kitaalamu, hasa katika maeneo yenye upungufu wa hospitali kubwa.
Kuathiri Uwekezaji katika Sekta ya Afya:
Sekta binafsi ya afya imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha huduma za afya nchini. Zuio hili limepunguza ari ya wawekezaji ambao walikuwa na mpango wa kuanzisha vituo vipya. Hii inaweza kusababisha kudumaa kwa ukuaji wa sekta hii muhimu.
Kukwaza Ubunifu na Uboreshaji wa Huduma:
Polyclinics nyingi zinatoa huduma maalum ambazo hazipatikani kwa urahisi katika hospitali za umma. Kuendelea kuwepo kwa zuio hili kutazuia ubunifu na ubora wa huduma za afya, kwani kliniki hizi mara nyingi huleta teknolojia mpya na njia bora za matibabu.
Kuongeza Msongamano wa Wagonjwa katika Hospitali za Umma:
Kutokana na zuio hili, wagonjwa wengi sasa wanalazimika kwenda kwenye hospitali za umma, hali inayosababisha msongamano na kupelekea kushuka kwa ubora wa huduma kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji kuhudumiwa.
Kuua uwekezaji wa ndani katika secta ya afya
Ni dhahiri kwamba zuio hili limeathiri uwekezaji na wawekezaji kwa kuwa uwepo wa Bima ya Afya na Uhaba wa huduma za Afya ilikuwa moja ya kivutio vilivyochochea uwekezaji katika sekta hii. Inatajwa kwamba kiwango cha chini cha gharama za uendeshaji wa polyclinics zinakadiriwa kufikia Tsh. Milioni Kumi kwa mwezi , ambapo kutokana na kukosekana kwa huduma ya NHIF vituo husika vimekuwa vikihudumia wagonjwa wasiozidi watatu (3) kwa siku licha ya Watanzania wengi kuendelea kupata adha ya msongamano wakati wa kupata huduma katika Vituo vilivyosajiliwa na Mfuko wa Bima ya Afya.
Aidha tathmini imebainisha kwamba katika kipindi chote cha zuio, Polyclinics zimehudumia wagonjwa kwa kiwango cha chini ya ufanisi unaokadiriwa kufikia asilimia 90-97% licha ya kutumia kiasi cha takribani Tsh. Bilioni 18 kwa mwaka kugharamia malipo ya mishahara, kodi ya pango, kodi za kimamlaka na gharama nyingine za uendeshaji, ambapo gharama hii ni nje ya ile iliyotumika kufanya uwekezaji.
Kuendelea kwa zuio hili, inaweza kupelekea takribani Watanzania wasiopungua kumi (10) kwa kila polyclinic kupoteza ajira zao pale ambapo Vituo vitasitisha kutoa huduma, na hivyo kutengeneza ukosefu wa ajira wa takribani watumishi 1500, kiwango ambacho ni kikubwa sana ukizingatia hali ya upatikanaji wa ajira na changamoto zake.
Zaidi, imethibitika kwamba zuio hili linawanyima wanachama wa Mfuko wa NHIF fursa ya kupata huduma bora, za kibingwa , kitendo ambacho ni kinyume na sera na jitihada za serikali kuhakikisha huduma bora zinafikia wananchi.
MAPENDEKEZO YETU
Kufanya Mapitio ya Zuio:
Tunapendekeza zuio hili litazamwe upya kwa kuzingatia athari zake kwa sekta ya afya na kwa wananchi wanaotegemea huduma za kliniki hizi.
Kuweka Vigezo na Masharti Badala ya Zuio:
Badala ya zuio kamili, tunaomba serikali iangalie uwezekano wa kuweka vigezo na masharti maalum ya kuhakikisha kliniki hizi zinafanya kazi kwa viwango vinavyokubalika. Hii itahakikisha ubora bila kuathiri upatikanaji wa huduma.
Kuhusisha Wadau katika Maamuzi:
Tunaomba serikali iweke utaratibu wa kuwashirikisha wadau wote katika sekta ya afya kabla ya kufanya maamuzi makubwa kama haya. Ushirikishwaji wa wadau utasaidia kupata mawazo mapya na suluhisho bora kwa changamoto zinazokabili sekta hii.
Mwisho policlinic zilizozuiwa zipewe bima ili ziendelee na utoaji huduma ya afya wakati mapendekezo tajwa yakifanyiwa kazi ili isiathiri uwekezaji.
HITIMISHO
Ni matumaini yetu kwamba uwepo wa Vituo vingi vya kutolea huduma za Afya Mathalani Kliniki za Kibingwa ambazo zimesajiliwa na Mfuko wa NHIF itakuwa ni fursa kwa Mfuko katika kuboresha huduma kwa wanachama wake, na hivyo kuvutia Makundi mengi zaidi kujiunga, na hatimaye Ukuaji wake. Uwepo wa huduma bora, na za uhakika kwa Wananchi utasaidia kufanikisha adhma ya Serikali ya kuwa na Bima ya Afya kwa Wote. Hivyo basi tunatoa wito kwa Wizara ya Afya kuingilia kati ili kunusuru hali hii mbaya, na hivyo kuinua hari na matumaini kwa wawekezaji wazawa, watumishi wa sekta ya afya na wananchi kwa ujumla.