Atukuzwaye
Senior Member
- Oct 5, 2026
- 191
- 250
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza rasmi marekebisho ya kanuni yaliyopunguza kwa kiasi kikubwa utitiri wa tozo na ada ambazo zimekuwa zikitozwa wasanii na wadau wa sekta ya sanaa nchini kwa mwaka, ikiwa ni utekelezaji wa mabadiliko yaliyofanywa na Bunge ili kuimarisha usimamizi na kukuza uchumi wa wasanii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Edward Buganga, ameeleza kuwa kanuni hizo mpya tayari zimeanza kutumika na zinalenga kulinda wasanii, hadhira, watoto, na urithi wa sanaa bila kuzuia ubunifu, huku zikiwahusisha makundi mbalimbali yakiwemo ya wasanii huru, vikundi vya sanaa, ma-DJs, washereheshaji, maproduza, mameneja, waandaaji wa matukio, studio, vyombo vya habari, na wamiliki wa kumbi.
Katika muundo huo mpya wa ada, msanii huru sasa atajisajili na kuhuisha kibali chake kila mwaka kwa kulipa Shilingi 10,000 pekee badala ya Shilingi 40,000 za awali, wakati usajili na uhuishaji wa vibali vya vikundi vya sanaa umepunguzwa kutoka Shilingi 60,000 hadi Shilingi 30,000 kwa mwaka.
Aidha, waandaaji wa matukio ya sanaa wametakiwa kuomba vibali kupitia mfumo wa kidijiti wa AMIS siku 30 kabla ya tukio, ambapo vibali hivyo sasa vitatolewa bure kabisa ili kuwezesha wataalamu wa baraza hilo kutoa mwongozo wa usalama na ufanisi.
“Hapa tunasisitiza waandaaji wa matukio ya sanaa wawe na vibali ili wataalamu wetu wawasaidie kuwapa mwongozo wa kwenda vizuri na kibali atapata bure, akikiuka tutamchukulia hatua,” alisema.
Buganga amesisitiza kuwa kanuni hizo mpya zimeweka misingi thabiti ya usimamizi katika mikoa na wilaya, ulinzi wa watoto, maadili, pamoja na udhibiti wa matumizi ya sanaa za jadi kwa madhumuni ya kibiashara ili kuhakikisha mapato yanayopatikana yanarejeshwa kwa jamii husika zinazomiliki urithi huo.
Pamoja na hayo, wasanii wanaotoka nje ya nchi au kwenda nje kwa ajili ya maonesho wametakiwa kufuata taratibu rasmi za kupata vibali vya BASATA, huku shughuli za mafunzo au ubadilishanaji ujuzi wa kidiplomasia zikiwekewa utaratibu maalum wa kutozwa ada.
Amesisitiza maadili kwenye kazi za sanaa akisema kazi za sanaa hazipaswi kuchochea vurugu, ubaguzi, unyanyasaji au kukiuka sheria na badala yake sanaa inaweza kuelimisha, kukosoa, kuonya na kuelekeza jamii na kwamba ukosoaji wa kijamii si kosa iwapo unazingatia sheria na maadili.
Akizungumzia ulinzi wa sanaa za jadi, amesema matumizi ya sanaa za jadi kwa madhumuni ya kibiashara nje ya muktadha wa jamii husika yatahitaji kibali cha BASATA.
Amesema hatua hiyo inalenga kulinda urithi, utamaduni na haki za jamii zinazomiliki na kurithisha sanaa hizo na kwamba mapato yatakayopatikana kupitia matumizi ya sanaa jadi yatarejeshwa kwa jamii husika kwenye eneo la sanaa.