Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Aidha , amesisitiza kuwa, hatua za kinidhamu ndani ya CCM hazipaswi kufanywa kwa mzaha kwa kuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aoitahadharisha bila CCM imara nchi itayumba.
Bashungwa alisema hayo Septemba 2, 2026 alipozungumza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika mkoani Kagera, ambapo alisema uamuzi hauo unaonesha uimara wa Chama katika kusimamia nidhamu na kuhakikisha kila mwanachama anazingatia katiba, kanuni na maslahi ya Chama na taifa badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Bashungwa aliwataka wanachama wa CCM kuunga mkono uamuzi wa NEC, akisema kufanya mzaha katika masuala ya nidhamu kunaweza kuhatarisha uimara wa Chama ambacho kimejengwa kwa misingi imara kwa muda mrefu na inapaswa kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Alisema CCM sio mali ya viongozi au wanachama waliopo madarakani kwa wakati mmoja, bali ni taasisi inayopaswa kuendelea kuwa imara kwa vizazi vijavyo, hivyo kila mwanachama ana wajibu wa kuhakikisha heshima na misingi ya Chama inalindwa.
Bashungwa alirejea kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyowahi kusema wakati akiondoka kwenye uongozi kwamba licha ya yeye kung’atuka, bado aliamini kuwa CCM madhubuti ni muhimu kwa sababu bila CCM madhubuti nchi inaweza kuyumba.
Kwa mujibu wa Bashungwa, kauli hiyo bado ina umuhimu mkubwa katika kipindi cha sasa kwa sababu uimara wa CCM unategemea nidhamu, kuheshimu Katiba na kuhakikisha wanachama wanaweka mbele maslahi ya Chama na taifa.
Alisema hatua zilizochukuliwa na NEC Agosti 26, 2026, zinapaswa kutazamwa katika muktadha wa kulinda ya Chama na sio hatua dhidi ya mtu binafsi, akisisitiza CCM inapaswa kuwa na uwezo wa kuchukua hatua pale inapobidi.
“Tunapokuja kwenye suala la kuchukua hatua za kinidhamu, huwa halina mzaha. Uimara wa Chama chetu ndio uimara wa serikali yetu,” alisema Bashungwa, akieleza umuhimu wa wanachama kuheshimu utaratibu ndani ya Chama.
Aidha, Bashungwa alitoa wito kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kukataa siasa za chuki na mgawanyiko, akisema tofauti za kisiasa na kimawazo ni jambo la kawaida katika demokrasia na hazipaswi kutumika kuvuruga mshikamano wa taifa.
Alisema CCM itaendelea kuamini kuwa watu wanaweza kuwa na mitazamo tofauti ya kisiasa, lakini tofauti hizo hazipaswi kugeuzwa kuwa chanzo cha chuki, migawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano uliopo ndani ya jamii.
Naye, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera Ndg. Faris burhan alionya dhidi ya watu wanaotumia siasa za chuki, propaganda na mgawanyiko kama njia ya kutafuta madaraka, akisema mikakati hiyo inaweza kuleta madhara kwa jamii na kudhoofisha mshikamano wa wananchi.
Kwa kutumia mfano wa safari ya watu ndani ya mtumbwi mmoja, Bashungwa alisema wanachama wa CCM wanaweza kufananishwa na wasafiri waliopo kwenye chombo kimoja, hivyo mmoja akiamua kukichoma chombo hicho anahatarisha maisha ya wote waliomo ndani yake.
Soma Pia: Dkt. Emmannuel Nchimbi afukuzwa uanachama wa CCM
Alisema katika mazingira kama hayo, chama kina wajibu wa kumwondoa mtu anayehatarisha safari ya pamoja na kumrudisha nje ya chombo hicho ili wengine waendelee na safari yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo haimaanishi kumtupa mtu baharini bali kumrudisha kwenye nafasi ambayo hatahatarisha safari ya chama.
Kwa upande wake Mjumbe wa NEC kutoka mkoa huo, Karim Amri
alisema kuwa historia ya CCM imewahi kushuhudia kuondoka kwa viongozi na wanachama mbalimbali wenye majina na ushawishi mkubwa, lakini chama kiliendelea kuwepo kwa sababu ya imani iliyojengeka miongoni mwa wananchi na misingi yake ya kisiasa.
Alisema CCM itaendelea kuwa imara ikiwa wanachama wake wataweka mbele nidhamu, umoja, Katiba na maslahi ya taifa, huku akiwataka Watanzania kukataa siasa za chuki na mgawanyiko na kuhakikisha tofauti za kisiasa hazivunji mshikamano wa taifa.
===