Habari hii pia iko katika Nipashe ya leo kama ifuatavyo:-
Takukuru yatesa Waziri Burian
Na Waandishi wetu
Maofisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha, wamewatia mbaroni wapambe wa mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini (CCM), Dk. Batilda Burian.
Hatua hiyo dhidi ya wapambe wa Dk. Burian ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), inaamsha hofu ya jinamizi la rushwa ya uchaguzi, ambayo imekuwa ikiwaandamana wagombea wa CCM tangu kwenye mchakato wa kura za maoni.
Wakati wa kura za maoni ndani ya CCM zilizofanyika Julai, mwaka huu, wagombea kadhaa na wapambe wao walidaiwa kujihusisha na rushwa walikamatwa na kuhojiwa na baadhi wamekwisha kufikishwa mahakamani.
Miongoni mwa kesi zilizoko mahakamani ni pamoja na mwanasiasa mkongwe na ambaye amekuwa Waziri katika serikali tangu uhuru, mbunge wa zamani wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai.
Pia ipo inayomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela. Makada hao walishitakiwa pamoja na viongozi wengine wa UVCCM mkoani Iringa. Kuna kesi nyingine mkoani Tanga.
Katika tukio la wapambe wa Dk. Burian, NIPASHE ilibaini kuwa walikamatwa juzi saa 2:30 usiku, wakila nyama choma eneo la Cet Garden, iliyopo kwa Mrefu jijini hapa.
Walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa watu waliotambulika kuwa maofisa wa Takukuru, walifika katika eneo hilo, wakawaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwahoji.
Ilielezwa kuwa baada ya kuwahoji waliwaingiza ndani ya magari matatu waliokuwa nayo, aina ya Toyota Land Cruiser na Toyota RAV 4 mbili, kisha waliondoka nao.
Mashuhuda hao walisema kuwa, tukio la kukamatwa kwa wapambe wa Dk. Burian halikufanyika kirahisi, kwani maofisa wa Takukuru walipata tabu wakati wa kuwakamata, hali iliyozusha purukushani.
Walisema wakati purukushani hizo zikiendelea, gari moja linalodaiwa kutumiwa na Dk. Batilda katika kampeni, likifika eneo hilo, lakini ghafla liligeuza na kuondoka kwa mwendo kasi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari lengo la wapambe hao wa Dk. Burian kuwepo mahali hapo halikujulikana mara moja.
Lakini kilichoshuhudiwa ni kwamba baada ya kufika, waliagiza aina tofauti za bia, kilo nne za nyama ya kuchomwa.
Miongoni mwao walisikika wakiagizia nyama ya kuku, mbuzi na ng'ombe.
Taarifa zaidi zilidai kuwa baada ya kupata huduma ya nyama choma na vinywaji, wapambe hao waliketi na kuanza kula na kunywa kabla ya kuzingirwa na kukamatwa.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vilidai kuwa baadhi ya watu waliokuwa katika mjumuiko huo, walisika wakishukuru kwa hatua ya kukutanishwa na kupongezwa kwa kazi nzuri wanayoifanya, ingawa haikujulikana.
"Ghafla tuliona wanakamatwa huku wengine wakikataa…walikuwepo wanawake na wanaume," mmoja wa watoa taarifa alieleza.
Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Arusha, Ayub Akida, alisema hana taarifa za kukamatwa kwa wapambe hao, licha ya habari hizo kuenea karibu kila kona jijini hapa.
NIPASHE ilipofika ofisini kwake kupata ufafanuzi, ofisa mmoja aliwataka waandishi wetu kusubiri, lakini aliporejea kutoka katika ofisi inayoaminika kuwa ya Akiba, alisema Kamanda huyo hakuwepo ofisini.
Kwa mujibu wa ofisa huyo ambaye jina lake halikupatikana, Akiba alikuwa anashiriki kikao maalum.
"Kamanda yupo kwenye kikao maalum cha muda mrefu, na hata chakula tutampelekea humo humo ndani, hivyo hata mkikaa hapa hamtapata nafasi ya kumwona, labda mpigieni simu kama atapokea," alisema ofisa huyo.
NIPASHE ilimpigia simu Akida na baada ya kupokea, aliulizwa kuhusu tukio hilo na kujibu kuwa bado hajapata taarifa hiyo.
Madai ya kukamatwa kwa wapambe hao na hali ya kusitasita kutoa taarifa zao kwa vyombo vya habari, imechukuliwa tofauti na tukio kama hilo lililotokea kwa wapambe wa aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Felix Mrema.
Wapambe hao walikamatwa wakiwa ndani ya nyumba moja iliyopo mtaa wa Sombetini wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Baada ya wapambe hao pamoja na Mrema kukamatwa, taarifa zao zilitolewa asubuhi na Akida, hali ambayo safari hii imekuwa kinyume chake.
Hata hivyo, Dk. Batilda alipopigiwa simu na waandishi wa habari, alithibitisha kukamatwa kwa wapambe wake.
Alisema kuwa baada ya kuhakikisha juu ya kukamatwa kwa wapambe hao, alimpigia simu Kiongozi wa juu wa Takukuru (hakumtaja) na kuuliza kosa walilofanya.
Dk. Batilda alisema baada ya kupata jawabu la `bosi' wa Takukuru, alimwambia kwamba wapambe wake walikuwa katika kikao cha ndani na kitendo cha kuwakamata kilikuwa sehemu ya mikakati yenye lengo la kumharibia kampeni zake.
"Baada ya kuwaambia hivyo, maofisa hao wakaelewa na kuwaachia," alisema Dk. Batilda
Hata hivyo alidai kuwa wakati huo wanakamatwa, yeye hakuwepo katika eneo hilo na badala yake alipigiwa simu.
Mgombea huyo wa ubunge alidai kuwa wapambe hao hawakuwa katika eneo lililotajwa, yaani baa ya Cet Garden, bali nyumbani kwa mmoja wa wanachama wa CCM ambaye hakumtaja.
CHANZO: NIPASHE