kiboko ya makonde
Member
- Jun 26, 2014
- 48
- 15
Kwa mara ya kwanza kituo cha BBC ambacho kinarusha vipindi vyake moja kwa moja London toka mwaka 1957 hadi sasa hivi wakati naandika uzi, kwa sasa matangazo yatakuwa yanarushwa dsm Tnzania kwa mara ya kwanza, wandugu mnaonaje,je kiswahili kinakuwa au kinatupwa
CHANZO: Mwananchi
BBC Swahili yafungua ofisi za kisasa nchini
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Ni kwa ajili ya kuhudumia nchi za Afrika Mashariki kupitia redio, simu na tovuti.
Dar es Salaam. Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), limefungua ofisi zake jijini hapa kwenye Jengo la Tangaza, Mikocheni, zenye vifaa vya kisasa vilivyogharimu Dola 1 milioni za Marekani.
Akizungumza katika uzinduzi wa ofisi hizo mwishoni mwa wiki, mhariri wa BBC Africa, Solomon Mugera alisema: "Kwa hakika ni jambo la kujivunia kwa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, kwa sababu ni moja ya idhaa za kimataifa zinazopendwa kutokana na ufanisi wake mkubwa."
BBC imefungua ofisi hiyo kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki kwa matangazo yote ya redio, tovuti na huduma ya habari katika simu za mkononi kupitia Idhaa ya Kiswahili. Alisema wakati mashabiki wa BBC nchini wakisherehekea ujio wa Amka na BBC, wasikilizaji wa Kenya watakuwa wakipokea matangazo ya Dira ya Dunia pamoja na Leo Afrika yanayohama kutoka London, Uingereza.
"Kimsingi Idhaa ya Kiswahili itakuwa imetua nyumbani na kukamilisha safari ndefu ya zaidi ya maili 4,000 na miaka 57 tangu ilipozinduliwa jijini London, wakati huo kuhudumia miliki za Kikoloni. Idhaa ya Kiswahili ilisikika hewani kwa mara ya kwanza Juni 27, 1957," alisema.
Mugera alisema uzinduzi huo ulifanyika wakati nchi zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara zikipigania uhuru. Ulikuwa mwaka wa mabadiliko makubwa ya kisiasa.
Ghana ilikuwa ya kwanza katika eneo hilo kujinyakulia uhuru wake na kuharakisha mchakato huo katika maeneo mengine. Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilikuwa mstari wa mbele kuripoti harakati za ukombozi na sherehe za uhuru Tanzania (wakati huo Tanganyika), Uganda, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi. Uhodari wa idhaa hii kuripoti kwa kina na kutangaza, umedhihirika wakati wa matukio mbalimbali, yakiwamo ya mashambulio ya mabomu katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania Agosti 1998.
Vita ya Kagera
"Kabla ya hapo, nani atasahau vita vya mwaka 1979 kati ya Tanzania na Uganda? Hapo ndipo Iddi Amin alipojaribu kuvamia Tanzania akipania kunyakua sehemu ya ardhi yake. Ugomvi kati ya Amin na Rais wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ulimalizika kwa mtutu wa bunduki. Wanajeshi wa Uganda walizidiwa nguvu, Amin akakimbilia uhamishoni, akianzia Libya na hatimaye Saudi Arabia hadi alipofariki dunia.
"Bila shaka hilo lilikuwa tukio kubwa katika historia na siasa, siyo tu ya Afrika Mashariki bali ya dunia nzima. Ni kwa sababu hiyo, Idhaa ya Kiswahili iliwakutanisha watoto wa kiume wa marais wawili (Mwalimu Nyerere na Amin) kwa mara ya kwanza tangu mzozo wa mwaka 1979," alisema.
Safari ya mtoto wa Amin
"Mtoto wa Amin, Jaffar, alisafiri takriban kilomita 500 kutoka Arua, Kaskazini mwa Uganda kukutana na mtoto wa Nyerere, Madaraka, anayeishi Butiama. Walikumbatiana huku wakazi wa Butiama wakishangilia," alisimulia.
Mugera alisema Idhaa ya Kiswahili inajulikana kwa ustadi wake katika kufuatilia na kufichua ukweli wa mambo. Mwaka wa 2008 ulighubikwa na matukio mengi ya mashambulio ya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini (albino), baadhi yao waliuawa.
Kwa mara ya kwanza katika matukio hayo, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Vicky Ntetema aliwasaka waganga wa kienyeji walioahidi kumpa damu ya albino, nywele, miguu na viganja kwa Dola 2,000 za Marekani. Walidai viungo hivyo vinaweza kutumika kutengeneza dawa ya kuwapa watu utajiri.
Habari hiyo ilisambaa sehemu mbalimbali duniani na kuzua hamasa kuhusu hatima ya albino. Serikali ya Tanzania ilianzisha uchunguzi na polisi wakaamuriwa kuchukua hatua za kuwasaka, kuwakamata na kuwafungulia mashtaka washukiwa. Tangu wakati huo mauaji ya albino yalipungua.
Ni wazi kwamba ukitaka kumhudumia vyema mteja wako, lazima ufahamu vizuri mahitaji yake. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2010, Idhaa ya Kiswahili ya BBC ilifahamu kwamba wasikilizaji wake walikuwa na tamaa ya kupata taarifa na jukwaa la kujadiliana.
Kwa kushirikiana na Radio One, pamoja na Radio Free Africa (RFA), Idhaa ya Kiswahili ya BBC iliandaa matangazo maalumu kwa saa 14 kila siku kwa muda wa wiki moja kutoa taarifa, uchambuzi na kuandaa farashani kwa wasikilizaji wa Tanzania na duniani kote. Pia katika kipindi cha miaka 20, kumekuwapo wahariri wanne katika idhaa hiyo, kuanzia Kari Blackburn, Tido Mhando, Solomon Mugera na Ali Saleh. Haupiti mwaka bila kufanya jambo kubwa na la kusisimua.
"Idhaa ilikuwa ya kwanza kuhamisha baadhi ya huduma kwenye eneo la utangazaji mwaka 2006. Sherehe za miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ‘zilipeperushwa' kwa redio na televisheni kutoka Dar es Salaam," alisema Mugera.
CHANZO: Mwananchi